By DORIS MALIYAGA
SIMBA imetamba kuwa Yanga ikipona
sana kwenye mechi ya watani wa jadi Jumapili itakula mabao 3-0. Lakini Yanga
wamejibu kwamba kama ikitokea hivyo watavunja timu.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix
Minziro ametamka kwamba wachezaji kama; Athumani Idd ‘Chuji’ na Mnyarwanda
Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ wamepania kuwaziba midomo Simba hasa kocha wao
msaidizi, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, ambaye amekuwa akiwapiga vijembe.
Yanga, ambayo imejificha kisiwani
Pemba ikiwa na wachezaji wake wote akiwamo, Salum Telela aliyekuwa majeruhi na
jana Jumatatu walipofika tu kutoka Dar es Salaam, walifanya mazoezi ya nguvu
mchana kweupe, kuanzia saa sita hadi saa nane kwenye Uwanja wa Gombani.
Minziro alisema: “Tunatengeneza timu
sehemu zote ili siku hiyo, kila mchezaji awe fiti. Tulishinda mechi na Kagera
Sugar (2-1) kulikuwa na upungufu kadhaa ambao pia tunayafanyia kazi, lakini
siwezi kuuweka wazi ni siri yetu.”
“Tumezisikia tambo za Simba na Julio
(Jamhuri Kihwelo) wanaongea tu, lakini wafahamu kuwa mpira dakika 90, hiyo
kauli yao ya kuwa watatufunga mabao 3-0, mimi nasema wakifanya hivyo tunavunja
timu, hivi timu yenyewe ipo wapi ya kutufunga?” Alisema Minziro kwa kujiamini.
“Atambue kuwa, hao wachezaji
anaowatajataja kama, Chuji na Niyonzima ni kama amewachochea, wameupania
vilivyo mchezo huo, watamwonyesha soka la uhakika hadi ashangae, ataona
mwenyewe. Sisi ni watendaji tu, hatutaki maneno mengi, ninachowaambia mashabiki
wa soka hasa wa Yanga, wafike kwa wingi kushuhudia kikosi chao kitakavyofanya
vizuri,” alisema Minziro.
Akizungumzia sababu ya kufanya
mazoezi jana Jumatatu mchana, Minziro alisema programu yao ni kama kawaida,
lakini ni kwa sababu walifika muda huo na jioni kulikuwa na mechi.
Yanga msimu uliopita kwenye mechi ya
mwisho iliifunga Simba mabao 2-0 ikiwa imetokea kwenye kambi hiyo hiyo ya
Pemba.
Wiki iliyopita Julio alitamba kikosi
chao kitawafunga Yanga mabao 3-0.
No comments:
Post a Comment