KOCHA wa Azam FC, Stewart Hall ameipa
Yanga asilimia 90 ya kuibuka na ushindi katika pambano la Ligi Kuu Bara dhidi
ya hasimu wake Simba litakalopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Pambano hilo ambalo kwa kiasi kikubwa
limetawala mazungumzo ya mashabiki wa soka nchini, litafanyika wakati
ambao, Simba ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 18, wakati Yanga
ipo nafasi ya nne na pointi zake 15.
Hall alisema: “Bila kuficha
ukiniuliza nani ataibuka na ushindi Jumapili bila wasiwasi nitakwambia asilimia
90 Yanga itashinda, Simba ina asimilia 10 tu.
“Unajua kwanini? Yanga ina wachezaji
bora zaidi lakini kubwa ni kwamba wamekaa pamoja kwa muda mrefu tofauti na
Simba ambayo ndiyo kwanza inajengwa hivyo inahitaji muda.”
“Nakupa mfano, mabeki wawili wa kati
wa Yanga yule Kelvin Yondani na Cannavaro (Nadir Haroub) wana uzoefu mkubwa na
wamekaa pamoja kwa muda mrefu, ukija pembeni David Luhende ni kijana mdogo
lakini amepevuka, Mbuyu Twite ni mchezaji bora,” alisema Hall.
“Nenda katikati Yanga ina Athumani
Iddi, Haruna Niyonzina hawa ni wachezaji mahiri kabisa sidhani kama Simba ina
wachezaji wanaoweza kulingana nao. Nataka unielewe kwamba nimezitazama hizi
timu msimu huu mara mbili kila moja, hivyo nimebaini uzuri na upungufu wao.
“Ukiwatazama mabeki wawili wa kati wa
Simba utagundua bado hawajazoeana sawasawa kama wale wa Yanga, kwa kifupi Simba
ya sasa ni kama Azam yangu, kuna vijana wadogo wazuri lakini wanatakiwa
kujifunza polepole kabla ya kuwa wachezaji wa kutegemewa,”aliongeza.
Lakini beki wa Simba, Joseph Owino
amesikia maoni ya kocha huyo akamjibu kwamba wako vizuri na mechi hiyo haina
mwenyewe.
“Kwa upande wetu tupo vizuri, mimi na
mwenzangu, Kaze (Gilbert) hakuna shida tumekamilika, lakini mechi yetu na Yanga
kulingana na uzoefu wangu wa miaka mingi, hadi sasa haitabiriki, nimewaona
Yanga wanavyocheza ukilinganisha na sisi tunavyocheza nashindwa hata kutabiri
naona atakayelala vizuri na kuamka na bahati atashinda,”alifafanua.
Chanzo: Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment