Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la kwanza lililofungwa
na Mrisho Ngassa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar jana
Jumapili.
By VICKY
KIMARO
YANGA wamekodi ndege tatu ndogo
kupeleka kikosi chake katika Kisiwa cha Pemba kujiandaa na mechi dhidi ya
Simba.
Pambano hilo la watani la jadi ambalo
litachezeshwa na mwamuzi mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa),
Israel Nkongo litafanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumapili ijayo.
Yanga, iliondoka jana Jumatatu
asubuhi ikiwa na wachezaji 28 kwenda kisiwani Pemba pamoja na viongozi na
benchi la ufundi lenye watu wanane.
Aliyeongoza kikosi hicho ni Mjumbe wa
Sekretarieti ya Yanga, Patrick Naggi, ambaye ni raia wa Kenya.
Wakati Simba wakiwa bado kwenye kambi
yao ya siku zote Bamba Beach, Dar es Salaam, Yanga walitua Pemba mchana na
kuingia moja kwa moja kujifua kwenye Uwanja wa Gombani. Yanga walianza kujifua saa
sita mchana huku kukiwa na jua kali, kuhakikisha kuwa wanakuwa fiti katika
mchezo huo wa Jumapili.
Naggi, ambaye anaandaliwa kuwa Katibu
Mkuu Yanga aliliambia Mwanaspoti kuwa kuanzia leo Jumanne, kikosi chake
kitakuwa kinafanya mazoezi mara mbili kwa siku ili kujiweka sawa kwa mchezo huo
unaosubiriwa kwa hamu kubwa.
“Wachezaji wote tumekuja nao kasoro
Salum Telela, yupo kwenye matibabu maalumu, aliumia tukicheza na Mbeya City,
lakini wengine wote wapo vizuri tunachokifanya ni kuwajengea uwezo wa uwanjani
na kisaikolojia,” alisema Naggi.
Hata hivyo Mwanaspoti jana Jumatatu
jioni lilifuatilia habari za mchezaji huyo na kuarifiwa kwamba naye amejiunga
na wenzake katika msafara huo.
“Mechi ya Simba ni presha kubwa, hawa
ni watani wetu hakuna timu ambayo inapenda kufungwa, kila timu inataka heshima
na ujue kupata pointi tatu kwa Simba zinakuwa tamu zaidi kuliko za timu yoyote,
na inajenga heshima pia.”
Naye Ofisa Habari wa Yanga, Baraka
Kizuguto alipoulizwa kuhusu gharama ambazo Yanga wametumia kukodi ndege hizo
ndogo alisema: “Ndege zimeshughulikiwa na watu wengine tofauti nje ya viongozi,
hakuna yeyote kati yetu anayeweza kujua gharama halisi zilizotumika.”
Hata hivyo, Mwanaspoti linajua kuwa
Yanga imetumia Sh milioni tano kwa ajili ya gharama ya ndege hizo tatu.
Yanga ilipoifunga Simba mabao 2-0
katika mchezo wa kufunga msimu uliopita Mei 18, mwaka huu ilikuwa imetokea
kuweka kambi Pemba.
Katika hatua nyingine, Naggi alisema
ratiba ya Ligi Kuu Bara inaumiza timu kwa vile mechi zimefuatana kitu ambacho
kinapoteza morali ya wachezaji.
“Tuna mechi tarehe 20, halafu
tunacheza tena tarehe 23 halafu 26 na tarehe 3 mwezi ujao, kwa kawaida mwili wa
binadamu viungo vinakaa sawa baada ya saa 72, lakini kwa ratiba hiyo kiafya si
vizuri, “ alisema.
Chanzo: Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment