Saturday, October 19, 2013

Wafanyakazi wa Serikali Marekani warejea kazini.



Malefu ya wafanyakazi wa serikali ya Marekani waliokuwa nyumbani kwa wiki mbili wanarudi kazini baada ya bunge kuidhinisha usiku wa Jumatano mswada wa wa kugharimu shughuli za serikali na kuiruhusu serikali kulipa madeni yake.

Rais Barack Obama alitia saini mswada wa matumizi ya serikali na kuongezwa kiwango cha serikali kukopa karibu usiku wa manane Jumatano.

Wakurugenzi wa idara mbali mbali walionekana wakiwakaribisha wafanyakazi waliokuwa wanarudi kazini asubuhi alhamisi.

Ingawa serikali imeanza kazi lakini wakuu wa vyama vya wafanyakazi wa serikali wanasema wafanyakazi wengi watahitaji muda kabla ya kurudi kazini kwani taarifa imetoka usiku sana na huwenda wengi hawakuwa wanafuatilia habari.

Zaidi ya hayo wakati sehemu kubwa ya wafanyakazi wa serikali waliporudishwa nyumbani hapo Oktoba Mosi hawakuwa na ruhusa ya kufungua mitandao ya mahali wanakofanyia kazi au kupiga simu na hivyo huwenda hawana habari ya kurudi kazini.

Uamuzi wa kufunguliwa serikali ulifikiwa baada ya Baraza la Wawakilishi kuidhinisha mswada wa sheria Jumatano usiku kwa kura 285 dhidi ya 144 baada ya mswaada kuidhinishwa awali na Baraza la Seneti kwa kura 81 dhidi ya 18.

Mswada huo unatokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya rais wa Baraza la Senet Mdemokrat Harry Ried na kiongozi wa upinzani Mitch McConnell juu ya kugharimia matumizi ya serikali angalau hadi Januari 15 na kupandisha kiwango cha kukopa ili kuepuka hatari ya serikali kushindwa kulipa madeni  hadi angalau Februari 7.

Viongozi hao walikubaliana pia kuanza majadiliano juu ya bajeti ya mwaka 2013 – 2014 na namna ya kupunguza matumizi ya serikali.

Rais Obama ameshukuru vyama vyote na kusema kuwa muda umefika wa kurejesha uaminifu uliopotea kwa Wamarekani.
Chanzo: VOAswahili

No comments: