Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga
wamesema wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya watani
wao wa jadi, Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
utakaopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari
baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji, Baraza la Wazee na matawi
ya Yanga ya jiji la Dar es Salaam kilichofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya
klabu hiyo jijini jana, msemaji wa matawi hayo, Bakili Makele alisema mipango
ya 'kumuua mnyama' imeshakamilika na wameshahakikishiwa kuibuka na ushindi wa
magoli 3-0 katika mchezo huo mgumu dhidi ya vinara wa ligi.
Tumepokea taarifa kutoka kwenye
Kamati ya Utendaji, Sekretarieti na Baraza la Wazee la Yanga kwamba mipango
yote inakwenda vizuri, hakuna matatizo kwenye timu na hatuna majeruhi hata
mmoja. Tunapiga magoli matatu Jumapili," alisema Makele.
"Tunaomba nidhamu kwa wanachama
na mashabiki wa Yanga siku hiyo. Tunaomba pia refa na wasaidizi wake siku hiyo
wawe makini maana wapinzani wetu mechi zao ni za penalti. Kila mechi wachezaji
wao wanajiangusha na kupewa penalti zisizo halali," alisema zaidi Makele,
ambaye pia ni kiongozi wa Tawi la Yanga la Temeke.
Naye Katibu wa Baraza la Wazee la
Yanga, Ibrahim Akilimali aliahidi ushindi mnono siku ya Jumapili katika mchezo
huo na kubainisha kuwa viongozi, makocha na wachezaji wameshamaliza kazi na
kilichopo kwa sasa wao wanamalizia kazi ili kunogesha ushindi huo.
"Yanga tuna tamaduni zetu,
sehemu yoyote ile ina asili yake, hivyo kwa hivi sasa sisi wazee kwa pamoja
tunaahidi lazima tumchinje mnyama Jumapili. Uwezo na nia tunayo, hivyo
washabiki wa Yanga mje kwa wingi Uwanja wa Taifa kuishangilia timu yetu"
alisema Akilimali.
"Baada ya kufungwa 3-2 na Azam,
nilisema kwamba Yanga sasa inaanza ligi. Watani wetu wanaweweseka kuona 'speed'
(kasi) yetu ni ya hali ya juu, tunachoomba ni waamuzi kuchezesha soka kwa
kufuata kanuni 17 za mchezo. Yanga si timu ya kuhurumiwa na marefa, na kama
watafuata sheria 17 za soka, basi lazima tumchape mnyama.
"Watani wetu walitufunga 5-0,
sisi (Yanga) hatutawafunga magoli hayo katika mchezo mmoja bali tutajibu kwa
kushinda michezo mitano mfululizo dhidi ya Simba. Hapo tutaona nani atakayeumia
zaidi; aliyefungwa 5-0 katika mchezo mmoja au aliyepoteza michezo mitano
mfululizo," aliongeza Akilimali.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka
Kizuguto alisema jana kuwa kikosi chao kinaendelea vizuri na mazoezi kisiwani
Pemba kujiandaa kwa mchezo huo utakaochezeshwa na refa mwenye beji ya
Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) Israel Nkongo wa Dar es Salaam, ambaye
aliwahi kukunjwa na kupigwa na baadhi ya wachezaji wa Yanga katika mchezo wa
ligi hiyo waliyolala 3-1 dhidi ya Azam FC msimu wa 2011/12.
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh
aliiambia NIPASHE akiwa Pemba baada ya mazoezi ya jana kuwa wachezaji wote 29
walioidhinishwa kuitumikia Yanga msimu huu wako 'fiti' kwa ajili ya mchezo huo
utakaokuwa wa tatu (wa watani) kwa kocha Mholanzi Ernie Brandts tangu atue
Septemba mwaka jana kuchukua mikoba ya kocha Mbelgiji Tom Saintfiet
aliyetimuliwa.
Mholanzi huyo aliyetua Yanga akitokea
klabu ya 'maafande' wa APR ya Rwanda aliyoifundisha tangu 2010, aliiongoza
Yanga kuichapa Simba 2-0 katika mchezo wao wa mwisho wa kufunga msimu uliopita
wa Ligi Kuu ya Vadacom Tanzanbia Bara iliyochezwa Mei 18 kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili
jana kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zilieleza kuwa kikosi chao kitaingia Dar
es Salaam muda wowote kuanzia leo jioni kikitokea Pemba tayari kwa mchezo wa
keshokutwa.
"Timu itatua Dar es Salaam kwa
ndege muda wowote kuanzia kesho (leo) jioni na itafikia kwenye moja ya hoteli
nzuri za jiji hili kuendelea na kambi," alisema mmoja wa 'vigogo' wa Yanga
ambaye aliomba jina lake lisitiriwe.
SIMBA WAJIBU MAPIGO
Kwa upande mwingine, uongozi wa Simba umesema hautishwi na tambo za watani wao wa jadi na umejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo utakaoanza saa 10:00 alasiri.
Kwa upande mwingine, uongozi wa Simba umesema hautishwi na tambo za watani wao wa jadi na umejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo utakaoanza saa 10:00 alasiri.
Mmoja wa viongozi 'wazito' wa Simba
ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji wa klabu hiyo
iliyoanzishwa 1936, alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaishangaza Yanga
kwa kuishushia kipigo kikali Jumapili.
"Yanga wanaongea kujifurahisha.
Katika mpira huwezi kusema unaingia uwanjani ukijua unashinda 3-0. Timu yetu
imeandaliwa vizuri ili iibuke na ushindi dhidi yao," alisema kiongozi huyo
huku akiweka wazi kuwa kikosi cha Simba kimeweka kambi yake Bamba Beach.
Kigamboni jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mchezo huo.
Chanzo: Nipashe

No comments:
Post a Comment