Saturday, October 19, 2013

Saudia yakataa nafasi katika UN



Serikali ya Saudi Arabia imekataa nafasi iliyopewa na baraza la usalama la umoja wa mataifa kuwa mwanachama asiye wa kudumu, huku ikituhumu baraza hilo kwa mapendeleo.

Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo , alisema kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kufanyiwa mageuzi mwanzo.
Aliongeza kusema kwamba baraza la usalama limefeli katika majukumu yake kuhusu Syria pamoja na katika mizozo mingine kote duniani.
Awali, Saudi Arabia iliwahi kuelezea uchungu wake kuhusu jamii ya kimataifa kukosa kutatua mzozo wa Syria, ambako inaunga mkono waasi dhidi ya serikali ya Rais Bashar al Asaad.

Kwa kawaida huwa kuna ushindani mkali miongoni mwa nchi kutaka moja ya nafasi kumi zisizo za kudumu katika baraza hilo ambazo hushikiliwa na nchi tofauti kwa awamu kwa muda wa miaka miwili, katika baraza hili linalosimamia maswala ya usalama duniani.
Lakini Saudi Arabia imeamua kutumia nafasi hii kuelezea pingamizi zake kuhusu baraza hilo.

Hii ni mara ya pili kwa Saudi Arabia kuelezea hisia zake kuhusu swala kama hili.
Mapema mwezi huu, waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, aligoma kutoa hotuba yake katika baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuelezea ,malalamiko yake kama hayo tu.
Bila shaka hatua ya Saudia imewashangaza wengi lakini ikiwa itaishinikiza kufanya mageuzi, haijulikani kama yatafanyika mara moja.

Hatua hii imekuja saa chache baada ya Saudia kuteuliwa kwa mara ya kwanza kuchukua nafasi hiyo katika baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Chanzo: BBCswahili

No comments: