Dar es Salaam.Vyama vya Upinzani
vimesema visipopata mwafaka wa mazungumzo baina yao na Rais Jakaya Kikwete juu ya Muswada wa
Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ya Katiba, vitarudi kwa wananchi kuwaleza hatua
ya kuchukua.
Kauli hiyo inatokana na hotuba ya
mwisho wa mwezi iliyotolewa na Kikwete, alipoviomba vyama hivyo kusitisha
dhamira ya kuandamana Oktoba 10 mwaka huu kudai usawa katika mchakato wa
katiba. Kikwete aliviomba vyama hivyo kukaa nao meza moja kwa lengo la kufanya
mazungumzo ya kina ili kuondoa tofauti zilizopo.
Hatua hiyo ilifikiwa na Wabunge wa
Upinzania baada ya kususia Mkutano wa Bunge uliomalizika mwezi uliopita mjini Dodoma, uliokuwa
ukipitisha muswada huo kwa kile walichokilalamikia wananchi kutowashirikisha
ipasavyo.
Wakizungumza jana katika Mkutano wa
Mashauriano juu ya mchakato wa Katiba ulioandaliwa na Jukwaa la Katiba Nchini,
viongozi wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, APPT-Maendeleo, National League of
Democracy (NLD) na UPDP walisema, wanakwenda kumsikiliza Kikwete na wasipofikia
mwafaka watajua nini cha kufanya.
Mkurugenzi wa Habari na Unezi wa
Chadema, John Mnyika alisema endapo mwafaka hautafikiwa watarejea kwa wananchi
kuwaeleza kipi kitafuata.
Mnyika alisema Rais Kikwete anafahamu
kila kitu kinachopigiwa kelele na wapinzania na asasi za kiraia, hivyo
wanaamini watafikia mwafaka katika mazungumzo hayo.
“Tunakwenda kumsikiliza, lakini kama hatutafikia mwafaka tutarudi kwa wananchi na
kuwaeleza hatua ya kufuata kuidai katiba yenye tija kwa wananchi,” alisema
Mnyika, Mbunge wa Ubungo.
Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter
Mziray alisema: “Kinachotakiwa ni mchakato kuanza upya na wananchi waelimishwe.
Tukiendelea hivi, maana yake tunaandaa katiba mbovu na isiyo na tija kwa
taifa,” alisema Mziray.
Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi
alisema serikali ikubali kwamba imepoteza fedha hivyo mchakato hauna haja ya
kuendelea.
Makaidi alisema katiba haitungwi
bungeni, ila nje ya Bunge hivyo mchakato kupitia bungeni na wabunge kutoweka
mbele masilahi ya taifa ni kuhatarisha mustakabali wa amani.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment