Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku
Na Exuper Kachenje, Mwananchi
Dar es Salaam/Mikoani. Kamishna wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku amesema ipo haja kwa tume iwezeshwe
kushiriki mchakato wa Katiba katika hatua zote zilizosalia, badala ya kubaki
nje ya Bunge la Katiba kama washauri baada ya
kukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba kwa Rais.
Butiku alisema licha ya umuhimu huo,
tume haiwezi kulazimisha kushiriki kwake katika hatua za utunzi wa katiba
zilizobaki na kwamba suala hilo linabaki
mikononi mwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwapo litaifanyia
marekebisho sheria husika.
Butiku ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Taasisi ya Mwalimu Nyerere alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na
gazeti hili, kuhusu mchakato wa uandikwaji wa Katiba Mpya, ambao umezua
mivutano ya kimasilahi miongoni mwa makundi ya kisiasa.
Moja ya vipengele vya Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa na Bunge
Septemba, mwaka huu, kinaeleza kuwa baada ya kukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba
kwa Rais, wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba hawatahusika tena na mchakato
huo, badala yake watabaki kuwa washauri tu.
“Sisi (Tume) tunafanya kazi kwa
mujibu wa sheria, sheria kwanza ilisema tutafanya kazi mpaka mwisho, sheria ya
sasa inasema tutaishia nje ya Bunge kama
washauri. Sasa hayo ni mambo ya Bunge, lenyewe liamue wanayoyaamua,
wakituhitaji kwenda (bungeni) kwa ushauri tutakwenda. Nadhani itakuwa vizuri
hivyo, maana kazi hiyo siyo ya mmoja na inahitaji umakini mkubwa,” alisema
Butiku na kusisitiza:
“Kama Bunge litaona inafaa hivyo,
ndiyo kazi yetu hatuna kipingamizi, tutakwenda.”
Alitoa kauli hiyo baada ya kuhojiwa
kuhusu kuwapo taarifa zilizodai kwamba wajumbe wote wa tume wamepanga kujiuzulu
iwapo sheria iliyopitishwa na Bunge haitarekebishwa, ili kuwapa nafasi ya
kisheria ya kufanyia kazi Rasimu ya Pili ya Katiba hatika hatua zote badala ya
kubaki kuwa washauri.
“Na labda niseme tu kwamba tishio la
wajumbe wa tume kutaka kujiuzulu halipo, tishio hilo halipo,” alisisitiza Butiku ambaye
aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Aliongeza kuwa kilichoikasirisha tume
ni mwelekeo wa makundi mbalimbali hasa ya kisiasa kuingilia mchakato wa Katiba,
hali iliyoifanya tume kuamini kuwa vyama vilikuwa vimeanza kuvuruga mchakato
huo.
Hata hivyo, alisema hivi sasa
inaonekana kama kila mmoja amerejea kuheshimu
sheria na kila mmoja anatimiza wajibu wake.
Mvutano wa kisiasa
Akizungumzia mvutano ulioibuka kati
ya vyama vya upinzani na Serikali kuhusu baadhi ya marekebisho yaliyofanywa
kwenye sheria, Butiku alisema: “Mimi sitaki kusema kama
huo ni mvutano, hiyo ni tofauti ya mawazo. Tusishangae, hamuwezi kufanya jambo
kubwa namna hii la kujenga misingi ya taifa letu, kutazama Katiba yetu iweje,
mwendesheje nchi yenu bila kutofautiana kimawazo.”
Aliongeza kuwa angeshangaa na
kusikitika kama zisingekuwapo tofauti za
mawazo kwa kuwa ndiyo afya ya mjadala wa Katiba Mpya, na kwamba ndiyo maana
Rais Jakaya Kikwete ameamua kukutana na viongozi wa vyama vya upinzani
vinavyolalamika.
“Hiyo ndiyo afya ya mchakato, tofauti
isionekane kama jambo la uhasama, nchi
nyingine huwa na matendo mabaya zaidi, wanaweza kugombana hata kupigana, sisi
hatujafanya hivyo, sisi tunajenga hoja. Kwa hiyo, hizo tofauti ni nzuri,”
alisema Butiku.
Alisema hatua ya Rais Kikwete kuamua
kukutana na viongozi wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF kuzungumzia
mustakabali wa mambo yanayolalamikiwa na upinzani inafaa kupongezwa.
“Ni jambo zuri, ni vizuri tumpongeze
Rais, anapenda mjadala kufikia mwafaka. Hii siyo kazi ya kikundi ni kazi ya
Watanzania wote…; Siyo jambo ya mtu mmoja, ni jambo la mwafaka. Mwafaka
unatokana na mazungumzo na Rais anakaribisha mazungumzo,” alisema Butiku lakini
akatahadharisha:
“Ni vizuri wanaokwenda kuzungumza
naye wazungumze vizuri, wajiandae vizuri kumsaidia Rais...Wazungumze na Rais
wetu kwa hoja, wamsaidie na yeye awasaidie, wote tusaidiane.”
Kasoro kwenye muswada
Baadhi ya wanasheria wasomi
wamesisitiza kuwa malalamiko ya wapinzani yana mashiko kwani ni dhahiri kwamba
muswada uliopitishwa na Bunge ulikuwa na kasoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la
Utafiti wa Mambo ya Uchumi na Umaskini (Repoa), Profesa Samwel Wangwe alirejea
hoja ya kutoshirikishwa kwa wadau wa Zanzibar na kusema: “Katiba siyo mali ya
chama cha siasa, Katiba ni mali ya Watanzania, hivyo ni lazima washirikishwe.”
Alisema kabla ya kuanza kutumia
sheria ya mabadiliko ya Katiba, lazima upatikane mwafaka wa kitaifa na
kusisitiza: “Katiba siyo mapambano na haitakiwi katika uandikwaji wake upande
mmoja ujione uko sahihi kuliko mwingine. Tujenge mwafaka wa pamoja.”
Naye wakili maarufu nchini, Peter
Kibatara alisema ili azma ya kuandika Katiba Mpya isiyokuwa na malalamiko
itimie ni lazima viongozi wawe na utashi, maono, kuacha ubinafsi, kuweka
masilahi ya wananchi mbele na kutafuta mwafaka wa pamoja.
“Wanasiasa wanatakiwa kuvua kofia zao
za kisiasa na kuzingatia hayo niliyoyataja. Wakifuata hayo mchakato utakwenda
vizuri na hakutakuwa na malalamiko,” alisema Kibatara.
Kwa upande wa mwanasheria wa Kampuni
ya Uwakili ya Rwelu ya jijini Mwanza, Alfred Sotoka alisema Rais ameona kuwa
wapinzani wana hoja za msingi na kukubali kwake kukaa nao meza moja ni jambo la
busara.
“Hii siyo mara ya kwanza kwa Rais
kukaa nao meza moja, hii ni mara ya pili toka mchato huu kuanza na tukumbuke
kuwa mazungumzo ya awali yalileta mafanikio na kupatikana makundi ya kijamii
ambapo walipata nafasi na kuunda Mabaraza ya Katiba na kupata fursa ya kutoa
maoni yao,”
alisema Sotoka.
Baadhi ya wasomi wanasema kuwa hatua
ya Rais Kikwete kuamua kukutana na wapinzani inathibitisha kwamba Muswada wa
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba , utarejeshwa bungeni
kwa ajili ya marekebisho, hata kabla ya kuanza kutumika.
Wakili Charles Semgalawe pia wa Dar es Salaam alisema
alichofanya Rais Kikwete ni kukwepa kuvunja bunge na Serikali yake, hatua
ambayo angelazimika kuichukua endapo asingesaini muswada huo.
Hata hivyo hadi sasa hakuna taarifa
zozote kuhusu kusainiwa au kutosainiwa kwa muswada huo.
“Muswada wa sheria yoyote ukipitishwa
na Bunge endapo Rais atakataa kuutia saini, maana yake lazima aivunje Serikali
yake na uchaguzi uitishwe upya kwa hiyo alichofanya ni ujanja tu,” alisema
Semgalawe na kuongeza:
“Ameamua kuwarudishia wabunge kile
walichopitisha ili warekebishe, ukijaribu kuangalia ni sawa na amewarudishia
matapishi yao
wayale tena.”
Hata hivyo, alisema kuwa, hatua hiyo
ya Rais Kikwete ni nzuri kwani angeweza kuamua kung’ang’ania kile
walichopitisha wabunge wa chama chake hata kama
hakina manufaa kwa taifa.
Vyama vya upinzani vilikuwa vimepanga
kufanya maandamano Alhamisi wiki hii kushinikiza Rais kutosaini muswada huo,
lakini vikaamua kuyasitisha baada ya Rais Kikwete kuwaalika kwenye meza ya
mazungumzo.
Mbali na hoja ya ukomo wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, mambo mengine yanayolalamikiwa katika sheria
iliyopitishwa ni nguvu ya Rais katika kuteua wabunge wa nyongeza 166 wa Bunge
Maalumu la Katiba, idadi ya kura zinazohitajika kupitisha uamuzi katika Bunge hilo na suala kwamba Zanzibar
haikushirikishwa.
Taarifa za nyongeza na Fidelis Butahe
na Freddy Azzah (Dar) na Sheilla Sezzy (Mwanza)
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment