Addis Ababa. Muungano wa Afrika (AU) umeitaka
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kusitisha kesi dhidi ya wakuu wa nchi
walioko madarakani kwa sasa hadi watakapomaliza vipindi vya uongozi wao.
Viongozi walioko madarakani kwa sasa
ambao wanakabiliwa na kesi kwenye mahakama hiyo ni Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na makamu
wake, William Ruto wanaotuhumiwa kwa makosa ya uchochezi, mauaji na uhalifu
dhidi ya ubinadamu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Mwingine ni Rais wa Sudan, Omar al-Bashir ambaye mahakama hiyo
imetoa hati ya kukamatwa kwake akihusishwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa
kuamrisha mauaji ya watu kwenye eneo la Darfur
nchini kwake.
Msimamo huo umefikiwa baada ya kikao
cha wakuu wa nchi mjini Addis Ababa jana, kilichozima shinikizo la kutaka nchi
wanachama wa umoja huo zilizo wanachama wa mkataba wa Roma ulioianzisha
mahakama ya ICC mwaka 2002 zijitoe.
Msimamo huo uliosababisha kuitishwa
kwa kikao maalumu cha dharura cha AU ilichofanyika juzi na jana ulipingwa
vikali na viongozi mbalimbali duniani, akiwemo Jaji Mtanzania aliyeapishwa wiki
hii kuwa Jaji wa ICC, Jaji Stephen Bwana ambaye alisema ICC ni wembe kwa
viongozi wanaojifanya miungu watu.
“Afrika ina viongozi wengi wazuri,
lakini pia tusifiche ukweli kwamba tunao viongozi wa ovyo, ambao wanadhani ni
(semi gods) nusu miungu. Wangependa kila kitu kiwe chao tu. Sasa tukisema
kwamba nchi zote za Afrika zijiondoe ICC, tunataka kusema kwamba hatufanyi
makosa.”
Jaji Bwana ambaye aliapishwa rasmi
wiki hii kuwa Jaji wa ICC nchini Cambodia aliongeza kwamba, viongozi
hao ‘miungu watu’ wamezifanya taasisi za utoaji haki kwenye nchi zao kuwa
dhaifu na kwamba kwa hali hiyo hawawezi kushtakiwa katika mahakama za nchi zao
kwa makosa wanayoyafanya.
Viongozi wengine maarufu duniani
waliopinga hatua hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (AU) Kofi
Annan ambaye alisema Afrika itaingia kwenye ‘dimbwi la aibu’ na Askofu Desmond
Tutu wa Afrika Kusini ambaye alisema viongozi wanaotaka nchi zao zijitoe
wanataka kujihalalishia “uuaji uliotukuka”.
Akizungumzia uamuzi wa mkutano huo wa
wakuu wan chi jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom
Ghebreyesus alisema uamuzi uliofikiwa ni wa kuitaka mahakama hiyo kutowakamata
na kuwashtaki viongozi walipo madarakani.
Alisema wakuu wa AU wamekubaliana
kuiandikia ICC na kuitaka kusitisha kesi dhidi ya Rais Kenyatta, makamu wake
William Ruto na hati ya kukamatwa kwa Rais Bashir kwa sasa.
Tedros ambaye ndiye mwenyekiti wa
Baraza Kuu la AU kwa sasa, alisema ICC imeonesha wazi kwamba imejigeuza kuwa
chombo cha kisiasa kinacholenga kuiyumbisha Afrika na Waafrika, suala ambalo
haliwezi kukubalika. Alisema kutokana na hali hiyo, ICC imeshindwa kutilia
maanani maombi ya awali ya AU, hivyo suala hilo kwa sasa litapelekwa kwenye hatua
nyingine.
No comments:
Post a Comment