Wilfred Kidau (nyuma ) na Shaffih
Dauda
Kamati ya Rufani ya Maadili ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewaadhibu walalamikiwa watano
kati ya saba baada ya kufanya mapitio (revision) kwa uamuzi wa Kamati ya
Maadili kutokana na maombi ya Sekretarieti, huku Richard Julius Rukambura
akifungiwa miaka 20 kujihusisha na mpira wa miguu.
Sekretarieti ya TFF iliwasilisha
maombi ya mapitio kwa Kamati ya Rufani ya Maadili ili kupata mwongozo kwa vile
kulikuwapo mkanganyiko kwenye uamuzi wa Kamati ya Maadili, hivyo kuiwia vigumu
kwake kuutekeleza.
Uamuzi huo wa mapitio umesomwa leo
jioni (Oktoba 15 mwaka huu) mbele ya waandishi wa habari na wajumbe wa Kamati
hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Victoria Makani.
Rukambura amefungiwa miaka 20 baada
ya kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika mahakama za kawaida kinyume na
Ibara ya 75 ya Katiba ya TFF na kifungu cha 73(3)(b) cha Kanuni za Maadili za
TFF toleo la 2013. Adhabu yake itamalizika Oktoba 15, 2033.
Kabla ya kutoa adhabu hiyo, Kamati
imejiridhisha kuwa Rukambura ni mwanafamilia wa TFF kwa vile aliwahi kuwa
Mwenyekiti wa klabu ya Pamba ya Mwanza, na fomu zake za kuomba uongozi TFF
ziliidhinishwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga. Vilevile ni
'Leadership Aspirant' kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii za TFF
toleo la 2013.
Pia imesema kwa Msajili wa Klabu na
Vyama vya Michezo kusajili Katiba ya TFF inayokataza masuala ya mpira wa miguu
kwenda katika mahakama za kawaida, na kutaja vyombo vya haki
vitakavyoshughulikia masuala hayo (judicial organs), Kamati ya Maadili ilikosea
kutomtia hatiani mlalamikiwa kwa kuegemea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Naye Shaffih Dauda, Kamati imebaini
kuwa mwanafamilia wa TFF kwani ni Mwenyekiti wa Bombom FC, fomu yake ya kuomba
uongozi ilipitishwa na klabu ya Simba na pia ameshakuwa kiongozi katika ngazi
mbalimbali ndani ya Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA), hivyo
yeye ni 'Leadership Aspirant' kwa mujibu wa kifungu cha 2(v) cha Kanuni za Utii
za TFF toleo la 2013.
Hivyo Dauda amepatikana na kosa la
kimaadili kwa kutotekeleza maagizo rasmi ya TFF ya kutosambaza barua iliyotoka
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwenda kwa Rais wa TFF,
Leodegar Tenga.
Kamati ya Rufani ya Maadili imempa
onyo kali na faini ya sh. milioni moja anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu
ambapo akishindwa kufanya hivyo atafungiwa mwaka mmoja. Adhabu hiyo imetolewa
kwa mujibu wa kifungu cha 6(1)(a),(c) na (h) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo
la 2013.
Akilipa faini ataweza kuendelea na
mchakato wa kugombea nafasi ya uongozi aliyoomba.
Nazarius Kilungeja amepatikana na
kosa la kimaadili kwa mujibu wa kifungu cha 73(8)(a) cha Kanuni za Maadili za
TFF toleo la 2013, kwani akijua kuwa ana adhabu ya kinidhamu ya kufungia miaka
mitano na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) iliyoanza 2009
alichukua fomu kuomba uongozi TFF.
Hivyo, amefungiwa miaka mitatu,
adhabu ambayo itakwenda sambamba na ile ya RUREFA ambapo kifungo chake sasa
kitamalizika Oktoba 15, 2016.
Sekretarieti ya TFF imepewa onyo kali
kwa kupokea fomu yake ya kugombea na malipo wakati akiwa amefungiwa. Onyo hilo
pia limetolewa kwa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) Mkoa wa
Rukwa kwa kuidhinisha fomu yake ya kugombea.
Naye Wilfred Kidao Mzigama ambaye ni
mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF amepatikana na kosa la kimaadili kwa kuwa na
nyaraka la Kamati ya Utendaji bila kibali na kukiuka taratibu za kuwasilisha
malalamiko kwa mujibu wa Ibara ya 12(2) na Ibara ya 50(1) na (5) ya Katiba ya
TFF.
Amepigwa faini ya sh. milioni moja
anayotakiwa kuilipa ndani ya siku tatu ambapo akishindwa atafungiwa mwaka
mmoja. Akitekeleza adhabu hiyo ataweza kuendelea na mchakato wa kugombea
uongozi kwa nafasi aliyoomba.
Vilevile Kamati hiyo imetoa onyo kali
kwa Sekretarieti ya TFF na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kwa kushindwa
kudhibiti nyaraka muhimu za vyombo vyao.
Pia Kamati ya Rufani ya Maadili
imempata na kosa la kimaadili Kamwanga Tambwe kwa mujibu wa kifungu cha 73(8)
cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013, kwa kuingia kwenye mchakato wa
uchaguzi wakati ana adhabu ya kinidhamu inayomalizika 2014.
Hivyo, amepewa adhabu ya kufungiwa
miaka mitatu ambayo itakwenda sambamba na ile ya kinidhamu na kumalizika Oktoba
15, 2016. Pia Sekretarieti ya TFF, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma
(FARU) na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) Mkoa wa Ruvuma
wamepewa onyo kali kwa kupokea na kuidhinisha fomu zake za kugombea uongozi
wakati akitumikia adhabu ya kufungiwa.
Kamati ya Rufani ya Maadili imewakuta
kutokuwa na hatia ya makosa ya maadili kama ilivyobaini Kamati ya Maadili
walalamikiwa Riziki Juma Majala na Omar Isack Abdulkadir, hivyo wana haki ya
kugombea uongozi kwa kufuata Katiba na Kanuni za TFF.
Kwa mujibu wa kifungu cha 74(4) cha Kanuni
za Maadili za TFF toleo la 2013, uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Maadili hauna
fursa ya rufani wala marekebisho kutoka chombo kingine chochote isipokuwa FIFA
na Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
chanzo: shafiidauda.com
No comments:
Post a Comment