Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete na
viongozi wa vyama vya siasa vya CCM, Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi, TLP na UDP
wamekubaliana mambo mawili makubwa baada ya kuweka pembeni tofauti za kiitikadi
na kutanguliza masilahi ya taifa walipokutana jana Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliitishwa na Rais
Kikwete ili kuondoa sintofahamu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba uliopitishwa Septemba na Bunge lilipokutana mjini
Dodoma.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya
Mawasiliano Ikulu jana jioni ilisema katika mkutano huo ilikubaliwa kwamba
vyama vyote vya siasa nchini vyenye mawazo, maoni na mapendekezo ya kuboresha
Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba viwasilishe mapendekezo
yao haraka serikalini ili ifatutwe namna ya kuyashirikisha mapendekezo hayo
katika marekebisho ya sheria hiyo.
Pia Rais na vyama hivyo walikubaliana
kwamba vyama vya siasa nchini, kama wadau muhimu katika mchakato wa Katiba
Mpya, viangalie namna ya kukutana na kujenga mfumo wa mawasiliano na maridhiano
kwa lengo la kusukuma mbele mchakato huo kwa masilahi mapana ya nchi yao na
mustakabali wa taifa.
“Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)
kimepewa jukumu la kuratibu jambo hilo ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano wa
vyama hivyo na wadau wengine nchini,” iliongeza taarifa hiyo.
Viongozi wa vyama vyama vya siasa
waliohudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM,
Philip Mangula, Isaack Cheyo ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo
na Nancy Mrikaria ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema.
Cheyo na Mrema wako nje ya nchi.
Wengine ambao waliambatana na
wenyeviti wao ni Mohamed Mnyaa na Julius Mtatiro wa CUF, Tundu Lissu na John
Mnyika wa Chadema na Martin Mng’ongo wa NCCR-Mageuzi.
Vicheko Ikulu
Vicheko na bashasha vyatawala Ikulu
Ilikuwa fursa kwa Rais Kikwete
kukutana na viongozi hao baada ya kipindi cha miezi miwili cha kurushiana
maneno baina ya viongozi wa Bunge, Serikali, CCM waliokuwa wakivutana na
viongozi wa vyama vitatu vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi.
Kama mtu yeyote angeulizwa kutabiri
katika tukio lililotokea jana lingetokea basi angekuwa na wakati mgumu kutokana
na ukali wa maneno na malumbano katika kipindi chote baada ya kumalizika kwa
mkutano wa Bunge wa Septemba.
Rais Kikwete alionekana mwenye furaha tele wakati
alipokutana na viongozi wa vyama hivyo na kivutio zaidi ilikuwa pale
alipokutana na Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani, Tundu Lissu.
Viongozi hao walisalimiana huku wote wakitabasamu na
kuashiria kuwa waliamua kuweka tofauti zao pembeni na kuangalia masilahi ya
nchi.
Kumbuka katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Septemba, Rais
Kikwete alimshutumu Lissu kwa kusema kwamba katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kuwa yeye hakuheshimu mawazo ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT).
Rais Kikwete alikaririwa akisema kauli hiyo ya Lissu ni
uzushi, uongo na uzandiki wa hali ya juu, huku akisisitiza kuwa mbunge huyo
alitoa kauli hiyo ili kupotosha ukweli na pengine isaidie kujenga hoja yake ya
kutaka Rais asiteue wajumbe 166 wa Bunge Maalum la Katiba.
Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alipinga
tuhuma hizo na kusisitiza Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT)
bila ya ridhaa yao.
Chikawe, Wassira na Lukuvi ndani
Mawaziri watatu, ambao walitetea kwa nguvu kupitishwa kwa
muswada ule ndani na nje ya Bunge walihudhuria mazungumzo hayo.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias
Chikawe na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mahusiano na
Uratibu, Stephen Wassira walikuwemo kwenye mazungumzo ya jana.
Mawaziri hawa kwa nyakati tofauti walitetea kuwa mchakato wa
muswada ule haukuwa na matatizo yeyote na kushikilia kuwa lazima Rais lazima
asaini muswada kwani ulikuwa umepitishwa kihalali na Bunge.
Pia walikuwa wameshikilia kuwa safari hii kulikuwa hakuna
mambo ya mazungumzo kati ya Rais na upinzani.
Chanzo cha sintofahamu
Wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi walisusia mjadala wa muswada huo wakipinga matayarisho yake
kutoshirikisha upande wa Zanzibar na pia walikuwa hawakubaliani na baadhi ya
vipengele vya muswada huo.
Katika hatua nyingine, taarifa kutoka
Ikulu zilisema kwamba Rais Kikwete alisaini muswada huo tangu Oktoba 10 mwaka
huu siku ambayo wapinzani walipanga kufanya maandamano nchi nzima.
Katika mahojiano na Mwananchi jana
jioni, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema muswada huo
tayari ulikwishasainiwa na Rais na kama kuna marekebisho yatafanywa.
Mwananchi ilimtafuta Rweyemamu baada
ya kusikia akithibitisha kusainiwa kwa muswada huo katika mahojiano na BBC
Idhaa ya Kiswahili jana.
Akizungumza na Mwananchi Rweyemamu
alisema, “Rais ameshasaini tangu Oktoba 10, unajua kulikuwa hakuna tatizo lolote
kuhusu muswada huu kwa sababu ulifuata taratibu zote bungeni.”
Rweyemamu alisema kuwa awali Ikulu
ilitoa taarifa kuwa Rais atakutana na wapinzani, pia atausaini muswada huo.
“Muswada umepitishwa bungeni na yeye
amekamilisha kazi kwa kuusaini ili kuwa sheria. Alipokutana na wapinzani leo
(jana) amewaeleza hilo na wameridhika” alisema Rweyemamu.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment