Wajukuu wa Mwalimu Nyerere wakiwa na baba yao mdogo, John Nyerere
(katikati). Kulia ni Moringe Magige na kushoto ni Julius Makongoro. Picha na
Julieth Kulangwa NyereNyerere(katikati) , Picha na Julieth Kulangwa.
Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Si urithi wa mali, isipokuwa ni
mapenzi kwa binadamu wenzake na hekima ambavyo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere ameviacha katika vitabu, maandiko mbalimbali na kwa
familia yake, tangu afariki dunia miaka 14 iliyopita.
Unapofika katika nyumba yake iliyopo
jijini Dar es Salaam maeneo ya Msasani maarufu kwa Mwalimu Nyerere,
kinachoyatofautisha maisha ndani ya nyumba hiyo na zile za Magomeni na Ilala ni
mazingira nadhifu.
Wenyeji ndani ya nyumba hii kwa
mwonekano na mazungumzo hawana tofauti na Watanzania wa kawaida, hawana
majivuno na wanamkaribisha mgeni kama ndugu au
jamaa waliyemfahamu miaka mingi.
Pamoja na kuwa nyumba ni kubwa na
wenyeji ni wengi, lakini kwenye maegesho ya magari lipo gari moja tu. Mwonekano
wa nje wa nyumba hii unaweza kukufanya ufikiri ndani kuna magari zaidi ya
matatu tena ya kifahari.
Wanafamilia ni wakarimu sana, kwa
kawaida ungetarajia kusikia wenyeji wakitumia maneno kama “Yes, No” na maneno
mengine ya Kiingereza kwa kuwa hiki ni kitambulisho cha vijana waliopata elimu
angalau ya sekondari, lakini hapa ni tofauti, wote wanazungumza Kiswahili na
bahati mbaya wakichanganya huwa ni lugha ya Kizanaki.
Wajukuu wa Baba wa Taifa, Moringe
Magige na Julius Makongoro wanasema huu ndiyo urithi ambao Baba wa Taifa
aliwaachia ndugu zake wakisema kuwa walilelewa kuamini kuwa mali siyo kitu
kuliko utu na ndivyo walivyo.
Maisha ya Mwalimu Nyerere kama babu
Wengi tunafahamu historia ya Baba wa
Taifa hasa katika majukumu yake ya uongozi wa Tanzania
na ukombozi wa bara la Afrika, lakini Moringe na Julius wanaturudisha nyumbani
wakisimulia walivyomfahamu babu yao.
Moringe anasimulia akisema; “Kwanza mimi sikufahamu kwa jinsi gani babu alikuwa mtu
muhimu katika nchi hii na bara la Afrika kwa ujumla, nilijua baada ya kufariki
dunia na kuanza kusoma historia yake na kugundua vitu vingi alivyofanya,”
“Sikuiona tofauti yake na mababu
wengine kwani shuleni nilisikia watu wakisimulia jinsi walivyoishi na babu zao
na sikuona tofauti na babu yangu,” anasema Moringe.
Anasema Mwalimu Nyerere aliwapenda
wajukuu zake, alipenda kufanya shughuli za shamba akiwa na wajukuu zake,
hakutaka hata mmoja azembee kwenda shambani.
“Babu aliipenda familia yake,
tumeishi na ndugu wengi kwa sababu hakutaka kukaa mbali na ndugu zake na kila
mmoja alihakikisha anapata wasaa wa kukaa naye na kuzungumza naye, mfano
alikuwa na utaratibu wa kula chakula cha jioni na sisi wajukuu zake,” anasema
Moringe.
Aidha anasema kwamba Mwalimu Nyerere
alikuwa akiwahimiza kuongeza juhudi shuleni hasa katika masomo ya Kiingereza na
Hisabati.
“Babu alikuwa akifuatilia maendeleo
yetu shuleni, kila mwisho wa muhula alikagua matokeo ya kila mmoja wetu na
alikuwa akisisitiza zaidi masomo ya Kiingereza na Hesabu akisema hayo ndiyo ya
msingi,” anasema Moringe.
Alikuwa anapenda kupiga makonzi
Kila mtu anakumbuka adhabu gani
alikuwa anapewa na bibi au babu yake pale anapokosea, lakini Julius anatuambia
kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa akiwapiga makonzi wajukuu zake pale wanapokosea.
Julius anasema adhabu kubwa
waliyokuwa wakipewa na babu yao
ni kupigwa makonzi hata hivyo utaokoka tu kwa juhudi zako za kutoka mbio kwani
ukisimama anaendelea kukupiga. “Babu alikuwa na tabia ya kutupiga makonzi hasa
ukiwa mtundu au ukimpitia karibu wakati anacheza bao lazima atakupiga japo
konzi moja,” anasema.
Pia anasema kamwe hatasahau siku moja
alipomuomba babu yake akaangalie mkanda wa video mchana;” Nilimwambia babu
tunaomba kuangalia mkanda kwa sababu Tv ilikuwa inakaa Maktaba, alinikubalia na
kuniambia nenda ukawaite na wenzako unaotaka kuangalia nao. Basi nikaenda
kuwaita tulivyofika alitufungia na kuanza kutupiga makonzi ,” anasema Julius.
Aidha anasema babu yao aliwapangia muda maalumu wa kuangalia
televisheni pia aliwachagulia mikanda ya kutazama kwa kuwa alipenda wawe na
maadili mema.
Vituko,utani wa babu na wajukuu zake
Pamoja na kuwapiga makonzi wajukuu
zake lakini kuna wakati alikuwa akiketi chini na kufanya utani na kushuhudia
vituko vya wajukuu zake.
Moringe anasema moja kati ya maswali
ya utani waliokuwa wakimuuliza babu yao
ni iwapo enzi za ujana wake alikuwa akifanya starehe za aina mbalimbali.
“Tulikuwa tunamuuliza babu hivi
unajua kuogelea au kucheza muziki kwa sababu hatujawahi kukuona hata siku moja
ukicheza, alijibu ‘siwezi’, tukawa tunamuuliza sasa wewe ujana wako ulikuwa
unafanya nini, alisema ‘kusoma tu’, anasema Moringe.
Aidha wanasema utani mwingine kwa
babu yao
ilikuwa ni kuwa hajui kuendesha gari. Julius anasema “Tangu nimepata akili
sijawahi kumuona akiendesha gari, nina wasiwasi alikuwa hajui kuendesha”.
Julius pia anasema hajawahi kumuona
babu yake akiwa amevaa suti au kuchomekea huku akisema inawezekana zamani
alikuwa analazimishwa kuvaa hivyo. “Sijawahi kumuona babu amevaa suti au
amechomekea shati, hata hakupenda ndugu wavae suti hasa tukiwa Butiama,
alipenda kuvaa ‘simple’.
Alisisitiza maadili
Moringe na Julius wanasema wanaamini
babu yao
alikuwa akilinda maadili kwa kutowaachia watazame televisheni ovyo na
kuwahimiza kushiriki kanisani.
“Babu hakuwa na mchezo linapokuja
suala la kanisani, yaani usipoenda kanisani ni ugomvi mkubwa anaweza hata
kukufukuza usile naye chakula cha jioni,” anasema Moringe.
Wakizungumzia iwapo Baba wa Taifa
angekuwa hai leo angebariki matumizi ya mitandao ya kijamii kama
‘facebook’ na ‘twitter’ kwa pamoja walisema asingepinga kwani alikuwa mpenda
maendeleo.
“Watu wengi huwa wanazungumza
wakisema kuwa babu alikuwa hataki watu waendelee kwa kutumia teknolojia, sio
kweli, babu alikuwa anapenda maendeleo lakini aliheshimu utamaduni,” anasema
Julius.
Akitolea mfano wa dada yao mmoja aliyekuwa akiishi Ulaya walisema, babu yao hakuwa na tatizo na
mavazi yake lakini alimwonya kuwa ni lazima aangalie anavaa wapi.
“Mfano tukiwa hapa Msasani babu
hakumkataza kuvaa nguo zake anazopenda, lakini tulipoenda Butiama alikuwa
akimrudisha pale anapovaa nguo anazoona haziendani na utamaduni wa watu wa
kule,” anasema Julius.
Anaongeza kuwa Mwalimu asingekuwa na
tabu na mitandao hiyo au teknolojia yoyote isipokuwa pale itakapotumikwa
visivyo kama wafanyavyo wengi.
“Ukiukwaji wa maadili unaotokana na
teknolojia unawakwaza watu wengi, watu wanatumia ndivyo sivyo na hiki pengine
kingemkera babu,” anasema Julius.
Siri ya kifimbo cha babu yao
Moringe na Julius wanasema wamesikia
hadithi nyingi kuhusu kifimbo cha Mwalimu Nyerere alichokuwa akipenda kukibeba,
wengine wamediriki kusema alizikwa nacho.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment