Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani
John Kerry anatetea shambulizi lililofanywa na kikosi maalumu cha Marekani
kumkamata kiongozi mwandamizi wa al-Qaida nchini Libya akisema operesheni hiyo
ilikuwa "halali na muafaka".
Serikali ya Libya inaitaka Marekani kuelezea kuhusu kile
inachokiita "utekaji nyara" wa Abu Anas al-Libi ndani ya ardhi ya Libya tukio lililofanyika
siku ya Jumamosi.
Kerry alisema Jumatatu pembeni ya
mkutano wa kieneo huko Indonesia
kwamba madai ya Libya
hayana msingi na kwamba Libi atafikishwa kwenye mahakama ya sheria.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani inasema
Libi amehamishwa kwenda "eneo salama" nje ya Libya.
Mahakama moja ya Marekani
inamfungulia mashtaka Libi kwa kuhusika kwake katika ulipuaji mabomu
uliofanyika mwaka 1998 katika balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania. Mashambulizi hayo yaliuwa
zaidi ya watu 200 na kuwajeruhi 5,000 wengine.
Saa kadhaa kabla ya kukamatwa Libi
siku ya Jumamosi majeshi maalumu ya Marekani pia yalishambulia kituo cha majini
cha al-Shabab chenye uhusiano na al-Qaida nchini Somalia.
Maafisa wa Marekani walisema kikosi
maalumu cha jeshi la Marekani, Navy SEAL, kiliuwa wanamgambo kadhaa wa
al-Shabab katika mapigano ya risasi baada ya kuja kwenye mwambao katika mji wa
Barawe.
Chanzo: voaswahili
No comments:
Post a Comment