Nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Magomeni ambayo kwa sasa ni makumbusho ya Taifa
Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakati Taifa linaadhimisha miaka 13
ya kifo cha Mwalimu Nyerere, pia anakumbukwa kwa namna alivyoona umuhimu wa
kununua kiwanja na kujenga nyumba yake mwenyewe, eneo la Magomeni mkoani Dar es Salaam.
Enzi hizo Magomeni ndiyo ilikuwa kama Masaki. Mwalimu Nyerere alimwomba rafiki yake
Mustafa Songambele amtafutie kiwanja katika maeneo hayo, naye akampatia hicho
ambacho sasa ipo nyumba ambayo imegeuzwa Makumbusho ya Taifa.
Mhifadhi Malikale anayesimamia nyumba
hiyo, Emmanuel Katoroki anasema si serikali iliyoamua kuifanya nyumba hii kuwa
makumbusho bali Mwalimu Nyerere mwenyewe, ambaye alitaka Watanzania wajue
ilipotoka historia yake kisiasa.
Katoroki anasimulia kuwa Mwalimu
Nyerere baada ya kupata tetesi kuwa anaweza kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu,
alitafuta sehemu ya usalama na ndipo rafiki yake alipomtafutia kiwanja hicho
kilichopo Magomeni, Mtaa wa Ifunda.
“Mwalimu alikinunua kiwanja hiki
mwaka 1957. Hii ilikuwa ni baada ya kupata tetesi kuwa anaweza kuwa Waziri Mkuu
na wakati ule alihitaji ulinzi kwa kuishi katika mazingira salama, kwa kuwa
Magomeni enzi zile ndiyo ilikuwa kama Masaki
sasa hivi, akanunua na kuanza ujenzi,” anasema Katoroki.
Ulinzi wake
Katoroki anasema kwa wakati ule
ulinzi ulikuwa mdogo hivyo kwa mtu anayeanza kuchipukia kisiasa tena anayetajwa
kuweza kushika nafasi kubwa katika nchi, alihitaji kujilinda kwa kuwa lolote
lingeweza kutokea.
Aidha, Katoroki anasema historia ya
kisiasa ya Mwalimu ilianza wakati akiishi katika nyumba hii na baada ya
kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwani baada ya hapo alikwenda kuishi katika nyumba
ya serikali Sea View na baadaye Ikulu.
“Pia ni nyumba ya kihistoria kwani
aliijenga kwa kiinua mgongo chake baada ya kuacha ualimu pale Shule ya
Sekondari ya Pugu. Baada ya kuwepo tetesi na pengine mwenyewe alikuwa na
taarifa kamili, aliamua kuachana na ualimu, “ anasema Katoroki.
“Ninasema historia yake kisiasa
ilianzia katika nyumba hii kwani aliamkia katika nyumba hii kwenda kuapishwa
kuwa Waziri Mkuu na kuanza rasmi shughuli za kisiasa na ukombozi wa bara la
Afrika,” anasema.
Kingine ambacho kinaifanya nyumba hii
kuwa ya kihistoria ni pamoja na kuwa alijinyima wakati akijenga, aliishi kwa
muda wa miezi minane tu kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika
Januari 1, 1960.
Katoroki anasema pamoja na nyumba
hiyo kuwa ya pekee, Mwalimu aliwahi kuiuza baada ya kutokea mgogoro katika
familia yake iliyokuwa ikiiogombea.
“Inavyoonekana Mwalimu baada ya kuwa
Waziri Mkuu aliitelekeza nyumba hii na ndugu wakaanza kuigombania. Mwenyewe
baada ya kupata taarifa hizo aliamua kuumaliza ugomvi wa ndugu kwa kuiuza,”
anasema Katoroki.
Hata hivyo historia nyingine
iliandikwa mwaka 1973 wakati Jumuiya ya Wafanyakazi (JUWATA), ikitimiza miaka
10 tangu kuanzishwa kwake ambayo Mwalimu Nyerere alialikwa kuwa mgeni rasmi
katika sherehe hizo na Jumuiya hiyo iliamzawadia nyumba.
“Juwata walimwambia Mwalimu tunataka
kukupa zawadi, alipoifungua alikuta ni hati ya nyumba yake ambayo aliwahi
kumuuzia mtu mwingine,” anasema Katoroki.
Viongozi wa Juwata walimnunulia
Mwalimu Nyumba hiyo kutoka kwa mtu aliyemuuzia kwa Sh 35,000 na kumrudishia
mwenyewe kwa njia ya zawadi.
Aliwashukuru kwa kuirudisha mikononi
mwake. Hata hivyo alisema asingependa ibaki kwenye mikono yake kwani inaweza
kurudisha matatizo aliyoyakwepa na hivyo akaamua kuitoa kwa serikali ili
iifanye kuwa Nyumba ya Makumbusho.
Serikali kwa muda mrefu iliitelekeza
nyumba hii na hivyo kuanza kuharibika na vyombo kuanza kupotea. Hata hivyo,
Wizara ya Utamaduni ilipewa jukumu la kuisimamia nyumba hii chini ya Idara ya
Mambo ya Kale na mwaka 2002 ilikabidhiwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii
chini ya Idara ya Mambo ya Kale.
Vitu vyake
Pamoja na kuwa vitu vingi vya Mwalimu
vilipotea baada ya Mwalimu Nyerere na familia yake, ndani ya nyumba hiyo vipo
vitanda vya familia kikiwamo kile alichokilalia mwalimu mwenyewe kabla ya
kuhama.
Vitu vingine vilivyopo ni kabati la
jikoni, kabati la kuhifadhia fedha (kibubu), pasi ya mkaa, mtungi wa kuhifadhia
maji, redio ya mbao, makochi, cherehani na vyombo vya jikoni.
Pamoja na vyombo ndani ya nyumba
hiyo, kuna noti za pesa zilizokuwa zikitumika enzi za utawala wake. Pia vipo
vitabu alivyowahi kuandika kama vile; Ujamaa ni Imani, Maendeleo ni Kazi,
‘Education to Self Relience’, Tujisahihishe, Tanu na Raia, ‘Our Leadership and
Destiny of Tanzania’ na vingine vingi.
Vitu vingi vilivyopo ndani ya nyumba
hiyo vilipatikana kutoka kwa Mzee Omary (Aliyekuwa baba mlezi wa Mwalimu
Nyerere), ambaye inadaiwa kuwa baada ya kuona nyumba haina mwelekeo alivichukua
na kwenda navyo Dodoma
ambako anaishi mpaka sasa.
“Mzee huyu ametunza vitu vingi vya
Mwalimu na kama unavyoona humu ndani, hivi
vyote tumevipata kwake, tunasikia kuna vingine walichukua ndugu na sasa
wameviuza kwa watu wa makumbusho binafsi,” anasema Katoroki.
“Nia yetu ni kupata kila kitu ambacho
kilikuwamo humu ndani, vingi viliuzwa kwenye makumbusho binafsi na wao
wanaviuza kwa bei za juu hivyo si rahisi kuvipata,” anasema Katoroki.
No comments:
Post a Comment