Sanamu ya Bikira Maria na Rozali vilivyokuwa vikitumiwa na Mwalimu Nyerere wakati wa salama. picha na Maktaba
Na Maimuna Kubegeya, Mwananchi
Dar es Salaam. Moja ya urithi mkuu aliouacha
Mwalimu Nyerere kwenye familia yake ni kumcha Mungu, ambapo watu wake wa karibu
wanasema alikuwa Mkristo wa kweli ambaye alikuwa akiishi maisha ya kumcha
Mungu.
“Tangu atimize miaka 51 babu amekuwa
akifanya ibada za asubuhi na jioni hadi alipokutwa na umauti” anasema Julius
Makongoro Nyerere mjukuu wa Mwalimu Nyerere.
Anasema wakati wa uhai wake, alikuwa
yuko tayari kukupa adhabu yeyote ile ikiwa tu utakosa kufanya ibada.
“Ilifikia kipindi tulikuwa tukipewa
adhabu ya kunyimwa chakula kwa kosa la kushindwa kusali,” anasema.
Kwenye familia yao ilikuwa ni kawaida kusali novena ambayo
kwa kawaida husaliwa kila baada ya saa nane.
“Hivyo ikitokea sala hiyo ikaangukia
usiku wa manane, babu alikuwa akituamsha nyumba nzima kwa ajili ya kusali,”
anasema Julius.
Monsinyori Deogratias Mbiku mlezi na
paroko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
ni miongoni mwa watu wanaomfahamu Mwalimu Nyerere.
“Kwa mara ya kwanza nilikutana na
Mwalimu mwaka 1963, pale Nyegezi, Mwanza, alipokuja kumtembelea Fideric Mula
aliyesoma naye huko nchini Scotland.
“Nyerere hakuwa na makuu vaa yake,
ongea yake hata ushiriki wake katika masuala mbalimbali ya kijamii, ulikuwa ni
wa kawaida kabisa”.
Kila mahali alipokwenda alikuwa
akiomba apelekwe kanisani na hakusita kuwaambia walinzi wake; “Nipelekeni
kanisani mimi ni Mkristu.” Alikuwa hafichi hilo.
Mbiku anasema ratiba ya Nyerere siku
zote ilianza kwa sala. “Na siyo tu alikuwa akisali, bali alikuwa pia akitoa
“comments” zake kuhusiana na ibada,” anasema Mbiku.
Anasema pia alikuwa muwazi katika
kueleza kama ameridhishwa au hakuridhishwa,
kwa kuwa sehemu nyingi kuna namna mbalimbali za kufanya ibada.
“Alikuwa akifuatilia ibada na siyo tu
kusali kwa kutimiza wajibu,” anasema na kuongeza:
“Kwa mfano alienda kanisa moja,
akakuta wanaimba sana, yaani wanatumia muda
mwingi kuimba na kwa muda mfupi wanasali, Mwalimu hakusita kuwaambia
kinachotakiwa ni kusali muda mrefu kila mtu apate muda wa kufanya toba na siyo
kuimba kama kwenye tamasha.
“Halafu hii baba yetu kama kuna ‘tune’ ambayo watu wanaweza kudaka sawa, lakini
hii ni sala ya bwana, tusali wote” alisisitiza na kuongeza kuwa kutoa huduma za
kiroho katika Kanisa la Mtakatifu Petro kuanzia mwaka 1972 alikokuwa akisali
Mwalimu.
Mbiku anasema Nyerere alikuwa ni
zaidi ya muumini, kwani siku zote alikuwa mshauri mzuri wa masuala
yanayohusiana na ibada, akilenga kuweka mazingira mazuri ya kumwabudu Mungu.
“Nilikuwa nikimshuhudia Mwalimu akija
kusali kila siku kabla ya kwenda kazini kwake,” anasema.
Sababu hizi na nyingine nyingi
zilifanya kiongozi huyu kuingia kwenye mchakato wa kutangazwa mwenye heri mara
baada ya kifo chake.
Mbiku anasema mchakato huo si wa muda
mfupi kwani una hatua kadha wa kadha. Hivyo katika hatua za awali uchunguzi
hufanyika juu ya maisha yake.
Anasema hatua hiyo ya kwanza inaitwa
mtumishi wa Mungu, halafu hatua pili ni kuangalia miujiza inayomhusisha huyo
mtumishi wa Mungu. Hatua ya mwisho ni kumtangaza mwenye heri. Kwa kawaida
mchakato huo huanza miaka mitano baada ya mhusika kufariki dunia.
Mbiku anasema mchango wa Mwalimu
Nyerere umekuwa ukitambuliwa na watu wengi, hususani waliokuwepo katika Kanisa
Katoliki.
“Kwa mfano mwaka 1994 nilikuwa Makamu
Mkuu wa Chuo katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki huko nchini Kenya,
kilichokuwa kikihudumia nchi nane za Afrika ya Mashariki.”
“Wakuu wa chuo kile walipendekeza
Mwalimu Nyerere apewe shahada ya heshima ya Kanisa Katoliki, hivyo nikaagizwa
kwenda kumpelekea taarifa.”
“Nilirudi nyumbani na nikamsubiri
kule kanisani, baada ya kanisa nilimwambia kuwa nahitaji kuongea naye na hivyo
akanikaribisha nyumbani kwake,” anasema.
Alipofika nyumbani kwake siku ya pili
yake, alikaribishwa chai na kufanya maongezi.
“Nilimfikishia ujumbe nikimwambia
kuwa, viongozi wa chuo wamemteua yeye kupokea shahada ya heshima,” anasema na
kuongeza kuwa majibu ya Mwalimu Nyerere yalikuwa; “Asante
sana kwa kunipa
nafasi hiyo, lakini kwa sasa sitoweza kuhudhuria kwani kwa sasa hali ya nchi
siyo nzuri, kuna matatizo fulani yanayohusiana na masuala ya muungano yameingia
hivyo ninaumiza kichwa katika kuyatafutia ufumbuzi.
“Lengo langu hasa ni kuhakikisha
muungano unasimama, nisingependa kuona muungano unakufa mimi nikiwa hai.”
Mbiku anasema baada ya Mwalimu
Nyerere kuacha kupokea shahada hiyo, Kadinari Rugambwa alichaguliwa badala
yake.
Jambo hili lilinifanya niwe naamka
mapema kumuwahi na huo ndiyo ukawa utaratibu wa maisha yangu.
No comments:
Post a Comment