Saturday, October 12, 2013

Mwalimu Nyerere alimfanya kila mmoja ajione muhimu



Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akiwa na mke wake.Picha na Maktaba 
Na Julieth Kulangwa, Mwananchi

Oktoba 14 ya kila mwaka Watanzania hukumbuka siku ya huzuni, ambapo walimpoteza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia tarehe na mwezi huo, mwaka 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza alipokwenda kwa matibabu.

Madaktari walieleza kuwa kifo cha baba wa taifa kilitokana na ugonjwa wa saratani ya damu. Julius Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika huru na baadaye alikuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika.

Mwalimu alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo alikaa madarakani akiiongoza Tanzania kwa miaka zaidi ya 20.
Oktoba 14 ya kila mwaka imefanywa kuwa ya kitaifa ikitoa nafasi ya kumbuka, kutafakari aliyolitendea taifa, lakini zaidi kuenzi yote mema na mazuri kwa Tanzania aliyoipenda.

Tangu kufariki kwake mengi yamekuwa yakikumbukwa na kutajwa kama mfano na watu wa kada mbalimbali, wakiwamo viongozi.
Ni wazi na hakuna anayeweza kupinga kuwa Mwalimu Nyerere ameacha mambo mengi mazuri ya kujivunia na mfano wa kuigwa na jamii ya Watanzania.

Historia hiyo ipo katika nyanja mbalimbali kama vile siasa, elimu, uchumi hata utamaduni katika taifa la Tanzania linaloelezwa kuwa na makabila zaidi ya 120, hivyo pia kuwa na tamaduni tofauti kati ya kabila moja na nyingine, ingawa baadhi ya makabila hufanana mila na utamaduni wao kwenye baadhi ya mambo.

Katika makala haya leo, tunaangalia namna Mwalimu Julius Kambarage alivyoacha historia ya kipekee katika kuenzi utamaduni wa kabila lake na kuheshimu uhusiano katika familia na urafiki wake na watu wengine.

Ukweli wa hilo unadhihirishwa na jinsi Mwalimu alivyokuwa akitoa majina kwa watoto wake, wajukuu na jinsi alivyokuwa akiwaita kila mmoja kwa namna yake, akizingatia uasili na heshima kati yake na watu wengine.

Ndivyo ilivyo, Mwalimu aliwapa majina watoto wake akitaka kila mmoja awe na jina lenye maana kama siyo kwa familia, basi kwake binafsi.
Hapa mfano wa karibu ni namna alivyowapa majina watoto wake kwa kuwapa majina ya pili ambayo ni ya kiasili na kwa namna tofauti, huku kila jina likiwa na maana kwa familia na kwake.
Katika uhai wake, Mwalimu Nyerere alibahatika kupata watoto saba ambapo mbali na majina yaliyotokana na imani yake ya dini ya Kikristo, kila mmoja alimpa pia jina la kiasili ya Kizanaki, kabila alilotokea, ukoo wake au wa mkewe mama Maria Nyerere.

Akionyesha mfano wa kuthamini uafrika na asili yake Nyerere alimwita mtoto wake wa kwanza kwa jina la Burito au Andrew, mwingine alimwita Watiku (Anna), Magige(Emily), Nyerere (John), Makongoro (Charles) na Madaraka ambaye ni Godfrey.

Mmoja wa wajukuu zake aliyempa jina la Moringe anasema kuwa anaamini kila mtu katika familia ya mwalimu alipewa jina kwa sababu maalumu, kwani pamoja na kuwa majina mbalimbali, bado babu yao aliwaita kwa maana ya jina la kiasili.

Anatoa mfano wa baba yake yeye, (Mzee Magige) ambaye alipewa jina la baba wa Mama Maria Nyerere, hivyo Mwalimu alikuwa akimwita Magige ‘mkwe’.
“Babu alikuwa akimwita baba yangu kwa lugha ya Kizanaki ‘Tata Kyara’ akimaanisha baba mkwe, nimemsikia akimwita hivyo siku zote na hakuwahi kutumia jina lake la Magige au Emily.

Anasema hata yeye alipewa jina la Moringe ambalo ni la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine kwa sasa ni marehemu, ambaye alikuwa ni rafiki mkubwa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Mimi siku zote alikuwa akiniita ‘rafiki yangu’ kwa kuwa alinipa jina la rafiki yake kipenzi, hakuwahi kuniita kwa jina langu la Moringe hata siku moja,” anasema.
Anaongeza kuwa alifanya vivyo hivyo kwa ndugu wote akiwaita kutokana na asili ya majina yao na kwa kuwa wengi walikuwa na majina ya Kizanaki aliwaita kutokana na uhusiano au tafsiri ya majina hayo.

Moringe anasema kuwa Nyerere aliwalea watoto na wajukuu zake katika maisha yaliyolenga kuwaonyesha Watanzania kuwa kila mtu ni sawa kwa kuwa pamoja na kuwa na madaraka, hakuyatofautisha maisha yake na ya Watanzania wengi.
“Nchi hii matajiri ni wachache kuliko maskini, alitaka familia yake iishi maisha ya kawaida, yanayofanana na ya Watanzania wengi ingawa alikuwa na uwezo wa kuwafanya waishi kama wako peponi.

Hii ililenga kuonyesha kwamba alijali usawa na kutaka kila mmoja ajione muhimu katika nchi yake,” anasema Moringe.
Anabainisha kuwa Mwalimu hakutaka Watanzania wajione wanyonge kwa tabaka na walionacho na wasionacho na yeye alipinga hali hiyo kwa kuonyesha mfano.

“Isingekuwa na maana kwa babu kufanya mambo ambayo kwa Watanzania ni mageni, kama angefanya hivi pengine leo hii sisi kama familia au kama Watanzania tusingejivunia kupata mtu kama yeye,” anasema Moringe.

Anaongeza kuwa unapotaka kusisitiza jambo fulani lifanyike, mwenyewe unatakiwa kuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano na hiki ndicho alichokuwa akifanya Baba wa Taifa.

“Kama angejihusisha na biashara nyingine wakati akiwa kiongozi wa nchi, maana yake angetengeneza mwanya kwa viongozi wengine kufuata nyayo zake na hii ingeweza kutengeneza mianya ya rushwa na ukiukwaji wa maadili,” anasema Moringe. 

Akizungumzia yeye kutaka kujiingiza katika siasa anasema atafuata nyayo za babu yake ambaye kabla alitumikia taaluma yake na baadaye ndipo akajiingiza huko.
“Ninapenda kufuata nyayo za babu, alisoma, akawa mwalimu na baadaye ndiyo akajiingiza katika siasa, nami nitafanya hivyo, sasa hivi ni wakati wangu wa kuitumikia taaluma yangu mpaka pale nitakaporidhika ndipo nitaingia kwenye siasa,” anasema Moringe.
                                            

No comments: