Mtoto wa kwanza wa Hayati Baba wa
Taifa, Madaraka Nyerere
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Kwa ufupi
Asema viongozi wa sasa wameshindwa kufuata nyayo
za baba yake, Mwalimu Nyerere na wapo hatua 20 nyuma.Pia anaamini vyama vya
upinzani vinaweza kupata mafanikio dhidi ya CCM katika chaguzi zijazo ikiwa
vitaungana kukikabili chama hicho tawala.
Mtoto wa kwanza wa Hayati Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aitwaye Madaraka, amesema viongozi wa sasa
wameshindwa kufuata nyayo za kiongozi huyo kutokana na sababu ambazo amesema
“haziko wazi”.
Katika mahojiano yake na gazeti hili,
Madaraka anasema: “Mazingira ya sasa hayaruhusu malengo ya uadilifu kuenziwa
kwa sababu nafasi za umma zinakubalika sasa kuwa ni maeneo ya kujinufaisha mimi
kwanza, halafu Tanzania Mungu akipenda”.
Yafuatayo ni mahojiano kamili na
Madaraka.
Mwananchi: Ni miaka 14 sasa tangu
kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, unaizungumziaje miaka hiyo
kimaisha katika familia, bila kuwapo kwa Mwalimu?
Madaraka: Binadamu tumeumbwa na uwezo
wa kukabiliana na kuondokewa ndugu na jamaa zetu wa karibu. Majonzi yalikuwa
makubwa baada ya kufariki Mwalimu, lakini tunatambua kuwa kuna umuhimu wa
kuomboleza na baadaye kuendelea kukabiliana na changamoto za kila siku za
maisha. Na yeye angetarajia hivyo.
Mwananchi: Mwalimu Nyerere alikuwa
kiongozi wa nchi, ni zipi fikra au mtazamo wako jinsi viongozi wetu wa sasa wanavyomuezi
kwa kuwa wafuasi wa nyayo zake?
Madaraka: Hebu tuseme tu bila unafiki
kuwa katika masuala mengi ya uongozi, hasa ya uadilifu, suala la kumuenzi
Mwalimu Nyerere ni lengo ambalo viongozi wengi wa sasa wanaweza kuwa wanalo,
lakini kutokana na sababu ambazo haziko wazi basi hilo lengo siku zote
halikamatiki, liko hatua kumi mbele yao. Na kila wakielekea kama kulifikia na
kulitimiza basi wanateleza na kuanguka na lengo hilo linawaacha hatua nyingine
20 mbele.
Mazingira ya sasa hayaruhusu malengo
ya uadilifu kuenziwa kwa sababu nafasi za umma zinakubalika sasa kuwa ni maeneo
ya kujinufaisha mimi kwanza, halafu Tanzania Mungu akipenda.
Mwananchi: Miongoni mwa mambo ambayo
Mwalimu Nyerere aliyaenzi na kuyasimamia enzi za uhai wake, ni Muungano. Kwa
maoni yako unadhani hili linaenziwa vipi? (rejea mvutano wa sasa wa Serikali
mbili, tatu nk, unatokana na mchakato wa Katiba Mpya).
Mwananchi: Nitumie msemo wa kisiasa
kuwa sasa hivi suala la kutengua Muungano linazungumzika. Wakati waasisi
wenyewe wapo hai wale waliofikiria kutengua Muungano walipata kigugumizi au
walishindwa kuwa wazi na fikra zao. Sasa hivi inaelekea kuna baadhi ya makundi
ya viongozi pande zote mbili za Muungano hawataki Muungano, lakini wanashindwa
kuwa wazi kutetea msimamo wao huo. Ni sauti chache sana utazisikia zikisimama
bila kutetereka kutetea kuwepo kwa Muungano.
Ni dhahiri kuwa sauti za kutaka
Zanzibar iachane na Muungano zimekuwa na nguvu zaidi kuliko zile ambazo
zinatetea Muungano. Naamini kuwa viongozi wanaozungumzia Muungano wa mkataba
hawajapata ujasiri wa kisiasa wa kusema kuwa hawataki kabisa Muungano.
Naweza kuwa siko sahihi, lakini
naamini kuwa yeyote anayejaribu kutetea umoja mkubwa zaidi kati ya Bara na
Visiwani na siyo mfano tu wa umoja anapingana na mtazamo uliojengwa juu ya
fikra kuwa maendeleo ya Zanzibar yanakwamishwa na kuwepo ndani ya Muungano.
Kwa sababu ni baadhi ya wanasiasa
ndiyo wanajenga fikra hizi tunaweza kusema kuwa ni siasa ndiyo inasukuma ukweli
badala ya ukweli kusukuma siasa. Kwa maoni yangu, ukweli wa kisiasa unajengwa
juu ya kushinda uchaguzi ujao.
Hilo ndilo jambo la msingi. Kusimamia
ukweli tofauti na hapo kunaweza kusababisha kushindwa uchaguzi. Ukweli
ninaoamini mimi ni kuwa siku zote umoja huleta nguvu, utengano udhaifu. Hii ni
kweli katika suala la uchumi na hata kisiasa.
Lakini iwapo hilo ndilo wananchi
wanataka, huwezi kulikwepa. Matokeo yake ni Serikali tatu. Umoja wa kweli
ungekuwa Serikali moja na sauti za ‘mimi’ na ‘wewe’ (Zanzibar na Bara)
zingepotea na kuchukuliwa na suala la ‘sisi’ (Watanzania). Lakini suala la
Serikali moja lilionekana haliwezekani, mwaka 1964 na la Serikali mbili
likaonekana mwafaka. Kwenda kwenye Serikali tatu ni kama kupiga hatua moja
nyuma katika kuulinda Muungano.
Mimi nalaumu uwezekano wa kupatikana
kwa rasilimali ya mafuta kama kichocheo kikubwa cha kuyumbisha Muungano. Siku
zote pesa na utajiri ndiyo hugombanisha ndugu. Ndugu wenye utajiri wana fursa
nyingi zaidi za kutoelewana kuliko ndugu wasio na utajiri.
Ukweli ni kuwa kama huna mali
hutakuwa na ugomvi kuhusu mali na ndugu yako. Mara tulipopata harufu ya mafuta
chini ya Bahari ya Hindi basi masuala ya kuukosoa Muungano yakapamba moto.
Mwananchi: Nje ya Serikali ambako
Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi, kuna familia ambako alikuwa baba. Ndani ya
familia je, mnamuenzi vipi Baba wa Taifa?
Madaraka: Ukiwa ndani familia huna
uchaguzi juu ya kama unataka kumuenzi Mwalimu au la. Watu watakupachika
matarajio yao na kiwango cha ulinganishi kimeshawekwa na Mwalimu Nyerere.
Kwa hiyo mwanafamilia anapokuwa na
mwenendo ambao haufanani na hicho kiwango kinachotarajiwa, basi wengi
wanashangaa. Mfano, mimi nikivuta bangi nitaandikwa kwenye gazeti, lakini
kitendo hicho kikifanywa na Mtanzania ambaye baba yake hana wadhifa mkubwa wa
uongozi hiyo haiwezi kuwa habari.
Labda wengine watasikitishwa na suala
hilo. Watakaofurahi ni wale ambao wanakubali kuwa uadilifu katika uongozi na
utumishi wa umma ni suala lisilowezekana.
Baadhi ya wanafamilia tunasimamia
kutangaza Kijiji cha Butiama kama eneo la kihistoria na la kiutamaduni. Wageni
wengi bado wanafika kutembelea Butiama mahususi kwa sababu ndipo alipozaliwa na
kuzikwa Mwalimu Nyerere.
Mwananchi: Ni tabia ya viongozi wengi
wa Afrika kujilimbikizia mali wanapokuwa madarakani. Ukiwa kiongozi wa familia
ya Mwalimu Nyerere, unaweza kueleza tofauti yao na Baba wa Taifa? Je, yeye
aliwaachia mali kiasi gani (kwa maana ya fedha, nyumba na mashamba)?
Madaraka: Awali, mimi siyo kiongozi
wa familia ya Mwalimu Nyerere. Hatuna nafasi hiyo ndani ya familia.
Mimi naamini kuwa mtu ambaye hana
tamaa ya kujilimbikizia mali huzaliwa hivyo. Huwezi kupenda kujilimbikizia mali
na utajiri (kwa njia halali au vinginevyo) halafu ukakaa madarakani kwa miaka
23 bila tabia yako hiyo kujitokeza katika matendo yako au ya wale waliokuzunguka.
Ukweli utabainika tu.
Sasa inawezekana kuwa kiongozi
akashika wadhifa akiwa mwadilifu halafu akiwa madarakani akapata vishawishi vya
kujilimbikizia mali.
Hapa ndiyo natoa hoja kuwa kama wewe
ulizaliwa kuwa mtu usiyesumbuliwa na kukosa mabilioni ya shilingi kwenye
akaunti yako basi hivyo vishawishi havitakusumbua. Lakini tofauti ya hivyo
utashawishika kujitajirisha mwenyewe na kusahau wajibu kwa umma.
Sisi hatukuachiwa mali yoyote ambayo
ilitokana na kipato chake. Kuna nyumba ile ya Msasani ambayo aliijenga kwa
mkopo ambao hakuweza kuulipa wakati anastaafu na aliamua kuikabidhi Serikali,
lakini Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi ilipitisha uamuzi wa kulipa au kufuta
deni na akakabidhiwa nyumba. Kuna nyumba ndogo ambayo alijenga akiwa Rais, iko
Butiama.
Vilevile, baada ya vita vya Kagera
alijengewa nyumba na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambayo baadaye
Serikali ilichukua jukumu la kuikamilisha. Awali, ni wanajeshi wenyewe walikuwa
wanakatwa mishahara yao kuchangia ujenzi wa nyumba hiyo.
Nyumba nyingine ipo Butiama na
alijengewa na CCM baada ya viongozi wenzake kuamua kuwa nyumba yake aliyojenga
Butiama ni ndogo sana na haistahili kutumiwa na Rais wa nchi.
Alipewa eneo la shamba na Kijiji cha
Buturu, jirani na Kijiji cha Butiama, ingawa kumekuwa na mbinu za kutaka kupora
hilo shamba zinazoongozwa na baadhi ya viongozi wa zamani wa kijiji hicho.
Mwananchi: Novemba 2004, familia ya
Baba wa Taifa ililalamikia Sheria ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa iliyopitishwa na
Bunge, kwa hofu kwamba ingepoteza uhalali wa kumilikia baadhi ya mali za
Mwalimu Nyerere. Ni kipi kinajitokeza kama changamoto tangu kupitishwa kwa
sheria hiyo?
Madaraka: Jibu hili litakuwa refu
kidogo kwa kuwa lina masuala mengi ndani yake. Mimi nilikuwa mmojawapo wa
wajumbe wa kamati ndogo ya Serikali iliyoshiriki kwenye kazi ya kuchangia
vipengele vya muswada wa ile sheria.
Nilikuwa ninaiwakilisha familia
pamoja na dada yangu Rosemary. Kuna baadhi ya vipengele ambavyo tulipendekeza
kama familia wakati wa kuandaa muswada na waziri mhusika alienda bungeni kutoa
tamko tukiamini kuwa mapendekezo yetu yangekuwa sehemu ya sheria, lakini waziri
alipofika huko hakuchukua mapendekezo yote kutoka upande wa familia.
Changamoto siyo nyingi, lakini kuna
jambo la msingi ambalo nafikiri linahitaji kutolewa uamuzi haraka. Sheria
inaweka wazi kuwa kazi ya kuwaenzi waasisi wa Tanzania ni jukumu la pamoja na
kuwa yeyote anayemiliki kumbukumbu za Mwalimu Nyerere na za Sheikh Abedi Amani
Karume ataendelea kumiliki hizo kumbukumbu, lakini atatarajiwa kushiriki kwenye
kizitunza kwa mujibu wa sheria hii na sheria nyingine zilizopo.
Tatizo mojawapo liliibuka wakati
tukishiriki mijadala ya kuandaa muswada wa sheria lilikuwa umiliki wa hotuba za
Mwalimu Nyerere. Kwa mujibu wa wawakilishi wa Serikali ni kuwa hotuba zote ambazo
Rais aliye madarakani anazitoa ni mali ya Serikali. Na wawakilishi wa Serikali
katika ile kamati walichukua huo msimamo kwa kuzingatia kipengele kimojawapo
cha Sheria ya Usalama wa Taifa.
Nakumbuka walisema mambo mawili:
Kwanza, kuwa nyaraka yoyote yenye nembo ya Serikali inayotumika kuandikia suala
lolote ni mali ya Serikali. Pili, kuwa nyaraka yoyote anayeiandaa mtumishi wa
Serikali akiwa madarakani ni mali ya Serikali. Kwa mantiki hii, Rais
anayeandika (au kuandikiwa) hotuba akiwa madarakani hamiliki hizo hotuba. Hizo
ni mali ya Serikali.
Kama hii ndiyo fasiri sahihi ya
sheria hii mimi naona ina hitilafu kubwa. Nakubali kuwa karatasi aliyotumia
Mwalimu Nyerere kuandikia hotuba zake ni mali ya Serikali, lakini sikubali kuwa
mawazo yake yanaweza kuwa mali ya Serikali. Unawezaje kumiliki mawazo ya
kiongozi yeyote yule?
Tukijadili kipindi cha utawala wa
Serikali ya Tanzania kati ya 1961 hadi 1985 alipostaafu, ni nadra kuzungumzia
‘mawazo ya Serikali ya Tanzania’ lakini tunazungumza kila wakati kuhusu ‘mawazo
na fikra za Mwalimu Nyerere’.
Kwa mujibu wa Serikali kama haya
‘mawazo na fikra za Mwalimu Nyerere’ yameandikwa kwenye karatasi yenye nembo ya
Serikali na iwapo yalitolewa yeye akiwa Rais, basi vyote hivyo ni mali ya
Serikali. Zaidi ya hayo kuna matukio ambayo ambayo yanaleta mkanganyiko zaidi
kuhusu huu msimamo wa Serikali. Akiwa madarakani, kampuni ya Oxford University
Press ilichapisha hotuba zake na Mwalimu Nyerere alilipwa mrabaha kutokana na
mauzo ya vile vitabu vyenye hotuba zake. Baada ya Mwalimu kufariki Oxford
University Press waliilipa familia mrabaha, kama warithi wake, kutokana na
mauzo ya hotuba hizo hizo.
Sasa tukikubali hoja kuwa hotuba zile
ni mali ya Serikali kuna kasoro kisheria kwa Mwalimu kuweza kuchapisha zile
hotuba akiwa madarakani na kulipwa mrabaha, na vilevile kuna kosa kisheria kwa
familia yake kulipwa mrabaha na Oxford University Press.
Tunaweza kuamini kuwa kwa sababu
Mwalimu Nyerere alichapisha hotuba zake akiwa madarakani, ilihitaji ujasiri
mkubwa kumfahamisha kuwa alikuwa anavunja sheria.
Sasa hivi hayuko madarakani na ni
rahisi sana kwa Serikali kutamka rasmi kuwa alifanya kosa na kuwa hata familia
yake haikustahili kupokea malipo toka Oxford University Press. Tukiwa kwenye
ile kamati tuliomba Serikali itamke hivyo, lakini mpaka leo bado haijatoa
tamko.
Lakini hata ikitamka itakuwa bado
kuna tatizo lingine. Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, katika mfululizo wa vitabu
vilivyochapishwa na Mkuki na Nyota Publications, amechapisha hotuba zake nyingi
alizotoa akiwa madarakani (1995 – 2005). Sidhani kama Mkuki na Nyota wanailipa
Serikali ya Tanzania mrabaha kutokana na mauzo ya vitabu hivyo: Uwazi na Ukweli
1 – 5.
Hotuba na maandishi ya Mwalimu
Nyerere vimekuwa mali ya kila mtu siku hizi, suala ambalo mimi naona si sahihi.
Tupo warithi wake na tunastahili angalau kuombwa ruhusa kutumia hizo hotuba na
maandishi.
Nafikiri wakati umefika kuangaliwa
tena hili suala na kubainisha kasoro zinazojitokeza kwenye msimamo wa Serikali
kuhusu umiliki wa hotuba za Mwalimu Nyerere. Hatusemi kuwa hotuba zote ni mali
ya Mwalimu Nyerere ila tunaamini kuwa sehemu kubwa ya hotuba alizotoa akiwa
madarakani na baada ya kung’atuka ni mali yake.
Mwananchi: Katika muktadha mzima wa
uhusiano wa familia ya Mwalimu Nyerere na Serikali, ni wakati gani shughuli za
Makumbusho ya Mwalimu Nyerere zinatofautina na shughuli za familia hasa katika
makumbusho yaliyopo Butiama?
Madaraka: Kimsingi kazi wanayofanya
Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere na malengo ya familia hayatofautiani sana
kwa sababu nia ni kutunza/kuhifadhi na kuendeleza kumbukumbu za Mwalimu
Nyerere. Inawezekana kuwa Makumbusho wanayo majukumu ya ziada, lakini lengo la
msingi linafanana.
Mwananchi: Kwa jinsi siasa za nchi
yetu zinavyoendeshwa, wewe binafsi una matarajio yoyote ya kuingia kwenye siasa
kwa maana ya kuogombea nafasi ya ubunge au urais kama wananchi watakuhitaji?
Madaraka: Kwanza Sina mawazo ya
kugombea urais. Pili ukichukulia kama uongozi ni wajibu niko tayari kushiriki
chaguzi za ubunge, lakini ukichukulia uongozi kama fursa ya kuitwa “mheshimiwa”
na kupata mshahara na posho ya uhakika huko sitajitokeza.
Wajibu unaoweza kunisukuma mimi
kuomba ubunge ni iwapo wale wanaojitokeza kama wagombea kwenye jimbo ni watu
ambao nikijipima nao naona kuwa naweza kuwa kiongozi bora kuliko wao.
Lakini nasikia kuwa kampeni za ubunge
zinagharimu pesa nyingi, ambazo mimi sinazo. Kwa hiyo uamuzi wa kujiingiza
kwenye kampeni za aina hii unaibua maswali mengine mengi. Nikope pesa kugombea
ubunge? Siwezi. Niombe pesa kugombea ubunge? Kwa nani? Kwa masharti gani? Kuna
mtu atatoa pesa bila kutarajia faida fulani?
Nikipata msukumo wa huo wajibu, na
nikipata majibu yenye kuridhisha ya baadhi ya haya maswali (na mengine ya aina
hiyo) nitaingia kwenye pirikapirika za siasa.
Mwananchi: Unavitazama vipi vyama vya
upinzani nchini, unadhani kwa jinsi vinavyoendeshwa ni ipi nafasi yao katika
chaguzi zinazokuja kwa maana ya kupata nafasi ya kuongoza nchi (urais)?
Madaraka: Vyama vya upinzani vina
jukumu kubwa la kimfumo la kukihangaisha, kwa kukosoa sera na utendaji, CCM na
inapowezekana kukiondoa madarakani kupitia chaguzi ili wale wanaokuwa na fikra
kuwa kuongoza serikali ni suala la kudumu watafakari vyema wanapochukuwa uamuzi
unaoathiri maisha ya wananchi.
Mara nyingi wanaokaa madarakani muda
mrefu hufikia kujisahau, hasa pale vyama vya upinzani vinapokosa nguvu ya
kisiasa.
Lakini katika chaguzi za 2010 tumeona
kuwa Chadema kimepata nguvu kubwa kuliko ambavyo imewahi kutokea kwa chama cha
upinzani tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi.
Iwapo Chadema na vyama vingine vya
upinzani vinataka kuongeza mafanikio katika uchaguzi unaokuja, basi hawana budi
kushirikiana katika kukikabili Chama Cha Mapinduzi.
Lakini iwapo vyama vya upinzani
vitafanikiwa dhidi ya Chama Cha Mapinduzi kutategemea pia wagombea wa urais ambao
watateuliwa kuwakilisha vyama vyao.
Kuna viongozi ambao wanahusishwa na
upungufu katika uadilifu, na uteuzi wao kama wagombea kwa upande wa CCM unaweza
kuongeza nguvu ya vyama vya upinzani. Kwa kifupi, siyo rahisi kuzungumza sasa
kuhusu yanayoweza kutokea kwa kuwa masuala mengi hayajajulikana.
Kwa nyongeza, mimi naamini baadhi ya
viongozi wa upande wa upinzani wanapaswa kuonekana kuwa ni viongozi ambao
wanastahili kukabidhiwa nchi kuongoza. Kwa mfano, iwapo yule mbunge aliyetolewa
kwa nguvu bungeni ameteuliwa kuwa waziri mwaka 2015, baada ya chama chake
kushinda Uchaguzi Mkuu, pale anapotofautiana mawazo na rais au waziri mkuu wake
tutegemee kuwa ataendelea kuonyesha tofauti zake za mawazo kwa njia ya vitendo,
na siyo kwa kujenga hoja?
Kwa mtindo huo Baraza la Mawaziri
litahitaji mabaunsa. Lakini nikisema hivi wala sidharau nguvu ya chama chake.
Natoa hisia tu ambazo naamini
wapigakura wengi wanaweza kuwa nazo na ambazo zinaashiria kuwa labda ni vyema
kurekebisha utaratibu wa kukabiliana na upinzani wa kisiasa.
Kwa kusema “kurekebisha utaratibu wa
kukabiliana na upinzani wa kisasa” namaanisha kuwa wale wanaoona kuwa nguvu
ndiyo suluhisho la kutoelewana waanze kutumia hoja zaidi kusisitiza yale ambayo
wanaamini yanakiukwa na wapinzani wao. Wawaelimishe na kuwashawishi wapigakura
ili watambue hizo hitilafu na hatimaye wale wanaodhaniwa hawazingatii misingi
ya haki na usawa katika harakati za ushindani wa siasa waweze kuondolewa
madarakani kwa njia ya kura.
Kuna hatari ya mifano ya aina hii
kupenyeza katika maisha ya kila siku ya wananchi ambao wataona kuwa njia pekee
ya kutafuta haki ni kutumia nguvu.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment