Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe ameitupia lawama Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kwa kile
alichokieleza kulala kwao siku za mapumuziko na sikukuu kunarudisha nyuma
ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri Mwakyembe aliyasema hayo jana
wakati wa ziara ya kikazi bandarini hapo akiwa ameongozana na Mkurugenzi
Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Omari Issa.
Mwakyembe alisema watendaji na
viongozi wa bandari, wamekuwa wakifanya kazi saa 24 ili kuhakikisha meli zinashusha
mizigo haraka na wahusika wanachukua mizigo hiyo pasipo vikwazo.
“Bandari wanafanya kazi saa 24 kwa
siku saba za wiki bila kupumzika, lakini wenzetu wa TRA wao sikukuu na siku za
mwisho wa juma wanalala hali hii inaturudisha nyuma kimapato,” alisema Dk
Mwakyembe.
Aliongeza: “Nchi bado ipo nyuma,
tunahitajika kuchapa kazi usiku na mchana kuhakikisha tunasonga mbele na hii
itafanikiwa ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake ipasavyo.”
\
Alisema kama TRA wataanza kufanya
kazi kila siku, hakuna shaka kwamba taasisi za fedha (benki) nazo zitaiga hatua
hiyo.
“Huwezi kusema kufanya kazi kila siku
watahitaji kuongezewa fedha, hapana kwani wanalipwa fedha nyingi. Nitaendelea
kufanya mawasiliano nao kuona ni jinsi gani suala hili tunaweza kulimaliza.”
Aidha, amewataka wamiliki wa Bandari
Nchi Kavu (ICDs), kufanya kazi ya kutoa mizigo ya wateja wao kila siku ili
kuepusha usumbufu usio wa ulazima.
“Unakuta mtu anahitaji kutoa mizigo
yake lakini wahusika siku za mapumziko hawafanyi kazi. Kwa nini wasifanye kazi
kila siku kama bandari,” alihoji Mwakyembe.
Naye Mtendaji Mkuu wa BRN, Omari Issa
alisema ameamua kufanya ziara hiyo kujionea changamoto wanazokutana nazo ili
kuona ni jinsi gani wataweza kuzitafutia ufumbuzi.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari,
Awadhi Massawe alisema changamoto wanazokabiliana nazo ni ufinyu wa maeneo ya
kuhudumia meli na kuhifadhi shehena za mizigo.
No comments:
Post a Comment