Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani Nchini (Necta),Dk Joyce Ndalichako PICHA|MAKTABA
Na Fredy Azzahi, Mwananchi
Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa
Baraza la Mitihani Nchini (Necta),Dk Joyce Ndalichako, ameanza likizo ya mwaka
mmoja kwa kile kilichoelezwa kuwa anafanya utafiti juu ya uendeshaji wa
mitihani nchini.
Akizungumza na Mwananchi jana, Dk
Charles Msonde ambaye ndiye anayekaimu nafasi ya Katibu Mtendaji wa Necta,
alisema Dk Ndalichako amechukua likizo ya mwaka mmoja kwa ajili ya kufanya
utafiti huo.
Dk Msonde alisema kuwa, likizo ya Dk
Ndalichako ilianza Oktoba Mosi mwaka huu na itamalizika Septemba mwakani.
“Amechukua sabbatical leave, kwa
wanataaluma ama watu walio kwenye ngazi kama zetu wanaweza kuchukua likizo kama
hii. Yeye atakuwa anafanya utafiti unaohusu uendeshaji wa mitihani hapa nchini
na pia ataangalia mambo ya matumizi ya alama za maendeleo za mwanafunzi
(continuous assessment – CA),” alisema Dk Msonde:
“Utafiti huo utakuwa na manufaa kwa
shirika na kwa kuwa yeye ni Rais wa Mabaraza ya Mitihani Afrika atapata nafasi
ya kuangalia wenzetu wanafanya nini, kwa hiyo utafiti wake ataufanya ndani na
nje ya nchi. Utafiti huu utakuwa na manufaa kwa baraza na nchi nzima.”
Agosti mwaka huu Mwananchi ilifanya
mahojiano Maalumu na Dk Ndalichano ambapo alizungumzia vitu mbalimbali ikiwamo
kile alichosema ni tishio kwa Necta.
Alisema kuwa,kitu ambacho anaona ni
tishio kwa baraza hilo ni mitizamo ya watu ambao kwa kiasi kikubwa wanakataa
ukweli.
“Suala la ukweli unataka lisiwe
kweli, mimi naona hiyo ni hatari mbaya zaidi, huwezi kutibu tatizo bila kujua
ukweli, ili tuweze kuboresha elimu lazima tukubali ukweli na kujirekebisha,”
alisema Dk Ndalichako.
Alizungumzia pia ubora wa mitihani na
kusema, mitihani inayotungwa na Necta ubora wake upo juu pamoja na usahihishaji
wake.
Alisema mfumo wa kila mwalimu
anasahihisha swali lake ni wa kipekee na Tanzania ni moja kati ya nchi za
mwanzo kutumia mfumo huo.
“Kuna nchi mtu anapewa burugutu la
mitihani ya watoto anaenda nayo nyumbani kusahihisha akishamaliza analeta
majibu kisha watoto wanatangaziwa. Sisi mfumo wetu ni bora na sijui kwa nini
watu wanakuwa na mtizamo hasi na Necta, sifa kubwa ya baraza lolote lile la
mitihani ni kutoa majibu yanayofanana na hali halisi ya elimu ilivyo” alisema.
“Kwetu sisi tunachotaka siku zote
kuona mtu anapewa kile anachostahili, watu wengine wanasema mitihani
inayotungwa na kupewa watoto wote siyo sawa kwa sababu kuna baadhi ya shule
walikuwa hawana walimu au vitabu, sasa swali la kujiuliza nani alitakiwa kutoa
hivyo vitabu?” alisema Dk Ndalichako.
No comments:
Post a Comment