Na Sitta Tumma, Mwanza
SIKU moja baada ya Jeshi la Polisi
mkoani hapa kulazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wananchi na
wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), waliokuwa wakiandamana
kutoka Uwanja wa Furahisha kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, mbunge wa Nyamagana
jijini Mwanza, Ezekiel Wenje (CHADEMA), amekamatwa akituhumiwa kutenda makosa
mawili.
Wenje alishikiliwa jana majira ya saa
5 asubuhi kwa mahojiano na Jeshi la Polisi yaliyodumu takribani saa nne.
Mbunge huyo aliitwa polisi kwa ajili
ya mahojiano kuhusiana na tuhuma za kuchochea maandamano na yeye kuandamana
bila kibali, jambo lililosababisha ghasia na uvunjifu wa amani.
Inadaiwa na polisi kwamba mbunge huyo
juzi aliongoza maandamano ya wafuasi wa CHADEMA na wananchi kutoka Uwanja wa
Furahisha kuelekea ofisi ya mkuu wa mkoa, yalikokuwa yakifanyika mazungumzo
baina ya Mkuu wa Mkoa Evarist Ndikilo na ujumbe ulioongozwa na mbunge wa
Ilemela, Highness Kiwia kuhusu hatima ya meya, naibu wake, na madiwani watatu
waliofukuzwa kinyume cha sheria.
Wenje aliyeongozana na mwanasheria
wake, Charles Kiteja, baadhi ya madiwani wa Nyamagana na Ilemela na viongozi wa
CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi, alifika katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza (RCO), majira ya saa 5 asubuhi.Akiwa huko, RCO
Joseph Konyo na baadhi ya maofisa wengine wa jeshi hilo, walitumia takribani
dakika 45 wakimhoji mbunge huyo kuhusiana na tuhuma hizo dhidi yake.
Wenje ambaye anasifika kwa msimamo na
ushawishi mkubwa kwa wananchi ndani na nje ya jimbo lake la Nyamagana,
aliliambia gazeti hili kwamba: “Polisi wanadai nimewaambia wananchi kwamba
Ndikilo na Matata ni adui wa wananchi, na wakiwaona wawazomee.
“Wananituhumu pia kuongoza
waandamanaji kutoka viwanja hivyo vya Furahisha kisha kuelekea ofisi za mkuu wa
mkoa, pamoja na kusababisha barabara ya Nera-Makongoro Mission kuzibwa kutokana
na ghasia zilizoibuka.”
Alipoulizwa kuhusiana na kushikiliwa
kwa mbunge huyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, na Naibu Kamishna wa jeshi hilo, Ernest Mangu
alikiri Wenje kushikiliwa.
“Kweli mheshimiwa Wenje tumemshikilia
kwa mahojiano. Anatuhumiwa mambo mawili ya kuchochea maandamano na yeye
kuandamana bila kibali cha polisi.
“Tunataka mheshimiwa Wenje atueleze
alipata wapi idhini ya kuandamana bila kibali, na aliandamana na akina nani.
Asipotutajia alioandamana nao tutamng’ang’ania yeye hadi kieleweke,” alisema
RPC Mangu.
Juzi majira ya alasiri, ziliibuka
ghasia baada ya Jeshi la Polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi,
kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA.
Ghasia hizo zilitokea wakati wa
maandamano ya chama hicho yaliyolenga kupinga uchaguzi ‘batili’ wa Meya wa
Manispaa ya Ilemela, Henry Matata na Naibu wake, Swila Dede, pamoja na kupinga
kufukuzwa madiwani watatu wa chama hicho kinyume cha taratibu, kanuni na sheria
za nchi.
Madiwani waliofukuzwa na Matata
kinyume cha sheria na kata zao kwenye mabano ni Abubakar Kapera (Nyamanoro),
Malietha Chenyenge (Ilemela), na Dany Kahungu (Kirumba).
Tarime hakukaliki
Wakati sakata la meya huyo likizidi
kuchemka jijini Mwanza, Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika hatua inayozidi
kuushangaza umma, kimeingilia kati na kuingizwa madiwani wake watatu wa viti
maalumu kinyume na utaratibu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
Hatua hiyo ilipingwa vikali na
madiwani wa CHADEMA wakiongozwa na Charles Ndesi Mbusiro wa Kata ya Turwa,
waliosusia kikao cha uchaguzi na kuitaka serikali izingatie hati ya awali
iliyotolewa na Katibu wa Bunge, Thomas Kashililla iliyotaka utaratibu wa uwiano
wa idadi ya kila madiwani wa vyama waliochaguliwa katika kata mbalimbali
kutimia moja ya tatu yao.
“Sisi tumesusia kikao cha kuchagua
mwenyekiti wa halmashauri hiyo na makamu wake na kuamua kupanga mipango yatu
thabiti kwa ajili ya kuipinga hati iliyowaingiza madiwani wa viti maalumu;
Prischal Matinde, Saluma Abubakari na Adina Chambiri ili utumike ule ulioletwa
na Katibu wa Bunge Kashilila wa kutumia moja ya tatu ya madiwani wa kuchaguliwa
kisheria,” alisema Ndessi.
Wajumbe wa halmashauri hiyo
waliosusia kikao hicho ni Peter Marwa Chacha (Kata ya Nyandoto), Mbusiro
(Turwa), Christopher Chomete (Sabasaba), Thobias Elias Ghati (Nyamisangura) na
Mbunge wa viti maalumu, Esther Nicholous Matiko.
Hatua hiyo ilisababisha kikao kubaki
na wajumbe wake saba, wote wakiwa madiwani wa CCM wakiwamo mbunge wa Jimbo la
Tarime Nyambari Chacha Nyangwine na Waziri wa Ajira na Kazi, Gaudensia Kabaka
hivyo kufikisha idadi ya wajumbe 12, na hivyo kuendesha uchaguzi uliomchagua
diwani Daudi Mrimi Wangwe (mdogo wa marehemu Chacha Wangwe) kuwa mwenyekiti wa
halmashauri na makamu wake Godfrey Michael Masubo.
Uchaguzi huo umekuja baada ya hati
yake kukabidhiwa kwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Venance Mwamengo Agosti 16
mwaka huu baada ya kuvunjwa kwa baraza la madiwani na mwenyekiti wake Amos
Sagara, kulipotangazwa rasmi Julai 1, mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Mara,
John Gabriel Tuppa.
Source: www.freemedia.co.tz/daima/
No comments:
Post a Comment