Imetimia miaka 50 tangu Martin Luther
King alipotoa hotuba yake ya kihistoria. King aliyekuwa mwanaharakati wa
kupigania haki za watu weusi Marekani, alizungumzia ndoto yake ya kuwa na nchi
yenye usawa kwa wote.
"Nina ndoto kwamba siku moja
watoto wangu wanne wataishi kwenye nchi ambapo hawatatathminiwa kulingana na
rangi ya ngozi yao bali kulingana na tabia yao." Ilikuwa tarehe 28 Agosti
mwaka 1963, pale ambapo Martin Luther King na maelfu ya Wamarekani weusi
waliandamana mjini Washington kudai uhuru na haki sawa ya kupata ajira kwa watu
weusi. King alikuwa miongoni mwa waandalizi wa maandamano hayo na mmoja wa watu
waliotoa hutoba siku hiyo. Hotuba yake ya I have a dream - yaani nina ndoto -
inaelezea mustakabali anaoutamani kwa nchi yake. Alitaka Marekani iwe na umoja
na watu wasibaguliwe kwa sababu ya rangi ya ngozi yao.
"Hatuwezi kuridhika iwapo mtu
mweusi kutoka Mississippi hana haki ya kupiga kura na mtu mweusi anayeishi New
York haoni sababu ya kupiga kura," alisema King katika hotuba yake. Miaka
hamsini baadaye, sehemu fulani ya ndoto ya Martin Luther King imetimia. Kwa
mara ya kwanza Marekani inaongozwa na rais mweusi.
Ubaguzi bado tatizo sugu
Barack Obama ni rais wa kwanza mweusi
wa Marekani Barack Obama ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani
Barack Obama leo ataongoza
maadhimisho ya miaka 50 ya hotuba ya King. Atatoa hotuba kwenye jengo la
kumbukumbu ya Lincoln mjini Washington - mahali pale pale ambapo King alielezea
ndoto yake miaka 50 iliyopita.
Obama ameeleza kuwa mafanikio yake
kama mwanasiasa mwenye mamlaka makubwa zaidi Marekani, yamejengwa juu ya
misingi ya juhudi za Martin Luther King na wenzake. Anaamini kwamba asingekuwa
rais wa Marekani leo, kama wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi wasingekuwa
tayari kuvumilia vitisho, mateso na hata kufungwa jela.
Hata hivyo, ubaguzi wa rangi bado ni
tatizo sugu kwenye baadhi ya maeneo ya Marekani. Kisa cha kijana Trayvon Martin
aliyepigwa risasi na Mmarekani mwenye ngozi nyeupe aliyehisi kuwa Treyvon ni
kibaka kiliweka wazi kwamba bado yapo maoni potofu juu ya watu weusi. Suala
lililozusha mjadala mkubwa zaidi ni kwamba aliyempiga risasi kijana huyo
hakupewa hukumu yoyote mahakamani.
Sherehe za leo za mjini Washington
zitahudhuriwa pia na marais wa zamani wa Marekani. Bill Clinton na Jimmy Carter
ni miongoni mwa wale watakaotoa hotuba.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/ap
Mhariri: Josephat Charo
No comments:
Post a Comment