Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG),Fredrick Werema
Serikali imesalimu amri kwa Kampuni
ya kufua umeme ya Dowans na imeanza mchakato wa kuwezesha kuondolewa
mahakamani, kesi ya muda mrefu baina ya pande hizo mbili, gazeti hili limebaini.Habari
za uhakika zilizopatikana jana zinasema hatua hiyo ya Serikali inatokana na
ushauri ambao imekuwa ikipewa na wanasheria wake kwamba "uwezekano wa
kushinda kesi hiyo ni mdogo sana."
Mvutano uliopo unatokana na Serikali
kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC),
ambayo iliipa ushindi Dowans Holdings ya Costa Rica katika kesi namba
15945/VRO.
Jana, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati
na Madini, Eliakimu Maswi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
Felichesmi Mramba kwa nyakati tofauti walisema Serikali ilikwishatangaza
bungeni kwamba inakusudia kumaliza kesi zote ambazo zimekuwa zikizorotesha
mipango ya maendeleo.
"Sifahamu kwa upande wa kisheria
wamefikia wapi katika suala hilo (la Dowans),
lakini niseme kwamba waziri wetu (Profesa Sospeter Muhongo), alitangaza bungeni
kwamba lazima tuondokane na kesi ambazo zinatukwamisha, kwa hiyo kama wameanza majadiliano ni hatua nzuri," alisema
Maswi.
Maswi alisema baada ya Waziri Muhongo
kutoa kauli hiyo bungeni, utekelezaji wake unapaswa kufanywa na wanasheria wa
Serikali na kwamba mtu sahihi wa kuulizwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)
kwa sababu Tanesco ni shirika linalomilikiwa na umma kwa asilimia 100.
Kwa upande wake, Mramba alisema:
"Ninachofahamu ni kwamba kuna maandalizi ya kuwezesha mazungumzo hayo
kufanyika, kama ulisikiliza hotuba ya bajeti
ya mheshimiwa waziri (Muhongo), alisema mpango wa Serikali ni kuondokana na
kesi hizi."
Awali, kulikuwa na taarifa kwamba
Serikali imewalipa Dowans kiasi cha Dola za Marekani 78 milioni (Sh124.8
bilioni), lakini Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alikanusha taarifa hizo
akisema hakuna ukweli kuhusu jambo hilo.
Akizungumza kwa simu kutoka Sudan jana, Dk
Mgimwa alisema: "Kwa uelewa wangu hakuna malipo hayo, isipokuwa kwa
masuala mengine ya kisheria unaweza kuwasiliana na AG (Mwanasheria Mkuu wa
Serikali), nikirudi unaweza kupata taarifa zaidi."
Hata hivyo, AG, Jaji Frederick Werema
alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema Serikali
haihusiki kwa namna yoyote na kesi ya Dowans na kwamba wanaopaswa kufahamu kwa
undani suala hilo
ni wale walioshtakiwa, akimaanisha Tanesco.
"Hiyo siyo kesi ya Serikali na
haihusiki kwa namna yoyote ile, kaangalie parties (wahusika) zinazotajwa kwenye
hati ya kiapo, hapo Serikali haipo bwana, kwa hiyo waulize wahusika wanaweza
kuwa na information (taarifa) zaidi," alisema Jaji Werema.
Suala la kufanyika kwa usuluhishi nje
ya Mahakama pia nalo bado ni kitendawili kutokana na ukweli kwamba hata Kampuni
ya Uwakili ya Rex Arttoneys ambayo imekuwa ikisimamia kesi Dowans hapa nchini,
haifahamu kuwapo kwa mazungumzo hayo.
Mmoja wa Mawakili wa Kampuni hiyo, Dk
Thomas Nguluma alisema juzi kuwa hawafahamu chochote kuhusu mpango huo wa
Serikali na kwamba ikiwa umeanza kufanyika basi wao hawakuhusishwa.
"Sisi bado tuna mkataba na
Tanesco, lakini kwa hilo unalolisema kwa kweli
kama lipo hatujahusishwa, kama tukihusishwa
basi hatutakuwa na haja ya kuficha chochote,"alisema Dk Nguluma.
Kesi ya Dowans
Katika madai yao, Dowans walikuwa
wakitaka walipwe kiasi cha Dola za Marekani 149 milioni kutokana na uzalishaji
wa umeme na gharama za kukatishwa kwa mkataba wake, lakini ICC iliwapa tuzo ya
kulipwa Dola za Marekani 65 milioni.
Wakati Dowans wakiwa kwenye mchakato
wa kukazia hukumu hiyo katika Mahakama Kuu jijini London,
Uingereza, Tanesco kupitia kwa mawakili wa Kampuni ya Matrix ya nchini humo
waliwasilisha maombi ya kutaka kuahirishwa kwa ukaziaji huo, kutokana na
kufunguliwa kwa kesi ya kuupinga katika Mahakama Kuu ya Tanzania.
Tangu wakati huo, Tanesco hawajawahi
kushinda kesi yoyote kati ya tatu ambazo zimewahi kujitokeza katika shauri hilo, huku riba ya fedha
wanazotakiwa kulipa kwa Dowans ikiwa watashindwa kesi, ikiongezeka kila
kukicha.
Kutokana na kesi ambayo ilifunguliwa
katika Mahakama Kuu na baadaye Mahakama ya Rufani hapa nchini, hivi sasa riba
imesababisha fedha zinazopaswa kulipwa kwa Dowans kukaribia Dola 120 milioni
(zaidi ya Sh190 bilioni).
Serikali kupitia Tanesco pia
ililazimika kuweka dhamana ya Dola 31 milioni za Marekani (Sh50 bilioni) za
dhamana kutokana na kesi zilizofunguliwa hapa nchini kuchelewesha kukaziwa kwa
uamuzi wa ICC Uingereza.
Chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment