Katibu wa Taasisi na Jumuiya za
Kiislamu Tanzania,
Sheikh Ponda Issa Ponda alisafirishwa jana kwa helikopta kutoka Dar es Salaam
kwenda Morogoro na kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa kujibu
mashtaka yanayomkabili.
Ponda jana alianza kwa kufikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu asubuhi na kufutiwa mashtaka ya
uchochezi yaliyokuwa yakimkabili baada ya kusomewa mara ya kwanza Agosti 14,
mwaka huu akiwa kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili,
baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya
kuendelea kumshtaki.
Alidaiwa kutenda makosa hayo katika
maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano kati ya Juni 2 na Agosti 11 mwaka huu.
Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa
12 asubuhi na baadaye alipandishwa kizimbani na kufutiwa kesi hiyo, baada ya
Wakili Kweka kuwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya Kifungu cha 91 (1) cha
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Hata hivyo, baada ya kufutiwa
mashtaka hayo, aliendelea kushikiliwa na kisha akachukuliwa na kupelekwa
Morogoro ambako pia alisomewa mashtaka ya uchochezi.
Kuwasili Moro
Sheikh Ponda aliwasili kwa helikopta
ya polisi na kutua kwenye Uwanja wa Gofu, Morogoro akiwa chini ya ulinzi wa
polisi na alipakiwa kwenye gari maalumu ambalo liliongozana na magari mengine
matatu ya polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama
ukiwajumuisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), askari wa upelelezi,
Usalama wa Taifa pamoja na mbwa wa polisi na kusababisha shughuli za kazi
katika Mahakama hiyo na ofisi za jirani kusimama kwa muda.
Baada ya kufika mahakamani saa tano
asubuhi, magari yalisimama kwa takriban dakika 30 kabla ya kumtoa na kumwongoza
kwenye Mahakama ya wazi ambayo tayari ilikuwa umejaa watu.
Baada ya kumalizika kusomwa kwa kesi
hiyo, msafara uleule ulimrejesha Uwanja wa Gofu saa sita mchana na kupandishwa
kwenye helikopta kurejea Dar es Salaam.
Mahakamani Morogoro
Ponda alisafirishwa kwa helikopta ya
polisi hadi Morogoro na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi
akiwa chini ya ulinzi mkali.
Mara baada ya kumfikisha katika
Mahakama hiyo iliyofurika mamia ya waumini na wafuasi wake, Wakili wa Serikali,
Bernard Kongola alimsomea mashtaka matatu yanayomkabili.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa
wa Morogoro, Richard Kabate alisema: “Agosti 10, mwaka huu katika eneo la
Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro Ponda Issa Ponda, aliwaambia wafuasi
wake.
“Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji
wa Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na
Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watakuja kwenu na
watajitambulisha kwamba wao ni Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti, fungeni
milango na madirisha ya msikiti yenu na muwapige sana.”
Kongola alisema kauli hiyo ilikuwa
ikiumiza imani za watu wengine na kwamba hatua hiyo ni kinyume cha agizo la
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lililotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9,
mwaka huu ikimtaka kuhubiri amani ndani ya mwaka mmoja na kwenda kinyume na
kifungu cha Sheria namba 124 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Ponda alikana.
Katika shtaka la pili, Ponda anadaiwa
Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro
aliwaambia Waislamu kuwa Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia vurugu
iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu
asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.
Alisema Serikali haikufanya hivyo kwa
wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji
baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo na
kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine jambo ambalo ni kinyume cha
Kifungu cha Sheria 129 cha mwaka 2002, shtaka ambalo pia alikana.
Shtaka la tatu linafanana na lile la
pili lakini na upande wa mashtaka ulieleza kuwa maneno hayo yaliumiza imani za
watu wengine na kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha Kifungu 390 cha Sheria na
Kanuni ya Adhabu namba 35 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Sheikh Ponda alilikana.
Baada ya kusomwa kwa mashtaka yote matatu, wakili wa Serikali aliiambia
Mahakama kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na kupanga kesi kuanza kusikilizwa
Septemba 2 mwaka huu. Upande wa utetezi uliomba Mahakama kupanga kuanza
kusikilizwa kwa kesi Agosti 26, mwaka huu.
Hakimu Kabate aliwapa mawakili
kujadiliana na baadaye kuomba kesi hiyo ianze kusikilizwa Agosti 28 mwaka huu.
Wakili alalamika
Akizungumza Dar es Salaam jana, Wakili wa Ponda, Juma
Nassoro alilaani kitendo cha kuondolewa kwa mteja wake gerezani na kwenda kusomewa
mashtaka mapya Morogoro bila taarifa.
Alidai kuwa polisi wanaendelea
kukiuka taratibu za kumshikilia kiongozi huyo kutokana na kufanya mambo kinyume
na sheria kwa lengo la kutaka waumini kufanya vurugu ili waendelee kumshikilia
kiongozi huyo.
“Kitendo cha kumuondoa mteja wangu
gerezani na kwenda kumsomea shtaka jingine Morogoro nimelilaani. Sijalipenda.
Polisi hawakuwa na nia nzuri na Ponda kwa sababu sheria zinajulikana na kila
mtu ana haki ya kutetewa,” alisema Nassoro.
Akizungumzia kufutiwa kesi Mahakama
ya Kisutu, Nassoro alisema Serikali imeamua kufuta kesi kabla ya kusikilizwa
baada ya kuona imeelemewa kwani alishapeleka maombi ya kuirudisha Mahakama Kuu
kutoka Kisutu kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi
hiyo na maombi hayo yalipewa namba 11/2013.
Msemaji wa familia, Isihaka Rashidi
alisema: “Hawa jamaa wamempeleka Morogoro kwa siri kwa sababu jana (juzi)
tulikwenda Segerea hakukuwa na hizo taarifa. Tumekuja kushtuka asubuhi baada ya
mke wake kwenda kumpelekea chai na kuambiwa ameondolewa na kupelekwa Morogoro.”
Alisema baada ya kupata taarifa hizo
iliwalazimu kuwasiliana na ndugu zao waliopo Morogoro kwa ajili ya kwenda
mahakamani kusikiliza kesi hiyo.
*Imeandikwa na Lilian Lucas na Hamida
Sharrif (Morogoro), James Magai, Aziza Masoud na Aidan Mhando, Dar.
SOURCE: www.mwananchi.com
No comments:
Post a Comment