Dar es Salaam. Jaji mstaafu wa
Mahakama ya Rufaa, Thomas Mihayo amesema kushamiri kwa matukio ya uuzwaji,
ununuaji wa dawa za kulevya, sambamba na upitishaji wa dawa hizo katika viwanja
mbalimbali vya ndege nchini, kunachangiwa na rushwa iliyokithiri katika Mahakama
na Polisi.
Amesema matukio mengi ya mauaji ya
raia wasio na hatia pamoja na upitishwaji wa wanyamapori (Twiga) katika viwanja
vya ndege mbalimbali nchini hayachukuliwi hatua stahiki kwasababu rushwa
imetawala, “Kuzungumzia rushwa siyo hoja, tatizo ni kuwa matendo yetu ni
tofauti na kauli tunazotoa.” Katika maelezo yake alisema anamuonea huruma
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kwani licha ya kuonyesha wazi kutaka
kupambana na watu wanaoingiza dawa za kulevya kupitia katika viwanja vya ndege,
hataweza kwa maelezo kuwa rushwa ndiyo inafanikisha mipango yote ya uingizwaji
wa dawa hizo.
Jaji Mihayo ambaye ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) aliyasema hayo jana katika
mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili, huku akitoa mifano ya kesi mbalimbali
ambazo watuhumiwa waliachiwa huru katika mazingira yanayoonekana wazi kuwa
Mahakimu walipewa rushwa.
“Twiga kusafirishwa kupitia viwanja
vya ndege maana yake ni rushwa ilitembea na siyo uzembe. Sasa tunaona mauaji ya
watu wasio na hatia lakini vyombo vya dola vinafumba macho na hakuna
kinachofanyika.Katika nchi inayofuata sheria mambo kama haya lazima yafanyiwe
kazi, lakini ukiona kimya maana yake rushwa imetawala” alisema na kuongeza;
“Rushwa imetoka huko sasa imeingia
katika dawa za kulevya, Watanzania wengi wanadhani dawa za kulevya kupita
katika uwanja wa ndege ni uzembe wa wasimamizi, hilo siyo kweli yamepita kwa
sababu ya rushwa.”
“Hawa watu polisi wanawajua lakini
wanawalinda…, ndiyo wanalindwa na haohao polisi” alisisitiza.
Akitolea mfano tukio la Julai 5 mwaka
huu la upitishaji wa mabegi tisa ya dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) lililoanikwa na hadharani na Dk
Mwakyembe, ambapo watu mbalimbali walitajwa kuhusika, wakiwemo maofisa wa Idara
ya Usalama wa Taifa ambao walidaiwa kuchelewesha mbwa kwa ajili ya kukagua
mizigo alisema, “Mbwa hawawezi kupokea rushwa na kama wangekuwepo katika uwanja
wa ndege. Ni wazi kuwa wangeweza kubaini dawa hizo za kulevya.”
Alifafanua, “Dk Mwakyembe alieleza
wazi kuwa mbwa walichelewa kufika uwanja wa ndege, swali la kujiuliza kwa nini
walichelewa? Sababu za kuwachelewesha zinaweza kuwa nyingi tu, unaweza kusema
gari liliharibika.”
Alisema haoni uwezekano wa Dk
Mwakyembe kufanikiwa katika mapambano hayo, kwani hata kama viwanja vya ndege
vitafungwa mashine za kubaini waliobeba dawa hizo, kama wasimamiaji watapokea
rushwa hakuna atakayekamatwa.
“Kama kutakuwa na sheria kali za
kudhibiti dawa za kulevya basi watekelezaji wa sheria hizo wanatakiwa kuwa
waaminifu na kuichukia rushwa. Pia tunaweza kuwa na sheria kali lakini ndiyo
rushwa ikaongezeka zaidi” alisema Jaji Mihayo
“Watanzania watafanikiwa kuikomesha
rushwa kama wakiichukia. Nasema hivi kwa sababu siku hizi mtu aliyekithiri kwa
kupokea rushwa anashabikiwa na wenzake. Mahakama zetu nazo zinatakiwa
zitekeleze wajibu wake ipasavyo” alisema
Rushwa katika Mahakama
Huku akitoa mifano halisi, Jaji
Mihayo alisema kuwa hivi karibuni alisomewa hukumu moja ya kesi ya dawa za
kulevya na Dk Mwakyembe, hukumu aliyodai kuwa inaonekana wazi hakimu alipewa
rushwa.
Bila kutaja Mahakama wala hakimu
aliyetoa huku hiyo alisema, “ Kuna mtu mmoja alikamatwa na dawa za kulevya
akiwa amezimeza baadaye alifikishwa mahakamani huku dawa zile alizokutwa nazo
zikitumika kama ushahidi,”
“Cha ajabu wakati wa hukumu ya kesi
hiyo hakimu alimuachia huru mtuhumiwa kwa maelezo kuwa hakukuwa na ushahidi wa
kutosha kwamba dawa zile za kulevya zilikuwa zimemezwa na mtuhumiwa huyo. Mimi
ni Jaji nilisikiliza uchakachuaji wa kesi hiyo nilijua tu kuna rushwa
ilitembea.”
Alisema kesi nyingine ambayo uamuzi
wake ulikuwa ya utata, alielezwa na ofisa mmoja wa Taasisi ya Kudhibiti na
Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Yule ofisa wa Takukuru alinieleza
kuwa kuna jamaa mmoja aliombwa rushwa na Sh1milioni. Kutokana na hali hiyo mtu
huyo alikwenda kuripoti Takukuru ambao waliandaa mpango wa kumkamata mwomba
rushwa kwa kumweka mtego wa Sh500,000” alisema na kuongeza;
“Yule mtu aliyeomba rushwa alikamatwa
na kufikishwa mahakamani, ila cha kushangaza hakimu alimwachia huru mtuhumiwa,
kwa maelezo kuwa aliomba Sh1 milioni lakini alipewa Sh500,000. Hiki ni
kichekesho kweli yaani kwasababu fedha aliyoomba siyo aliyopewa basi akaachiwa
huru.”
No comments:
Post a Comment