Dar es Salaam. Kamati ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAAC), imebaini mtandao wa ufisadi unaoshirikisha wakurugenzi 70 wa
halmashauri mbalimbali hapa nchini ambao wanashirikiana na baadhi ya watendaji
wa Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha
Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja
na Wilaya ya Monduli, Arusha, Mwanza, Mbeya na Ilala.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rajab Mohamed Mbarouk
alisema keshokutwa atataja majina ya wakurugenzi hao ili wananchi waweze
kuwafahamu.
Mbarouk alisema kuwa Tanzania Bara
ina halmashauri 134, kwa hiyo ina maana zaidi ya nusu ya wakurugenzi
wanajihusisha na mambo hayo.
“Baadhi ya wakurugenzi hao
walihamishwa kwenye vituo vyao vya kazi kutokana na kashfa ya matumizi mabaya
ya fedha za Serikali, lakini bado wanajihusisha na mambo haya,” alisema
Mbarouk.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati
hiyo imepanga kukutana kesho na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Tamisemi,
Hawa Ghasia ili kuzungumzia suala hilo.
“Kuna zaidi ya wakurugenzi 70 wako
kwenye mtandao wa ufisadi kwa kushirikiana na watendaji wa Hazina na Tamisemi,
jambo ambalo limesababisha halmashauri zao kupata hati chafu kwa miaka mitano
mfululizo,”alisema Mbarouk.
Aliongeza wakurugenzi hao wamekuwa
wakishirikiana na wahasibu wao katika kutumia vibaya fedha za Serikali
zinazotolewa kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika
halmashauri zao.
Akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Jiji
la Mwanza, Wilson Kabwe ambapo halmashauri yake imefanya vibaya katika ripoti
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hajachukuliwa
hatua na badala yake amekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Alisema mbali na halmashauri hiyo,
aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Rhoda Nsemwa
ambaye alisimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ufisadi, lakini bado anaendelea
kupata mshahara na stahiki zake kama mtumishi
aliye kazini.
“Tumeshangaa kuona kuwa, aliyekuwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo bado anaendelea kulipwa
mshahara, kodi ya nyumba na marupurupu mengine kama
ofisa aliye kazini wakati ana kesi ya matumizi mabaya ya fedha za Serikali,”
alisema.
Alibainisha kamati hiyo pia imebaini
kuwa Takukuru inajihusisha moja kwa moja na vitendo vya rushwa, kutokana na
kupotosha ukweli wa taarifa za watuhumiwa na kuchelewesha kuwasilisha jalada
mahakamani.
“Ukiangalia kesi zilizoko mahakamani
ambazo upelelezi wake bado unaendelea utaona wazi kuwa Takukuru ni miongoni mwa
watu wanaopokea rushwa, jambo ambalo limesababisha kuchelewesha upelelezi au
kupindisha ukweli,” aliwatuhumu.
Akizungumzia tuhuma hizo, Waziri wa
Fedha, Dk William Mgimwa alisema, “Hazina kuna taratibu na sheria kuhusu
matumizi ya fedha na kama jambo hilo
limefanyika kweli ni wazi kuwa litakuwa kinyume na sheria na taratibu
zilizopo.”
Alisema licha ya kuwa mpaka sasa
hajasikia malalamiko yoyote, aliahidi kufuatilia jambo hilo
ili kubaini ukweli na kwamba kama kuna mtu
atabainika atachukuliwa hatua stahiki. Alisema, “Ngoja tufuatilie ili kujua
ukweli.”
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa aliomba atafutwe leo kwa maelezo kuwa
atakuwa ameshapata maelezo ya kutosha kuhusu tuhuma hizo.
“Sijajua hizo halmashauri ni zipi,
pamoja na idara ambazo zipo chini ya wizara hii, ngoja kwanza nizungumze na
wahusika ambao pia najua watanieleza kilinachoendelea, nitafute kesho (leo)
nitatoa ufafanuzi wa kina,” alisema Majaliwa.
Kamati yawabana Mambo ya Nje
Katika hatua nyingine; Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), imemwagiza CAG kufanya ukaguzi
maalumu wa matumizi ya fedha katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa hasa katika uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Gaudence Kayombo alisema jana alipokutana na viongozi wa wizara hiyo kuwa kuna
matumizi makubwa ya fedha katika uendeshaji wa mikutano ya kimataifa.
“Kamati itamwandikia CAG, afanye
ukaguzi maalumu ili kubaini utata unaoonekana katika matumizi ya fedha ya
wizara hiyo hasa kwenye eneo la mikutano,” alisema Kayombo.
Kayombo alisema kutokana na utata
huo, kamati imeona haiwezi kuijadili ripoti hiyo ya fedha ya mwaka 2012/13 hadi
CAG atakapofanya ukaguzi maalumu.
Aidha, Kayombo aliwataka viongozi hao
wataje gharama za Ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliojengwa kwa mkopo na msaada wa
Serikali ya China,
lakini Katibu Mkuu wa wizara hiyo, John Haule alisema ataitaja baadaye baada
kujiridhisha.
“Tunataka kufahamu gharama za ujenzi
wa jengo hilo,
vifaa vilivyosamehewa kodi ili kamati iweze kujua, kwa sababu hadi sasa
haieleweki umegharimu kiasi gani,” alisema Kayombo.
Hata hivyo, alisema asilimia 46 ya
gharama za ujenzi wa jengo hilo ni msaada wa
Serikali ya China
huku asilimia 54 ikiwa ni mkopo.
Source: www.mwananchi.com
No comments:
Post a Comment