Dodoma. Halmashauri Kuu ya Chama Cha
Mapinduzi (Nec), jana iliridhia kumvua uanachama, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe
Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mansour Yussuf Himid kutokana na kukiuka miiko
ya chama hicho.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nauye aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa Mansour ambaye
hivi karibuni alikuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),
amefukuzwa uanachama kutokana na kukiuka mambo matatu.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni
kushindwa kutimiza malengo ya CCM na kutekeleza malengo ya uanachama, kushindwa
kutekeleza wajibu wa uanachama na kukiuka maadili ya uongozi, kuikana na
kuisaliti Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015.
Kutokana na uamuzi huo, Nape alisema
Mansour hatakuwa na nafasi ya kukata rufani mahali popote kwa kuwa uamuzi
uliofikiwa jana ni wa kikao cha juu cha mwisho.
Akizungumza na Mwananchi jana,
Mansour alisema kwa sasa hawezi kuzungumza mengi kwani anahitaji muda wa
kutafakari kutokana na uzito wa suala lenyewe.
“Ndugu yangu nashukuru sana kwa
kunipigia simu. Ila ninahitaji muda wa kutulia kwanza. Nipe kama siku mbili au
tatu hivi halafu nitaongea,” alisema Mansour, ambaye amekuwa Mwakilishi wa
Kiembe Samaki tangu mwaka 2005.
Nec ilifikia uamuzi huo ikibariki
mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Kuu ya CCM upande wa Zanzibar iliyomvua
uanachama kutokana na misimamo yake ya kisiasa na hasa suala la Muungano.
Mansour aliwahi kushika nyadhifa
kadhaa ndani ya CCM ikiwamo ya ujumbe wa Halmashauri Kuu na Mweka Hazina wa
chama hicho upande wa Zanzibar.
Kilichomponza
Kwa mara ya kwanza, tuhuma za Mansour
zilifikishwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi
Agosti 16, mwaka huu katika Ofisi za CCM Kisiwandui ambacho wajumbe wa kamati
hiyo kwa kauli moja walitoka na azimio la kumfuta uanachama.
Suala hilo lilifikishwa Kamati Kuu ya
CCM, Zanzibar Agosti 22, mwaka huu kupitia uamuzi huo na iliafiki. Kitendo cha
Mansour kuingia kwenye Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar inayoongozwa na
mwanasiasa mkongwe Hassan Nassor Moyo ambayo imekuwa ikipigania Muungano wa
mkataba ilichochea tofauti yake na makada wenzake wa CCM Zanzibar.
Kitendo cha kuungana na Mzee Moyo na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad kupigia debe suala la
Muungano wa Mkataba kati ya Tanganyika na Zanzibar kuliwakera makada wa CCM
waliomchukulia kuwa anapingana na Katiba na Ilani ya CCM vilivyosimamia katika
Serikali mbili.
Nyadhifa SMZ
Mansour, ambaye amekuwa Naibu Waziri
wa Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira kuanzia mwaka 2000-2005. Alipanda cheo na
kuwa waziri kamili katika wizara hiyo kuanzia mwaka 2005 hadi 2010
alipohamishwa kuwa Waziri wa Kilimo kati ya 2010 na 2012 na Aprili, mwaka jana
aliteuliwa kuwa waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu na Mjumbe wa Baraza la
Mapinduzi la Zanzibar.
Hata hivyo, hakudumu muda mrefu
katika wadhifa huo kwani alivuliwa wadhifa huo kutokana na kile kilichokuwa
kimeelezwa tangu awali kwamba ni kutofautiana na chama hicho. Nyota yake
iling’ara zaidi alipokuwa Wizara ya Nishati akiwa naibu na baadaye waziri
kamili kwani alikuwa mmoja wa wanasiasa wa Zanzibar waliopinga waziwazi suala
la mafuta kuingia kwenye masuala ya Muungano na hasa kwenye mijadala ya Baraza
la
Wawakilishi.
Bukoba ngoma nzito
Kwa upande wa sakata la mgogoro wa
Bukoba, Nape alisema Kamati Kuu itaendelea kuwahoji wahusika hao leo baada ya
kushindwa kukamilisha kazi hiyo jana.
Suala hilo linawapambanisha vigogo wa
siasa wa Mkoa wa Kagera wakiongozwa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki
na Meya, Dk Anatory Amani.
“Suala la Bukoba tutaendelea nalo
kesho (leo) saa tano asubuhi baada ya kutokukamilisha kazi yake leo (jana),
hivyo Kamati Kuu inatarajia kuendelea kushughulikia mgogoro huo kabla ya
kuondoka mjini Dodoma,” alisema Nape.
Mbali na kutoa maoni yao kuhusu
Rasimu ya Katiba, Halmashauri Kuu pia ilipitisha majina ya makatibu watatu wa
CCM ngazi ya mikoa.
Waliopitishwa ni Mary Maziku, Romuli
Njovu na Kassimu Mabrouk ambao watapangiwa mikoa. Pia ilipitisha uteuzi wa
makatibu 25 wa wilaya wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment