Rais Barack Obama, Mkewe Michelle
Obama, marais wa zamani Jimmy Carter na Bill Clinton Agosti 28, 2013
Akizungumza na maelfu ya watu
waliohudhuria maadhimisho ya miaka 50 tangu maandamano ya kutetea haki za
kiraia kufanyika jijini Washington, rais Barack Obama jana Jumatano alisema
'kazi haijamalizika' ya kutetea haki na usawa kwa wamarekani wote.
Miaka 50 baada ya Mchungaji Martin
Luther king Jr. kutoa hotuba ya kihistoria na ya kusisimua akisema; "I
have a dream" wakati wa ubaguzi mkubwa wa rangi Marekani, rais wa kwanza mweusi
Marekani alisimama katika ngazi zile, zile alizosimama kwenye mnara wa
kumbukumbuku wa Lincoln Memorial.
Bw. Obama alielezea wasifu wa Dr.King
pamoja na kujitolea kafara kwa walioshiriki maandamano makubwa ya Washington
miaka 50 iliyopita. Alisema kutokana na maandamano yao, sheria ya haki za
kiraia ilipita. Na kwa sababu waliandamana sheria ya haki za kupiga kura
ilitiwa saini na kwa sababu hiyo hiyo wasichana na wavulana weusi wanaweza
kuishi maisha yao kikamilifu bila kuwa watumwa wa mtu mwingine.
Rais Obama aliendelea kusema na kwa
sababu waliandamana, hata White House imebadilika huku maelfu ya watu
wakimshangilia. Bw. Obama alisema maandamano hayo yalileta haki sio tu kwa
wamarekani weusi lakini kwa watu wa rangi nyingine Marekani na duniani waliokuwa
na kiu cha kuwa huru.
Alisema mengi yamebadilika tangu
maandamano hayo ya mwaka wa 1963 lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanywa.
Alisema kuna mwanya mkubwa kati ya matajiri na maskini miongoni mwa watu wa
rangi mbalimbali Marekani na migawanyiko mikubwa ya kisiasa hapa Washington
inayofanya ndoto ya Martin Luther King Jr. kuonekana kuwa mbali sana kutimia.
Rais Obama alisema Marekani ina
chaguo, ama kuendelea na msukumo huu mkubwa wa kidemokrasia, au kuzembea na
kukifanya kizazi kijacho kuishi bila matumaini au kujikakamua na kufanya
mabadiliko ya kuleta usawa na haki kwa wote.
Orodha ya waliotoa hotuba katika
maadhimisho hayo ilikuwa ndefu, na ilijumwisha mwana wa kike wa Dr. King,
mchungaji Bernice King, marais wa zamani Bill Clinton, Jimmy Carter, wacheza
sinema maarufu na hata watangazaji mashuhuri wa televisheni. Mbunge John Lewis
mmoja wa viongozi wa maandamano ya kutetea haki za kiraia mwaka wa 1963 alisema
ingawa kuna maendeleo, ubaguzi wa rangi ungali umejikita katika jamii ya wamarekani.
No comments:
Post a Comment