Kwa mara ya kwanza katika historia ya
Liberia, wanafunzi wote wamefeli mtihani wao wa mwisho wa sekondari na hivyo
kumaanisha kuwa hakuna hata mmoja ambaye atafuzu kuingia chuo kikuu.
Waziri wa elimu wa Liberia amesema
ameshinda kufahamu ni kwa nini hakuna wanafunzi hao wamefeli kiasi hicho.
Zaidi ya wanafunzi elfu ishirini na
watano walianguka mtihani huo ambao ungewapa fursa ya kujiunga na chuo kikuu
cha Liberia ambacho ni moja ya vyuo vikuu vinavyoendesha na serikali.
Lakini wasimamizi wa chuo hicho
wameiambia BBC kuwa wanafunzi hao hawakuwa makini na ufahamu mzuri wa lugha ya
Kiingereza ambayo ilitumiwa kuwatahini.
Taifa la Liberia linaendelea
kujinasua kutokana na athari za mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyomalizika
zaidi ya miaka kumi iliyopita.
Rais wa Liberia, Ellen Johnson
Sirleaf, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, amekiri kuwa mfumo wa
elimu nchini humo bado ungali duni na unahitaji marekebisho ya dharura.
Mwandishi wa BBC mjini Monrovia,
anasema shule nyingi nchini humo havina vifaa vya kimsingi na waalimu
waliohitimu.
Lakini hii ni mara ya kwanza katika
historia ya taifa hilo kwa wanafunzi wote kufeli mtihani huo licha ya kulipa
ada ya usajili ya dola ishirini na tano.
Chuo hicho kikuu ambacho kina idadi
kubwa ya wanafunzi hakitakuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wakati muhula
mpya utakapoanza mwezi ujao.
Lakini wanafunzi wengi wanasema
hawajaamini matokeo ya mtihani huo na waziri wa Elimu Etmonia David-Tarpeh,
ameiambia BBC kuwa anatarajia kukutana na wasimamizi wa chuo hicho ili kujadili
suala hilo.
Chanzo: Mjengwablog.com
No comments:
Post a Comment