Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu Tanzania,
Sheikh Ponda Issa Ponda amesema alichanganyikiwa kiasi cha kushindwa kujielewa
kwa muda baada ya kupigwa risasi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu
na Mwananchi kwenye wodi binafsi ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi)
alikolazwa jana, Sheikh Ponda alisema kutokana na hali hiyo hakumbuki matukio
yaliyofuata baada ya hapo.
“Sikumbuki hata nilipata huduma ya
kwanza hospitali gani kwa sababu sikuwa katika hali ya kawaida. Mambo mengine
yaliyotendeka kabla ya kujeruhiwa ninayakumbuka vizuri,” alisema Ponda ambaye
inasadikiwa kwamba alipigwa risasi ya begani, Ijumaa iliyopita mjini Morogoro.
Alisema alihutubia katika Kongamano
la Waislamu kwa muda mfupi akizingatia muda uliokuwa umetolewa kumaliza mkutano
huo na baada ya hapo alishuka na kupanda kwenye gari binafsi ambalo
lilizingirwa na polisi ndipo akaamua kushuka na kuanza kutembea kabla ya
kujeruhiwa.
Mahojiano maalumu na Sheikh Ponda
Swali: Je, watu waliokupa huduma ya
kwanza mara baada ya kujeruhiwa walikuta risasi iliyokujeruhi?
Jibu: Nilipigwa risasi kwa nyuma ikatokea
mbele kwa hiyo haikubaki mwilini wala haikuonekana ilipoangukia kwa wakati huo
maana kulikuwa na purukushani.
Swali: Ulipata wapi huduma ya kwanza?
Jibu: Kwa kweli kwa sasa siwezi
kukumbuka nilihudumiwa wapi kwa sababu mara baada ya kujeruhiwa sikuwa katika
hali yangu ya kawaida, nilichanganyikiwa.
Swali: Utathibitisha vipi kama ulipigwa risasi?
Jibu: Bahati nzuri ni kwamba tukio
hili lilitokea kweupe wapo wengi walioshuhudia, kwa hiyo wanaweza kusaidia
kuthibitisha na ushahidi mwingine ni jeraha hili.
Swali: Nini msimamo wako baada ya
tukio?
Jibu: Nitaendelea kuzungumzia haki za
Waislamu na siwezi kurudi nyuma. Pamoja na kwamba wananiona mimi ni mtu
mchochezi lakini wanaeneza chuki dhidi yangu kwa njia wanazojua wao.
Nitaendelea, risasi haitaninyamazisha.
Swali: Umehusishwa kufanya uchochezi Zanzibar, unalizungumzia vipi hilo?
Jibu: Zanzibar nilichozungumza ni kuhusu kesi dhidi
ya viongozi wa Kundi la Uamsho. Watu wamewekwa ndani kwa miezi tisa sasa, kwa
mujibu wa sheria za nchi yetu, kesi wanayoshtakiwa ina dhamana, sasa nikauliza
kwa hao viongozi, kwa nini hawazingatii sheria? Kesi zina muda mrefu hazitolewi
uamuzi, nikawasisitiza wazingatie misingi ya sheria kwa kuwa hivyo
wanavyowatendea wananchi wajue kwamba hawastahili kupewa tena ridhaa ya
kuongoza nchi, nilifikisha ujumbe wangu.
Swali: Kuna tukio la kumwagiwa
tindikali mabinti wawili wa Uingereza lililotokea Zanzibar, ambalo wewe pia unahusishwa, hili
unalizungumziaje?
Jibu: Sijaona huo ushahidi ambao
wanahangaika kunihusisha na tukio hilo,
nahusishwa vipi? Matukio ya kumwagiwa tindikali yamekuwa yakijitokeza mara kwa
mara huko kabla sijakwenda kuhutubia. Vyombo vya dola vifanye kazi yake vyema
ili kubaini ukweli wa jambo hili.
Pia Mwananchi ilizungumza na mke
wake, Sheikh Ponda, Hadija Ahmad ambaye alikuwa ameketi pembeni ya kitanda
alicholazwa mumewe.
Swali: Unazungumziaje tukio hili la
kujeruhiwa kwa mumeo?
Jibu: Hili ni dhumuni la Serikali,
lililenga moja kwa moja kumdhuru ili kunyamazisha harakati zake za kutetea
wanyonge. Ni tukio la kupangwa, halijatokea bahati mbaya. Serikali inamfuatilia
sana hivyo
ililenga kumnyamazisha.
Namshauri Rais (Jakaya Kikwete),
kuhakikisha kwamba haki za wanyonge zinawafikia, asije akafikiri hili
lililotokea kwa Sheikh Ponda ni suluhisho, ni vyema kufanya mazungumzo ili
kuweka mabadiliko.
Alivyowaponyoka polisi
Mtu wa karibu wa Sheikh Ponda
alisimulia jinsi walivyomsafisha kiongozi huyo kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam na kukwepa
vizuizi vya polisi ambao walikuwa wakiendelea kumsaka.
“Msafara ulikuwa na magari mawili.
Moja lilitumika kwa uangalizi, lingine lilimbeba Sheikh Ponda. Tulipofika
Chalinze tulikuta kizuizi tukakikwepa kwa kupitia Msata kisha Bagamoyo hadi Dar es Salaam na
kumfikisha Muhimbili,” alisema.
Waigomea polisi
Msemaji wa familia ya Sheikh huyo,
Isihaka Rashid alisema hawaitambui tume iliyoundwa na polisi kwa kuwa jeshi hilo ndilo
linalotuhumiwa.
“Tunachofanya hivi sasa ni kukusanya
ushahidi wetu, kwa bahati nzuri tayari tumepata mkanda wa tukio lenyewe ambao
utatuwezesha kumbaini aliyemshambulia Sheikh Ponda.
“Hatuwezi kuhitaji majibu ya hiyo
tume yao na hata leo kuna maofisa wa polisi
kutoka Makao Makuu na Kituo cha Kati, Dar
es Salaam walifika wakitaka kumhoji eti kuhusu
uchochezi lakini alikataa kuzungumza hadi mwanasheria wake awepo, wakaondoka,”
alisema Rashid.
Source: www.mwananchi.com
No comments:
Post a Comment