William Lukuvi
Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amesema baadhi ya majina
ya wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya
dawa za kulevya lakini Serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa haraka.
Majibu hayo ya Waziri Lukuvi yamekuja
baada ya wabunge kumbana na wengine wakizomea baada ya kueleza ugumu wa kutaja
majina ya washukiwa pasi na ushahidi wa kutosha.
“Serikali haiwezi kutaja majina
haraka kiasi hicho kwani inaogopa kukurupuka na kushindwa mahakamani, hivyo
lazima tuwe makini sana na jambo hilo. Hatuwezi kukurupuka tu eti ni fulani
wakati hatuna vithibitisho.
“Kumbukeni wengine mpo humu ndani ya
Bunge na tukianza wengi mtakwisha maana katika orodha hiyo kubwa na ninyi mmo
na orodha ni kubwa kweli ambayo wakati mwingine inatakiwa umakini wa hali ya
juu,” alisema Lukuvi alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Karatu
(Chadema), Mchungaji Israel Natse.
Katika swali lake ambalo
lilisababisha kelele za kuzomea, Natse alitaka majina hayo yatajwe hadharani.
Hata hivyo, hali ilitulia baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuingilia kati
na kusema: “Hii tabia ya zomeazomea siitaki humu ndani, acheni tabia hiyo
lazima mumsikilize mtu kwa kile anachokisema kwanza lakini mtindo huu si mzuri...”
Patashika hiyo ilitokana na swali la
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige aliyetaka kujua iwapo Serikali
inaweza kuwaambia Watanzania ukubwa wa biashara hiyo nchini na kama haioni kama
kuna tatizo katika ukaguzi wa abiria na mizigo katika viwanja vya ndege na
juhudi za Serikali kumaliza tatizo hilo.
Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema
ukubwa wa biashara hiyo hapa nchini unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274
waliokamatwa kati ya mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu kwa kosa la kujihusisha na
dawa za kulevya katika nchi mbalimbali za nje.
Alisema Serikali inafahamu ukubwa wa
tatizo la matumizi ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini na alitaja
takwimu za ukamataji wa dawa hizo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi
Machi, 2012.
Alisema pamoja na kukamatwa kwa
Watanzania hao nje ya nchi, wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika Magereza ya
Keko na Ukonga, Dar es Salaam ambao ni raia wa Iran, Pakistan, Senegal na
Afrika Kusini.
Hata hivyo, katika swali lake la
nyongeza, Magige alisema uteketezaji wa dawa zinazotajwa kukamatwa umekuwa wa
siri kiasi cha kutiliwa shaka kuwa huenda zinachukuliwa na maofisa
waliozikamata ndiyo maana hakuna uwazi.
Kuhusu hilo, Waziri Lukuvi alisema
suala la uteketezaji wa dawa hizo hauko wazi kutokana na sheria zilizopo
kutotoa nafasi ya kuteketezwa mapema kwa kuwa zinatumika kwa ajili ya ushahidi
akisema wakati mwingine hukaa zaidi ya miaka 10.
CHANZO: Mwananchi
No comments:
Post a Comment