SEHEMU (I)
Arusha. Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani la Taifa (Necta), Dk Joyce Ndalichako amesema siasa hazipaswi kupewa
nafasi katika mchakato wa usimamizi wa mitihani na kwamba athari za mwenendo wa
aina hiyo ni kubwa kwa taifa.
Dk Ndalichako alisema akiwa kiongozi
wa Necta hapendi ifike mahali ambako kila mtu atatakiwa afaulu hata kama hana
sifa kwani madhara yake yatakuja kuonekana kwenye rasilimali watu siku zijazo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu
Arusha hivi karibuni alisema: “Tukiruhusu mitihani iingiliwe na
wanasiasa tutakuwa tunajimaliza wenyewe, kama ni wanasiasa wafanye kazi ya
kushauri halafu waache wanataaluma husika wafanye kazi yao.
“Wanaohusika na kutunga sheria
watekeleze jukumu lao siyo kuingilia moja kwa moja suala la mitihani.
Sisemi kuwa tuachwe tu tufanye kazi kama tunavyotaka, ikibidi kuwe na chombo
cha wanataaluma kutukagua, kwa sababu hii ni taaluma siyo kitu cha kila
mtu kuingilia.
“Madhara ya kuingilia mitihani
matokeo yake yataweza kuja kuonekana baada ya miaka hata 10 ijayo, ili kukwepa
hali hiyo, kila mtu afanye kazi yake kama itaonekana watendaji hawana sifa
waondolewe wawekwe wengine wenye sifa.”
Dk Ndalichako ambaye hivi karibuni
alichaguliwa kuongoza Mabaraza ya Mitihani Afrika (AEAA) alisema: “Mtu akipewa
alama asizostahili na akawa mwalimu atawafundisha nini watoto? Hawa ndiyo
utakuta wana sababu zisizokwisha, kila siku utamsikia akisema watoto wa siku
hizi hawaelewi kabisa.”
Dk Ndalichako pia alipinga mawazo
kwamba Necta inapaswa kushirikiana na wadau wa elimu katika kila kitu. Alisema
ni hatari... “Tusifike mahali tuambiwe tuwaulize watoto tuwaletee maswali gani
kwenye mtihani.”
Kauli ya Dk Ndalichako imekuja wakati
taifa likiendelea kuugulia maumivu yaliyotokana na matokeo mabaya ya mitihani
ya kidato cha nne ya 2012 ambayo karibu nusu ya wanafunzi walifeli. Matokeo
hayo yaliifanya Serikali kuunda tume iliyoogozwa na Katibu Mkuu wa sasa wa
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome ambayo ilipendekeza
matokeo hayo yafutwe na yapangwe upya, hatua ambayo wengi waliita ni ya
kisiasa.
Mahojiano kati ya Dk Ndalichako
Swali: Hii ni mara ya tano kwa Necta
kuwa mwenyeji wa mkutano wa AEAA, na pia mmekuwa mkihudhuria mikutano kama hii
inapofanyika nje ya nchi, ni nini hasa mmeona kuwa ni changamoto kwa mitihani
inayotungwa katika ngazi ya shule?
Jibu: Hii mitihani inayotungwa
shuleni ni changamoto sana, lakini ukiangalia utagundua kuwa tatizo lipo kwenye
mitalaa ambayo walimu wanafundishiwa. Huko suala la ufundishaji limetiliwa
mkazo sana lakini lile la kuwapima watoto halijapewa kipaumbele kabisa.
Wanachofundishwa huko ni kama
orientation (utangulizi) tu, walimu wanatakiwa wajue mbinu gani zitumike
kutunga mitihani.
Sisi kwenye ngazi ya taifa
tunapotunga maswali tunazingatia mengi, kuanzia idadi ya watahiniwa na mambo
kama hayo. Mwalimu darasani angetakiwa kutunga mtihani kwa kuangalia watoto
wake na ajue ni mbinu gani za kutumia.
Tumekuwa tukifanya mafunzo kwa baadhi
ya walimu kuhusu namna bora ya kutunga mitihani, ili waweze kufanya tathmini ya
kile walichowafundisha watoto. Hata hivyo kwa kuwa sisi tupo wachache na
mitihani yetu ni mingi tunashindwa kuwafikia wote. Tuna mpango wa kutoa mafunzo
hayo kwa wakufunzi 200 wa walimu.
Swali: Vipi kuhusu ubora wa
mitihani inayotungwa na Necta, mnadhani inakidhi viwango?
Jibu: Ubora wa mitihani inayotungwa
na Baraza upo juu sana, hata usahihishaji wake ni wa hali ya juu. Mfumo wa kuwa
kila mwalimu anasahihisha swali lake ni wa kipekee na sisi tulikuwa kati ya
nchi za kwanza kuutumia.
Kuna nchi mtu anapewa burungutu la
mitihani ya watoto anakwenda nayo nyumbani kusahihisha akishamaliza analeta
majibu kisha watoto wanatangaziwa. Sisi mfumo wetu ni bora sana na sijui kwa
nini watu wanakuwa na mtazamo hasi na Necta. Sifa kubwa ya baraza lolote
lile la mitihani ni kutoa majibu yanayofanana na hali halisi ya elimu ilivyo.
Tunachotaka siku zote kuona ni mtu
anapewa kile anachostahili. Watu wengine wanasema mitihani inayotungwa na
kupewa watoto wote siyo sawa kwa sababu kuna baadhi ya shule walikuwa hawana
walimu au vitabu, sasa swali la kujiuliza nani alitakiwa kutoa hivyo vitabu?
Kwa vipi utunge mtihani mmoja useme
ni kwa ajili ya shule ambayo haina vitabu na walimu! Ni watoto gani ambao
tumewaandaa kwa sababu ya kwenda kwenye hizo shule?
Naona ni bora kabisa shule isiwepo
kama hakuna walimu na vitabu kwa sababu hii ndiyo roho ya elimu. Kukiwa na
walimu na vitabu watoto wanaweza kukaa hata chini ya mti na wakafundishwa na
kupata maarifa.
Necta tunatunga maswali kwa
kuzingatia vitu vingi na kutokana na suala la uwazi, kila swali linalotungwa
kuna sehemu tunaonyesha mada ambayo swali hilo lilipotolewa kwa mujibu wa
silabasi pia kuorodhesha baadhi ya vitabu vyenye mada hiyo, mpaka ukurasa tunaonyesha.
Hata Tume ya Waziri Mkuu walipokuja tuliwaonyesha vitu vyote hivyo.
Swali: Katika mkutano huu, baadhi ya
mambo yaliyozungumziwa ni pamoja na athari za siasa kuingizwa kwenye mitihani,
kwa upande wa Tanzania unazungumziaje hali hiyo?
Jibu: Tukiruhusu mitihani iingiliwe
na wanasiasa tutakuwa tunajimaliza wenyewe, kama ni wanasiasa wafanye kazi ya
kushauri halafu wawaache wanataaluma husika wafanye kazi yao, wanaohusika
na kutunga sheria watekeleze jukumu lao siyo kuingilia moja kwa moja suala
la mitihani.
Sisemi kuwa tuachwe tu tufanye kazi
kama tunavyotaka, ikibidi kuwe na chombo cha wanataaluma kiwe kinatukagua,
kwa sababu hii ni taaluma siyo kitu cha kila mtu kuingilia.
Madhara ya kuingilia mitihani
matokeo yake yataweza kuja kuonekana baada ya miaka hata 10 ijayo, ili kukwepa
hali hiyo kila mtu afanye kazi yake kama itaonekana watendaji hawana sifa
waondolewe wawekwe wengine wenye sifa.
Tukitaka kila mtu afaulu hata kama
hana sifa madhara yake yatakuja kuonekana kwenye suala la rasilimali watu,
mtu akipewa alama asizostahili na akawa mwalimu atawafundisha nini watoto? Hawa
ndiyo utakuta wana sababu zisizokwisha, kila siku utamsikia akisema watoto wa
siku hizi hawaelewi kabisa.
Pia hili suala la kusema kila kitu
tushirikishe wadau ni la kuangalia. Tusifike mahali tuambiwe tuwaulize watoto
tuwaletee maswali gani kwenye mtihani.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment