Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch
limechapisha ripoti inayoelezea mazingira magumu wanayokumbana nayo watoto
wanaojiingiza kwenye ajira ya uchimbaji madini nchini Tanzania, wengi wao
wakiathirika kiafya.
Ikiwa na kichwa cha habari kisemacho "Ajira ya Watoto
katika Migodi", ripoti hiyo imefichua vitendo vya dhuluma na ukatili
wanaokutana nao watoto wao ambao baadhi yao wako hatarini kuangukia kwenye
matatizo ya kiafya ikiwemo mtindio wa ubungo kutokana na kemikali
zinazokutikana kwenye machimbo hayo.
Ripoti hiyo iliyotangazwa leo jijini Dar es salaam inafuatia
utafiti uliofanyika katika maeneo ya machimbo ambako watoto wengi wameajiriwa.
Maafisa wa Human Rights Watch wamesema kuwa pamoja na
kutumika katika kazi ngumu ya utafutaji madini, lakini baadhi ya watoto hao
wanalazimika kutumika katika biashara za kingono na kukubwa na matukio ya
unyanyasaji wa kijinsia.
Ripoti hiyo ambayo pia imeangazia athari zitokanazo na matumizi
ya madini ya zebaki kwenye machimbo hayo, imesema kuwa baadhi ya kampuni
binafsi na vikundi vya watu huwatumia watoto hao kusaka madini jambo ambalo
linakwenda kinyume na sheria za kimataifa.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mtafiti mkuu wa Human Watch, Jenina
Morna, alisema kuwa idadi kubwa ya watoto hao hufanya kazi kwenye mazingira
magumu na wakati mwingine hulazimika kuingia kwenye mapango yaliyoko chini kwa
chini kwa ajili ya kusaka madini.
"Watoto hufanya kazi katika migodi yenye kina kirefu
mno, watoto hawa husafirisha mizigo mizito ya dhahabu, na wakati mwingine
hutumia vifaa hararishi kusaka madini kama vile mawe." Alisema Morna.
Moja ya sababu kubwa inayowasuma watoto wengi kuingia kwenye
migodi ni hali ya kipato duni iliyopo kwenye familia nyingi, kama
inavyothibitika katika makala fupi iliyoandaliwa na Human Watch ikionyesha kina
mama na watoto wakihangaika na maisha.
Kwa sasa Tanzania ni nchi ya tatu barani Afrika kwa
kuzalisha kwa wingi madini ya dhahabu, ikizidiwa na nchi za Afrika ya Kusini na
Ghana.
Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Josephat Charo
Mhariri: Josephat Charo
No comments:
Post a Comment