Arusha. Kikao cha Bunge la Afrika
Mashariki (EALA), jana kilivunjika kwa mara ya pili baada ya Wabunge wa
Tanzania, kutoka ndani ya ukumbi wakipinga kanuni kuvunjwa juzi.
Baada ya wabunge wa Tanzania kutoka
nje, Spika wa Bunge hilo, Margareth Zziwa aliahirisha Bunge kwa dakika 15 ili
kuweka mambo sawa, lakini jitihada za kuwashawishi ziligonga mwamba na kuamua
kuahirisha Bunge hadi leo.
Hata hivyo, Mbunge wa Tanzania,
Makongoro Nyerere hakuungana na wenzake kugoma kwani alibakia ukumbini na
kuungana na wabunge 32 wa Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda.
Awali, Mbunge Abdullah Ali Hassan
Mwinyi alitoa msimamo wa wabunge wa Tanzania kuwa walitoka, kupinga kitendo cha
wabunge wengine kudharau kiti cha Spika juzi na kutoka nje ili kushinikiza hoja
yao.
Mwinyi alisema ili kushinikiza
kuheshimiwa kiti cha Spika, wameamua kutoka nje ya ukumbi huo kwa kuonyesha
hawaungi mkono, tabia ya baadhi ya wabunge kushinikiza hoja zao, kujadiliwa na
Bunge hata kwa kukiuka kanuni na taratibu.
“Jana(juzi) ilikuwa ni mara ya pili
wenzetu, kudharau kiti cha Spika na kutaka kutoa hoja na kujadiliwa bila
kufuata kanuni, sasa tumeona ni vizuri na sisi kwa kupinga kuvunjwa kanuni,
tutoke ili kuonyesha tunapinga mchezo huu,” alisema Mwinyi.
Mwinyi alisema kitendo cha wabunge
wenzao kutoka nje ya ukumbi kwa kukataliwa kuvunja taratibu, kinadhalilisha
kiti cha Spika na hata wabunge wenyewe.
Mbunge mwingine wa Tanzania, Twaha
Taslima alisema kanuni zipo wazi kuwa kama mbunge ana hoja na kutaka Bunge
lijadili mambo ambayo si ya dharura ni lazima aiwasilishe saa 24 kabla kwa
Spika.
“Sasa jana(juzi), Mbunge wa Kenya,
Peter Mathuki alitaka hoja yake ya kutaka utaratibu wa kufanyika bunge kwa
mzunguko ijadiliwe kitu ambacho hakikuwa sahihi,” alisema Taslima.
Muthuki, juzi aliungwa mkono na nchi
zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), isipokuwa Tanzania.
Jana aliwasilisha hoja hiyo kwa
kufuata utaratibu lakini haikujadiliwa baada ya wabunge wa Tanzania kutoka nje.
Katika hoja hiyo, msimamo wa wabunge
wa Tanzania na Kamati ya Uongozi ya Bunge ni kuwa vikao vyote vifanyike katika
ukumbi wa Bunge, Arusha baada ya kukamilika.
Wabunge wa Tanzania ambao jana
walitoka ni Shyrose Bhanji, Profesa Nderakindo Kessy na Taslima. Wabunge wanne
hawakuwapo.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo,
kama wabunge watatu wa nchi moja, wakitoka nje kupinga jambo lolote basi kikao
kinaahirishwa kwa dakika 15 na wasiporejea bunge linaahirishwa.
Akizungumzia mgogoro huo, Ofisa
Habari wa EALA, Bobi Odiko alisema kilichotokea jana si ukiukwaji wa taratibu
na kuongeza kuwa ana imani mambo yatakuwa sawa na vikao vitaendelea leo kwa
amani.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment