Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), imesema itawafikisha kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge, Waziri
wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
akiwatuhumu kwa kulidanganya Bunge.
Hatua hiyo ilitangazwa jana na
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe baada ya kumhoji Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi, Balozi Herbert Mrango kuhusu hati ya mashaka waliyoipata kutoka kwa
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mwaka wa fedha 2011/2012.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kwenye
Bajeti ya mwaka huo kiasi cha Sh348,075,000,000 fedha za ndani zilizokuwa
zimetengwa chini ya fungu lililotajwa kuwa ni la mradi maalumu (Special Road
Construction Project) hazikutumiwa kwa malengo yaliyoelezwa bungeni.
“Ni vizuri leo uiambie kamati fedha
hizi ziliombwa kwa kitu gani na zilitumika kwa jambo gani. Tunajua kwamba fedha
hizi zilipunguzwa kiasi cha Sh95 bilioni na kupelekwa Wizara ya Uchukuzi,
zilibakia Sh252.975bilioni katika kifungu hicho lakini kuna bilioni 100
zimetumika visivyo,” alisema Zitto, ambaye pia ni Mbunge huyo wa Kigoma
Kaskazini (Chadema).
Alisema katika majumuisho ya Bajeti
ya wizara hiyo, Dk Magufuli na Dk Mwakyembe wakati huo akiwa Naibu Waziri wa
Ujenzi na Lukuvi walitoa maelezo yasiyo ya kweli bungeni kuhusu fedha.
Alikariri maneno yaliyorekodiwa
kwenye Hansard ya Bunge yaliyosemwa na viongozi hao watatu.
“Tunaomba fedha Sh252 bilioni kwa
ajili ya kuanzia kazi za ujenzi wa barabara,” Zitto alisema akikariri maneno ya
Dk Magufuli wakati anawasilisha bajeti.
“Fedha hizi zitachangia miradi ya
wafadhili,” haya yalikuwa maneno ya Dk Mwakyembe wakati akifanya majumuisho.
“Hizi ni fedha kwa ajili ya
counterpart fund,” alimkariri Lukuvi wakati akichangia hotuba ya wizara hiyo.
Zitto alisema CAG alihoji mwaka huu
kuhusu matumizi ya fedha hizo na alitoa taarifa akidai kuwa fedha hizo zilikuwa
miradi hewa na kasma kivuli.
Zitto alisema kuwa Dk Magufuli na
Katibu Mkuu wake walipohojiwa walidai kutumia fedha hizo kulipa madeni.
“Kwa nini mlidanganya Bunge? Mliomba
fedha za kuanza miradi maalumu. Hamkuomba fedha za madeni. Kwa nini mliunda
kasma kivuli na kuifuta baada ya pesa kulipwa?” Zitto alimhoji Balozi Mrango.
Katika majibu yake, Balozi Mrango
alisema kwa nia njema, fedha hizo zilitumika kuwalipa makandarasi waliokuwa
wamechachamaa, huku baadhi yao
wakisisitiza kusitisha kuendelea na miradi. Hivyo wakalazimika kuomba fedha kwa
njia hiyo ili miradi kuendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Zitto hakuridhishwa na majibu hayo
akisema hapakuwa na haja ya kutumia fedha hizo kuwalipa makandarasi wakati
kulikuwa na kasma yao
ya awali. Alisema kama kulikuwa na haja hiyo, wizara isingeita mradi rasmi.
“Jambo hili siyo sahihi hata kidogo
kulidanganya Bunge na hadi sasa wewe na waziri wako hamuonyeshi kukubali kosa
hili, hata Waziri Lukuvi naye alisisitiza bungeni kwamba fedha hizo zinaombwa
ili kutekeleza mradi maalumu lakini sasa imebainika sivyo, kwa mujibu wa Kanuni
za Bunge tutawafikisha kwenye Kamati ya Maadili ili wahojiwe nao wajieleze kwa
kulidanganya,” alisema Zitto.
Pia kamati hiyo imeitaka wizara hiyo
kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu matumizi ya Sh100 bilioni zilizotumika kinyume
na maombi yaliyowasilishwa kwenye Bajeti ya mwaka huo wa fedha.
CAG ameshauri madeni yote ambayo
Wizara ya Ujenzi inadaiwa yaorodheshwe ili yawe wazi kuepuka migongano katika
matumizi ya fedha.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Lukuvi
alisema haelewi chochote na kusisitiza kuwa akipata taarifa rasmi za Kamati ya
PAC, atatoa ufafanuzi.
Halmashauri zinavyotafuna mabilioni
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Serikali za Mitaa (LAACc), imeeleza namna mamilioni ya fedha za Serikali
zinavyoibwa kutoka Hazina kupitia halmashauri za wilaya huku Ilala ikitajwa
kuongoza kwa ufisadi huo.
Mwenyekiti wa LAAC, Rajab Mbarouk
Mohammed aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba Hazina imekuwa ikipeleka
fedha kwenye halmashauri zikiwa zimezidi na kwamba kiasi kinachozidi
hakirudishwi badala yake huliwa.
Alisema kamati hiyo imefanya
uchunguzi kwenye halmashauri 43 na kubaini kwamba mtindo huo ndiyo unaotumika
kuiba fedha za Serikali.
“Mwaka 2011/12 kiasi cha Sh1.5
bilioni zilipelekwa zikiwa zimezidi kwenye halmashauri hizo lakini
hazikurudishwa Hazina kama inavyoonyesha
kwenye ripoti ya CAG.
Alisema kati ya kiasi hicho,
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilipewa ziada ya Sh213 milioni ikifuatiwa na
Geita iliyopewa Sh129 milioni.
“Fedha hizo za mishahara zilipelekwa
kwenye halmashauri hizo na Hazina kimakosa zikiwa zimezidi lakini watendaji wa
hawakuzirudisha kama wanavyotakiwa kisheria
badala yake zikayeyuka,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa
uchunguzi huo pia ulibaini kwamba katika halmashauri hizo 43 kiasi cha Sh693
milioni hulipwa mishahara hewa ambayo wafanyakazi wake walishakufa na wengine
kustaafu.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya
Sengerema ililipa mishahara hewa yenye thamani ya Sh79.4 milioni ikifuatiwa na
Ukerewe iliyolipa Sh57.5 milioni.
Kwa upande wa fedha za miradi ya
maendeleo, mwaka 2011/12, Hazina ilipeleka katika Halmashauri ya Mbarali, Mbeya
Sh724 milioni kwa ajili ya Mradi wa Maendeleo ya Elimu Sekondari wakati mradi
huo ulikuwa ukihitaji Sh70 milioni tu.
“Kiasi cha Sh654 milioni zilipelekwa
kimakosa na Hazina lakini badala ya kurudishwa zilitumiwa katika mazingira ya kutatanisha,”
alisema.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya
Korogwe ilipelekewa ziada ya Sh500 milioni na Mvomero ilipewa Sh85 milioni.
“Kuna mtandao mkubwa wa Hazina na halmashauri ambao ukiachwa utaendelea
kupoteza fedha nyingi za walipakodi,” alisema.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment