Morogoro. Kiongozi wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda jana alisababisha kusimama kwa
shughuli za Serikali wilayani Morogoro baada ya ofisi kadhaa ikiwamo ya Mkuu wa
Wilaya na baadhi ya mitaa kufungwa ili kupisha kusikilizwa kwa kesi
inayomkabili katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.
Tofauti na Agosti 19, mwaka huu
wakati aliposafirishwa kwa helikopta, jana Sheikh Ponda alisafirishwa kwa
barabara kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro akiwa chini ya ulinzi.
Mbali ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Morogoro kufungwa, nyingine ni Hazina Ndogo, Madini, Posta, Vipimo, Ukaguzi na
Maktaba ya Mkoa.
Sababu za kufungwa kwa ofisi hizo
pamoja na Mtaa wa Stesheni na maeneo ya Posta ni kuwa jirani na Mahakama hiyo.
Magari yalizuiwa kutembea katika njia na maeneo ya karibu na ofisi pamoja na
Mahakama hiyo huku kukiwa na idadi kubwa ya askari polisi na magereza kwa muda
wote wa takriban saa mbili.
Alifikishwa mahakamani hapo saa 4:10
asubuhi akiwa katika basi la Magereza ambalo lilisindikizwa na jingine dogo,
huku magari mengine yakisimamishwa kupisha msafara huo. Mahakama hiyo ilifurika
umati wa wafuasi wa kiongozi kiasi cha kuwalazimu polisi na wana usalama
wengine kuweka utepe kuwazuia wengi wao kufika katika jengo lililokuwa
likitumika kuendesha kesi hiyo.
Shughuli katika eneo hilo zilirejea
katika hali yake ya kawaida saa 6:25 mchana baada kesi yake kuahirishwa na
msafara wa Sheikh Ponda kurejea katika Gereza la Segerea, Dar es Salaam ambako
yuko rumande.
Muda wote tangu kuwasili mpaka
kusikilizwa kwa kesi hiyo, wafuasi hao walikuwa kimya hadi pale ilipoahirishwa
na hasa baada ya Sheikh Ponda kuwapungia mkono alipokuwa akielekea kwenye basi
ambako walisikika wakisema: “Takbriir na kuitikia Allahu Akbar – (Mungu
Mkubwa).”
Kesi yenyewe
Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali,
Benard Kongola alisema mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro,
Richard Kabate kuwa Sheikh Ponda alitenda makosa ya uchochezi Agosti 10, mwaka
huu saa 11.45 jioni kwenye maeneo ya Kiwanja cha Ndege, Morogoro.
Alisema siku hiyo, Sheikh Ponda
alialikwa kutoa maelezo machache kwenye Kongamano la Eid lililoandaliwa na
Umoja wa Wahadhiri Mkoa wa Morogoro (Uwamo) na kwamba akiwa hapo alitamka
maneno: “Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za
misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata),
ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na
kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni
milango na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana,” huku akijua kutoa
maneno hayo ni kosa kisheria.
Alisema kwa kufanya hivyo, Sheikh
Ponda anayetetewa na mawakili watatu wanaoongozwa na Juma Nassoro, alivunja
masharti ya Mahakama ya kifungo cha nje iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu ya Mei 9, mwaka huu iliyokuwa imetamka kuhubiri amani.
Katika shtaka la pili, Sheikh Ponda
anadaiwa kuwashawishi wafuasi wake kutenda kosa la jinai kwa kuwaambia:
Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na
gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi
wake ni Waislamu, lakini haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo waliokataa
Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa
sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.” Shtaka la tatu ni kudaiwa
kutamka maneno yaliyoumiza imani ya watu wengine kama yalivyo katika shtaka la
pili.
Baada ya kusoma mashtaka hayo,
Kongola alisema walikuwa na mashahidi 15 na vielelezo vitatu ambavyo ni DVD
mbili na kibali kilichotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro(OCD), Agosti
Mosi, 2013 cha kongamano husika na hati ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya
Kisutu, Mei 9, 2013.
Baada ya kusomewa, Sheikh Ponda
alikana mashtaka yote matatu huku akikubali kuwemo kwenye kongamano hilo.
Alikiri kukamatwa na polisi Agosti 11, Dar es Salaam.
Wakili wa utetezi, Nassor
aliwasilisha ombi la dhamana kwa mteja akisema mashtaka hayo yote kisheria yana
dhamana. Pia aliwasilisha ombi la kupatiwa hati yenye maelezo ya mlalamikaji
ambaye ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani alisema kuwa kutokana na upelelezi
upande wa mashtaka kukamilika, wanahitaji maelezo hayo kwa ajili ya kuandaa
utetezi.
Hata hivyo, Wakili Kongola aliiomba
Mahakama kutompa dhamana mshtakiwa kutokana na cheti kilichotolewa na
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kupinga dhamana ya mshtakiwa huyo kwa masilahi ya
usalama wa nchi.
Akitoa mwongozo wa maombi
yaliyowasilishwa na pande zote mbili, Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi
Septemba 11, mwaka huu itakapotajwa tena na kwamba Septemba 17, mwaka huu
Mahakama itatoa uamuzi endapo mshtakiwa atapewa dhamana au la wakati
itakapoanza kusikilizwa.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment