Dodoma. Suala la kutimuliwa kwa
madiwani wanane wa CCM katika Manispaa ya Bukoba limeingia sura mpya baada ya
Kamati Kuu kuwazuia Meya, Dk Anatory Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi
Khamis Kagasheki kushiriki katika siasa mkoani humo hadi mwaka 2015.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya
kikao hicho zinaeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika mgogoro wa
viongozi hao, unakiumiza chama katika jimbo hilo.
Taarifa zilidai chanzo cha ugomvi
kati ya Balozi Kagasheki na Dk Amani, ni kwa kila mmoja kutaka kugombea nafasi
ya ubunge Jimbo la Bukoba mjini katika uchaguzi ujao. Na kwa uamuzi huo,
Kagasheki na Dk Amani hawatashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hata hivyo, akitangaza uamuzi huo
jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema
viongozi hao watakutana na Kamati Kuu leo na baada ya hapo utatangazwa uamuzi
uliofikiwa.
Mbali na meya na mbunge huyo ambaye
pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, wengine walioitwa katika kikao hicho cha
leo ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Costansia Buhinye, katibu wake, Averin
Mushi pamoja na mwenyekiti wa chama Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na katibu
wake, Janath Kayanda.
Kutokana na uamuzi huo, Kamati Kuu
ambayo ilimaliza kikao chake saa 8:30 usiku wa kuamkia jana italazimika kukaa
tena leo kuwaelezea uamuzi uliofikia.
Kumekuwapo na mgogoro mkubwa katika
Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, ukimuhusisha Kagasheki na baadhi ya
madiwani kwa upande mmoja; na Dk Amani na kundi jingine la madiwani kwa upande
mwingine.
Wakati wa mgogoro huo madiwani
wamekuwa wakituhumiana ufisadi, na CCM imekwishawatuma viongozi wake wa juu
kuingilia kati mgogoro huo akiwamo mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, lakini
hakuna mafanikio yaliyopatikana.
Kufikishwa kwenye Kamati Kuu kwa
suala hilo kumekuja baada ya uongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kuamua kuwatimua
uanachama madiwani hao, hatua ambayo ilikuwa inahatarisha nafasi zao na hivyo
kukiingiza chama hicho kwenye uchaguzi mdogo.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo
zinasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa viongozi hao kuwajibishwa kwa kukiuka
kanuni, kwa kuwa upo uamuzi wa chama unaokataza viongozi waliochaguliwa katika
vyombo vya dola kuwajibishwa kwa staili hiyo.
Madiwani waliovuliwa uanachama na
kata zao katika mabano ni pamoja na Richard Gaspar (Miembeni ), Murungi
Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya
(Buhembe) na Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai).
Wengine ni Deusdedit Mutakyahwa
(Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na Dauda
Kalumuna (Ijuganyondo).
Baada ya kutimuliwa Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema chama Mkoa wa Kagera hawana uwezo wa
kuvua uanachama na kwamba wenye uwezo huo ni ngazi ya taifa.
Nape alisema kwa mujibu wa taratibu
za CCM, Mkoa wa Kagera walitakiwa kuwasilisha tuhuma hizo ngazi za juu ili
zijadiliwe na kuamuliwa na Kamati Kuu (CC).
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa
taratibu, viongozi wa kuchaguliwa na wananchi kama wabunge na madiwani,
hawawezi kuvuliwa uanachama na vikao vya chini bali chombo chenye mamlaka hayo
ni Kamati Kuu.
Hata hivyo, siku moja baada ya tamko
hilo la Nape, CCM mkoani Kagera kilisisitiza kuwa uamuzi wa kuwafukuza madiwani
hao ni halali, kwa kuwa ulifanywa na kikao halali kwa mujibu wa katiba na
kanuni za chama hicho.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera,
Costansia Buhiye, alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho, hakuna
kikao chochote ndani ya chama kinachoweza kukinzana na kikao kingine kwa hivyo,
bado madiwani hao wamefutiwa dhamana ya uanachama kama mkoa ulivyoamua.
Buhiye alisema kikao cha Halmashauri
Kuu ya Mkoa ndicho kikao kikuu chenye uamuzi wa kumwajibisha mwanachama yeyote,
iwapo atabainika kwenda kinyume cha taratibu na kanuni za chama, kwa mujibu wa
katiba ya CCM.
Suala la Mansour
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu
imelipeleka suala la kutimuliwa uanachama kwa Mwakilishi wa Kiembesamaki
Zanzibar, Mansour Yusuf Himid kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambako litajadiliwa
leo na kutolewa uamuzi.
Nape alisema mamlaka ya mwisho ya
kumteua mwakilishi ni NEC, hivyo lisingeweza kujadiliwa na Kamati Kuu.
Chanzo: www.mwananchi.com
No comments:
Post a Comment