Dodoma. Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi
(CC-CCM) kimeiomba Serikali kumtuma Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), Ludovick Utouh kwenda Bukoba, Kagera kuchunguza tuhuma dhidi ya
Meya wa Manispaa hiyo, Dk Anatory Aman.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana mjini Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema
kamati hiyo imewaagiza Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki na Dk Aman
kurudisha utulivu wa kisiasa katika Manispaa hiyo ambayo katika siku za
karibuni imekuwa na mgogoro mkubwa.
Alisema Kamati Kuu inaamini kuwa kwa
CAG kwenda Bukoba kutasaidia kujulikana kwa mambo anayolalamikiwa ili ukweli
ujulikane na hatua stahiki zichukuliwe.
Alisema CAG ametakiwa kwenda haraka
Bukoba na uchunguzi unatakiwa kufanyika katika kipindi cha muda mfupi kuanzia
jana.
“Hivi ninavyozungumza ama CAG
ameondoka kuelekea Bukoba au yuko katika maandalizi ya kwenda Bukoba kufanya
uchunguzi huo na ukweli utajulikana. Hatuna hofu juu ya kwenda CAG maana katika
kikao hiki yupo Waziri Mkuu na vyombo vingine kwa hiyo wamewasiliana naye,”
alisema Nape.
Nape alisema wamelazimika kuitaka
Serikali kumtuma CAG kwa kuwa tume iliyotangulia iliyomhusisha Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Abbas Kandoro na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi haikuwa ya
kiuchunguzi, bali ilishughulikia suala la migogoro.
Alisema kuwa taarifa ya uchunguzi huo
inapaswa kupelekwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba
ili waijadili na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa
halmashauri hiyo.
Dk Aman anapingwa kutokana na hatua yake
ya kuanzisha miradi ya kupima viwanja vya Mji wa Bukoba, ukarabati wa soko na
ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ambayo inadaiwa kuwa na harufu ya ufisadi.
Madiwani wapeta
Akizungumzia kubatilishwa kwa uamuzi
wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Kagera wa kuwafukuza uanachama madiwani
wanane wa Manispaa ya Bukoba, Nape alisema uamuzi huo ulikiuka Katiba ya CCM ya
mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.
Alitaja kifungu kilichokiukwa kuwa ni
Ibara ya 93 (15) ambacho kinataka CC kujulishwa uamuzi huo kabla ya kuchukuliwa
kwa hatua hiyo.
“Kamati Kuu inawataka madiwani wa CCM
wa Manispaa ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba na Meya wa Manispaa hiyo kurudisha
utulivu katika halmashauri yao. Pia kurudisha mshikamano katika chama ili Ilani
ya CCM itekelezwe kama ilivyokusudiwa,” alisema Nape.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment