Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi
wa makatibu wakuu kumi na mmoja na naibu makatibu wakuu 14 wapya katika wizara
mbalimbali.
Miongoni mwa walioteuliwa ni Katibu
Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Sifuni Mchome ambaye
sasa anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na aliyekuwa
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deodatus Mtasiwa ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu,
Tamisemi.
Mtasiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni walisimamishwa kazi na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda Februari, mwaka jana kupisha uchunguzi dhidi yao, kutokana
na kukithiri kwa migomo ya madaktari nchini, pamoja na utendaji wao
kulalamikiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema: “Mtasiwa ameteuliwa kwa kuwa
uchunguzi dhidi yake haujaonyesha kuwa ana kosa lolote, lakini wenzake (Nyoni)
na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo bado
wanachunguzwa.
Katika uteuzi huo, aliyekuwa Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo amehamishiwa Ikulu kusimamia Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN), kuwa Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha
na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo.
Makatibu wakuu walioachwa kwa maelezo
kuwa watapangiwa kazi nyingine ni Sethi Kamuhanda (aliyekuwa Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo), Kijakazi Mtengwa (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na
Watoto) na Omary Chambo (Uchukuzi), huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa akistaafu wa hiari.
Balozi Sefue alisema Rais Kikwete
ameanzisha kitengo kipya katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), kitakachokuwa
kikishughulikia afya ambacho kitasimamiwa na Dk Mtasiwa.
Aidha, aliwataja makatibu wakuu
waliohamishwa wizara kuwa ni Florens Turuka kutoka Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu na Joyce Mapunjo kutoka Viwanda na
Biashara kwenda Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Makatibu wakuu wapya
Alisema Jumanne Sagini ambaye alikuwa
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu
wa wizara hiyo.
Dk Servacius Likwelile ambaye alikuwa
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Dk Patrick Makungu ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano,
Sayansi na Tekinolojia pia ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu (Tamisemi), Alfayo Kidata ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Dk Shaaban Mwinjaka aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara
ya Uchukuzi. Uledi Mussa ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano
wa Afrika Mashariki ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na
Masoko.
Charles Pallangyo aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu sasa anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya.
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
Anna Maembe ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Sihaba Nkinga ambaye alikuwa Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni ameteuliwa kuwa Katibu
Mkuu wa wizara hiyo na Sophia Kaduma ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika pia ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Naibu makatibu wakuu wapya
Naibu makatibu wakuu wapya wizara zao
katika mabano ni Angelina Madete (Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira), Regina
Kikuli (Ofisi ya Waziri Mkuu), Zuberi Samataba (Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi
anayeshughulika na Elimu), Edwin Kiliba (Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi), Dk
Yamungu Kayandabila (Kilimo, Chakula na Ushirika), Profesa Adolf Mkenda
(Fedha-Sera), Dorothy Mwanyika (Fedha-Fedha za Nje na Madeni), Rose Shelukindo
(Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Dk Selassie Mayunga (Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi), Monica Mwamunyange (Uchukuzi).
Consolata Mgimba (Elimu na Mafunzo ya
Ufundi), Profesa Elisante ole Laizer (Habari, Utamaduni na Michezo) na Armantius
Msole (Ushirikiano wa Afrika Mashariki).
Waliohamishwa
Naibu makatibu wakuu waliohamishwa ni
John Mngodo (Uchukuzi kwenda Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Selestine
Gesimba (Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwenda Wizara ya Maliasili na
Utalii).
Injinia Ngosi Mwihava (Ofisi ya
Makamu wa Rais kwenda Wizara ya Nishati na Madini), Maria Bilia (Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi kwenda Viwanda na Biashara na Nuru Milao (Maliasili na
Utalii kwenda Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto).
Aidha, Dk Donaldo Mbando
amethibitishwa kuwa Mganga Mkuu wa Serikali baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu
kusimamishwa kwa Dk Mtasiwa.
SOURCE: www.mwananchi.com
No comments:
Post a Comment