Arusha na Dar. Wakati Tanzania
ikisema kuwa iko tayari kukaa meza moja na jirani yake Rwanda kumaliza hali ya
uhasama iliyoanza kujitokeza katika siku za hivi karibuni, Katibu Mkuu wa
Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk Richard Sezibera amesema
jitihada za kidipolomasia zinafanyika kutatua tofauti hizo za kimawazo.
Bila kutaja taasisi wala wanaohusika
katika jitihada hizo za kidiplomasia, Dk Sezibera aliwaambia waandishi wa
habari jijini Arusha jana kuwa jitihada hizo zinafanyika kimya kimya bila
kushirikisha vyombo vya habari “Migongano na tofauti za kimtazamo miongoni mwa
viongozi wakuu wa nchi wanachama wa EAC ni jambo lisilo la afya kwa Jumuiya na
linastahili kushughulikiwa kidiplomasia,” alisema Dk Sezibera.
Akizungumza kwa tahadhari kubwa
kukwepa kuingia kwa undani kuhusu suala hilo, Katibu Mkuu huyo alisema inafaa
kila linalowezekana lifanyike kutatua mgongano wowote unaotokea kati ya
viongozi wakuu.
Mjini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe naye alisema katika mahojiano
kuwa iwapo Rwanda itaomba kukutana na Tanzania kwa ajili ya kumaliza mzozo huo
Serikali itakuwa tayari kutoa ushirikiano.
“Tanzania tunaona kuwa hii itakuwa
njia ya busara zaidi kumaliza tofauti zetu kwa njia ya mazungumzo badala ya
kuendelea kuishi kwa uhasama” alisema Membe na kwamba hali ya ujirani mwema na
tofauti zetu tuzimalize kwa njia ya mazungumzo.”
Waziri Membe alisema siyo jambo la
busara kuacha mzozo huo ukakaamuliwa na mataifa ya nje ili hali nchi zenyewe
bado zinafursa nzuri ya kukaa mezani na kujadiliana namna ya kutafutia ufumbuzi
mzozo huo.
Uhusiano wa Tanzania na Rwanda
unatajwa kuwa katika wakati mgumu kutokana na kauli za majibizano baina ya
viongozi wa pande zote mbili. Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete aliisihi Rwanda
kutotoa kauli za kejeli kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha uhusiano
uliodumu kwa muda mrefu .
Hata hivyo, Dk Sezibera alisema
tofauti na migongano kati ya viongozi haiwezi kuathiri wala kuvunja Jumuiya ya
sasa ya Afrika Mashariki kama ilivyotokea kwenye Jumuiya ya awali mwaka 1977
kutokana utofauti wa muundo na misingi ya Jumuiya ya sasa.
“Jambo lililo dhahiri ni kwamba
tofauti za kimtazamo kati ya viongozi wa nchi wanachama (Kikwete na Kagame),
haziwezi kuhatarisha uhai wa Jumuiya ya Afrika Mashairiki kwa sababu muungano
huu umejengwa katika muundo na misingi imara tofauti na ule (jumuiya) wa
zamani,” alisema Dk Sezibera
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment