Vyombo vya usalama nchini Misri
vimeanzisha operesheni kubwa kuwatawanya wafuasi wa rais aliyepinduliwa,
Mohamed Mursi kutoka kambi mbili kubwa mjini Cairo. Watu zaidi ya 43 wameuawa katika
ghasia zilizofuata.
Operesheni hiyo imeanza muda mfupi
baada ya mapambazuko alfajiri ya leo. Maafisa wa usalama walizizingira kambi za
Rabaa al-Adawiya na al-Nahda, ambazo ziko katika maeneo tofauti ya mji mkuu Cairo, wakisindikizwa na
tingatinga. Watu waliokuwepo wameliambia shirika la habari la AFP kuwa
wanajeshi walitumia magari maalum kuwamwagia waandamanaji maji ya kuwasha, na
vile vile walirusha mabomu ya kutoa machozi. Kwa mujibu wa mashahidi hao,
mashambulizi hayo yaliwaweka waandamanaji katika hali ya mkanyagano.
Katika upande mmoja wa kambi,
yalikuwepo makabiliano baina ya waandamanaji na maafisa wa usalama, ambayo
yalifuatiwa na milio ya risasi, ambazo imethibitika zilifyatuliwa na polisi.
Picha za televisheni zimeonyesha watu waliojeruhiwa wakiwa wanakimbizwa katika
vituo vya dharura vya matibabu, na polisi waliokuwa wakiwaburura waandamanaji
waliokaidi kuondoka.
Polisi imeshutumiwa kutumia nguvu
kupindukia kupambana na waandamanaji Polisi imeshutumiwa kutumia nguvu
kupindukia kupambana na waandamanaji
Nguvu kupita kiasi
Waandamanaji wameilaumu polisi
kutumia nguvu kubwa kupita kiasi, katika kuwatawanya.
''Mashambulizi yalikuwa ya ghasia
kubwa. Polisi imetumia mabomu ya kutoa machozi, risasi za moto na za mpira, na
aina zote za ukandamizaji kujaribu kuwatimua waandamanaji. Watu wamepoteza
maisha yao.''
Alisema mmoja wa waandamanaji.
Kwa mujibu wa tangazo la wizara ya
ndani ya Misri, tayari polisi imeweza kuwaondoa kabisa waandamanaji kutoka
kambi ndogo ya katika viwanja vya al-Nahda. Vile vile afisa mmoja wa usalama
ameiambia AFP kuwa watu kadhaa wanaomuunga mkono Mursi wamekamatwa kwa msaada
wa wakazi wa maeneo jirani. Miongoni mwa hao waliokamatwa wameonekana wakiwa
wamechuchumaa chini, wakizingirwa na maafisa wa usalama.
Aidha, vituo vya televisheni
vimeonyesha familia za watu waliokuwa wamekita kambi katika uwanja wa al-Nahda,
miongoni mwao wakiwemo watoto na wanawake, wakiwa wanauhama uwanja huo,
wakisindikizwa na polisi.
Udugu wa kiislamu wakaza kamba
Hakuna dalili kuwa wafuasi wa Mursi
wanasalimu amri Hakuna dalili kuwa wafuasi wa Mursi wanasalimu amri
Huku hayo yakijiri, kundi la udugu wa
kiislamu la Mohamed Mursi limewataka wafuasi zaidi kujimwaga mitaani, kulaani
kile wanachokiita ''mauaji ya halaiki''. Msemaji wa kundi hilo Gehad al-Haddad amesema kupitia mtandao
wa kijamii wa Twitter, kuwa kinachoendelea sio juhudi za kuwatawanya
waandamanaji, bali jaribio la kunyamazisha sauti ya upinzani dhidi ya mapinduzi
ya kijeshi.
Msemaji huyo hali kadhalika alisema
kuwa watu 250 wamekwishauawa, na wengine zaidi ya 500 wamejeruhiwa.
Mwandishi wa shirika la habari la AFP
amesema amehesabu maiti 43 kwenye kituo cha muda cha kuhifadhia maiti katika
eneo la Rabaa al-Adawiya, na kuongeza kuwa wengi wa marehemu walionekana kuuawa
kwa risasi. Mwandishi huyo amesema hakuona maiti za watoto, wala za wanawake.
Viongozi wa waandamanaji watiwa
mbaroni
Wizara ya mambo ya ndani ya Misri,
imesema kuwa maafisa wawili wa polisi pia wameuawa. Wizara hiyo pia imearifu
kuwa viongozi kadhaa wa udugu wa kiislamu wametiwa mbaroni, lakini hawakutaja
majina yao.
Taarifa za hivi karibuni zinaeleza
kuwa waandamanaji wanaomuunga mkono Mohamed Mursi wameshambuliana na vikosi vya
usalama katika miji ya Minya na Assiut, ambako kanisa la madhehebu ya Koptiki
limechomwa moto.
Hatua hii ya serikali ya mpito
kuingilia kati kuwatawanya waandamanaji imechukuliwa saa chache baada ya
Marekani kuitolea wito kujizuia kufanya hivyo, na kuitaka kuwaruhusu wapinzani
kuandamana kwa uhuru. Umoja wa Ulaya umeitaka serikali mjini Cairo kujizuia.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE/APE
Mhariri:Josephat Charo
SOURCE: http://www.dw.de/idhaa-ya-kiswahili
No comments:
Post a Comment