Dodoma. Historia inatarajia kuandikwa
katika Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano unaoanza leo, mjini Dodoma
wakati litakaposafisha njia kwa Watanzania kwa mara ya kwanza, kupiga kura ya
maoni ya Katiba.
Bunge litajadili Muswada wa Sheria ya
Kura ya Maoni 2013, ambao ndiyo utakaotoa njia kwa Watanzania kuamua Katiba
Mpya baada ya Bunge la Katiba kumaliza kazi yake.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa
Tanzania Bara kupiga kura ya
maoni ya aina yoyote ile tangu Uhuru
mwaka 1961 na ya pili kwa Zanzibar ambayo ilifanya hivyo kwa mara ya kwanza
mwaka 2010 kutoa nafasi ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kuelekea mchakato huo wa Katiba Mpya,
Bunge pia litajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba wa mwaka 2013.
Hatua hiyo inatokana na safari ndefu
ya mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi iliyoanza Aprili 13, mwaka jana
kwa Rais Jakaya Kikwete kuzindua Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji
Joseph Warioba.
Juni 3, mwaka huu, Jaji Warioba
alizindua Rasimu ya Katiba baada ya mchakato huo na kuruhusu uundwaji wa
Mabaraza ya Katiba kwa kutegemea makundi maalumu ambayo mchakato wake unamalizika
Agosti 31, mwaka huu.
Baada ya hatua hiyo, Bunge
litapelekewa maboresho ya mapendekezo ya rasimu hiyo na kuyajadili ikiwamo
kupitisha sheria ya mabadiliko hayo na baadaye kuweka muundo wa sheria na
muundo wa kupigiwa kura hatua itakayofuata katika Bunge la Katiba baadaye
Novemba, mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na
Ofisi ya Bunge, hoja hizo mbili zimetengewa siku tano kuanzia Septemba 9 hadi
13, mwaka huu na mjadala wa marekebisho hayo unatarajiwa kuchukua nafasi hasa
kwa wabunge wa pande mbili, CCM cha Chadema juu ya kutengeneza muundo.
Chadema, kimeshatoa baadhi ya
mapendekezo yake katika muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba na Kura ya Maoni ikiwamo kupinga Rais kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu
wasiotokana na Bunge na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment