Jeshi la Polisi limeingia katika
kashfa nzito baada ya mkuu wake, Inspekta Jenerali Said Mwema, kuibiwa upanga
wa dhahabu ambao ni mali ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi za
Kusini mwa Afrika (SARPCCO).
Upanga huo wenye uzito wa takriban
kilo tatu na wenye thamani ya zaidi ya fedha za Tanzania Sh600 milioni, ni
kielelezo kwa nchi inayokabidhiwa uongozi wa SARPCCO.
Mwaka jana Tanzania ilikuwa
mwenyekiti wa SARPCCO, ambapo upanga huo ulikabidhiwa kwa IGP Mwema na Jenerali
Magwashi Victoria ‘Riah’ Phiyega, ambaye ni Kamishna wa Taifa wa Polisi wa
Afrika Kusini aliyekuwa amemaliza muda wake kwa wakati huo.
Hilo ni tukio la pili la wizi la mali
zinazohusu ofisi ya IGP, ambapo mwaka jana ndani ya ofisi hiyo kuliibwa
kompyuta ndogo (laptop), ikiwa na taarifa muhimu za kipolisi. Hadi sasa hakuna
taarifa za kupatikana kwa kompyuta hiyo.
IGP Mwema alikabidhiwa upanga huo
Septemba 5, 2012, katika mkutano saba wa SARPCCO uliofanyika Zanzibar na
kuhudhuriwa na wakuu wa majeshi ya Polisi kutoka nchi 13, pamoja na mashirika
ya kimataifa.
Upanga huo ambao unakwenda sambamba
na bendera ya SARPCCO, ni moja ya vielelezo vya nchi iliyochaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa shirikisho hilo, ambaye moja kwa moja anakuwa ni Mkuu wa Jeshi la
Polisi katika nchi husika.
Kwa mujibu wa taratibu za SARPCCO,
vielelezo hivyo hutakiwa kuwekwa ofisini kwa kiongozi husika, ikiwa ni alama ya
kila mgeni atakayeingia ofisini hapo kutambua uwepo wa wadhifa huo wa
kimataifa.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini
kuwa IGP aligundua kutoweka kwa upanga huo wiki iliyopita, wakati akijiandaa
kwenda kuukabidhi kwa mwenyekiti mpya wa SARPCCO, ambaye ni IGP wa Namibia.
Taarifa za ndani ya jeshi hilo
zilibaini kuwa, IGP alilazimika kuondoka bila upanga huo alipokwenda Namibia
wiki iliyopita kuhudhuria mkutano wa nane wa SARPCCO, uliofanyika Jumapili
iliyopita mjini Windhoek.
Kwa mujibu wa uchunguzi, IGP Mwema
alikabidhi upanga unaofanana na huo ambao siyo wa dhahabu, alioazimwa kutoka
kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia, Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali
Sebastian Ndeitunga, na kukabidhiwa kama ishara ya kukabidhiwa uenyekiti wa
SARPCCO kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Uchunguzi ulibaini kuwa IGP Mwema
alitoa ahadi ya kurejesha upanga halisi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, au
Serikali ya Tanzania italazimika kutengeneza mwingine kulipa uliopotea.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha
kuwa kashfa hiyo ametupiwa Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa
pamoja na dereva wake, ikidaiwa kuwa upanga huo baada ya kupokewa na IGP Mwema,
Septemba mwaka jana uliwekwa kwenye gari la kamishna huyo.
Kamishna Mussa ndiye alikuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Saba, na pia ofisa mwenyeji
kwa wajumbe wa mkutano huo uliofanyika Zanzibar.
Hata hivyo, taarifa zingine zilidai
kuwa IGP Mwema naye analaumiwa kwa kutofuatilia kwa karibu zana za kazi, kwani
baada ya kuupokea alitakiwa kuhakikisha unakuwepo ofisini kwake kama alama ya
uenyekiti wake.
Gazeti hili lilipowasiliana kwa njia
ya simu na Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa kuhusu madai hayo
alisema, kitara (upanga) hicho ni kweli kimepotea, lakini yeye hahusiki kwa
kuwa kila kitu kina utaratibu wake.
“Ni kweli kitara kilikabidhiwa kwa
afande IGP na mimi nilishuhudia kikikabidhiwa, na ni kweli kitara hakijulikani
kiliko, lakini mimi sihusiki na kupotea kwake. Ni kweli mimi nilikuwa ofisa
mwenyeji wa mkutano huo, lakini siku hiyo zilitolewa zawadi nyingi, watu
walipewa mikoba, kwa hiyo mtu akipoteza mkoba wake niulizwe mimi?” alihoji
Kamishna Mussa.
Alisema kila kitu kina utaratibu wake
na kwamba taarifa kwamba yeye amehojiwa kutokana na upotevu wa kitara hicho au
kuna kamati imeundwa, hazina ukweli.
“Sijawahi kuona kamati hiyo. Kamati
hiyo kwanza imeundwa na nani na inatoka wapi? Hayo maneno yanatengenezwa na
watu wa nje,” alisema Kamishna Mussa.
Alisema kinachofanyika hivi sasa ni
kukitafuta ili kiweze kurejeshwa kunakohusika.
Taarifa zingine zilidai hata bendera
ya mezani ya mwenyekiti wa SARPCCO, aliyokabidhiwa sambamba na upanga huo nayo
kuna hatihati ilipotea.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini,
Advera Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema aulizwe kamishina wa
polisi Zanzibar.
“Suala hilo muulize Kamishina wa
Zanzibar ndiye anayejua,” alisema Senso.
Uchunguzi unaonyesha kuwa maofisa
katika ofisi ya IGP na ile ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, wamehojiwa akiwamo
Kamishna Mussa, na kwamba upelelezi mkubwa umekuwa ukiendelea ndani ya jeshi
hilo.
Hata hivyo, juhudi za gazeti hili za
kutaka kufahamu uamuzi wa SARPCCO katika ofisi yake ya uratibu iliyopo kwenye
ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Polisi wa Kimataifa (INTERPOL), Harare,
Zimbabwe, hazikuzaa matunda baada ya baruapepe iliyotumwa kwa ofisa mratibu wa
SARPCCO ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya Kanda ya INTERPOL, C. Simfukwe kutopata
majibu.
No comments:
Post a Comment