Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu (PAC), Zitto Kabwe.
Serikali hupoteza zaidi ya Sh700
bilioni kwa mwaka kutokana na utaratibu wa kukusanya mapato kwa kutumia
stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono.
Taarifa iliyotolewa jana na
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu (PAC), Zitto Kabwe imesema kwa sasa
Serikali hukusanya Sh741 bilioni kwa mapato yasiyo ya kikodi ambayo ni nusu tu
ya mapato ambayo Serikali ingestahili kupata.
Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini (Chadema), ameishauri Serikali itumie risiti za elektroniki kwa
kukusanya maduhuli.
"Utaratibu wa kutumia risiti za
elektroniki utaongeza maradufu mapato ya Serikali na kuifanya kuachana na
mtindo wa kupandisha kodi kwenye bidhaa muhimu kwa wananchi.
"Uamuzi wa Kamati za Bunge za
Hesabu wa kuitaka Serikali kukusanya maduhuli yake kwa kutumia risiti za
elektroniki unapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania," ilisema taarifa
hiyo ya Zitto.
Alisema walipitia mpango wa Serikali
na kugundua kuwa mapato yasiyo ya kikodi yamekadiriwa kuwa ni Sh741 bilioni
kutoka wizara, idara na mikoa.
"Serikali inapata Sh383 bilioni
kutoka kwenye halmashauri za wilaya, miji na manispaa. Hatukuweza kupata mapato
ya mashirika ya umma maana hayaletwi kwenye Bajeti za Serikali," alisema.
Wizara zinazoongoza kwa mapato
(mapato kwenye mabano ni Nishati na Madini (Sh220 bilioni), Fedha (Sh126
bilioni), Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (Sh100 bilioni), Maliasili na
Utalii (Sh84 bilioni), Mambo ya Ndani (Uhamiaji Sh92 bilioni na Usalama
Barabarani Sh17 bilioni), Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (Sh19 bilioni), Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (Sh16 bilioni).
Hata hivyo, Zitto alisema mapato ya
Serikali yameongezeka kwa asilimia 60 kutoka Sh500 bilioni mpaka Sh800 bilioni.
Maazimio
Pia kamati tatu zinazosimamia hesabu
za Serikali zimetoa maazimio 14 baada ya kumalizika kwa mafunzo yaliyofanyika
Bagamoyo wiki iliyopita.
Kamati hizo za PAC, Bajeti na ile ya
Serikali za Mitaa (LAAC), zimeagiza kuwapo kwa mkutano kati ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Hazina, Hesabu za Bunge, Benki Kuu ya
Tanzania
(BoT), ili kupata usahihi wa deni la taifa.
Pia kamati hizo zimesema kuna umuhimu
wa kuandaa mkutano wa kutathmini mafanikio na changamoto za mfumo wa bajeti ya
mwaka huu na kukutana na maofisa masuuli hatarishi (risk based) ili kutathmini
utendaji wao.
Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na
Bunge na Tamisemi zimetakiwa kuanza kuratibu mikutano na mafunzo ya wakurugenzi
wa halmashauri na kuanzishwa kwa mfumo wa kutunza kumbukumbu za hesabu na
nyaraka mbalimbali katika Serikali Kuu na halmashauri.
"Kamati zimetaka CAG akague mara
kwa mara sehemu zote zenye matatizo, pia wametaka taarifa za mwaka za kamati za
Bunge ziwe na kipengele cha kiwango cha utekelezaji wa mapendekezo ya kamati
yaliyotolewa awali.
"Pia mikataba katika ngazi ya
Serikali za Mitaa iandikwe kwa Kiswahili. Serikali inatakiwa kufanya jitihada
za ziada kuzalisha wataalamu wa fani ya ununuzi na bajeti ya Bunge iongezwe
kupitia Mfuko wa Bunge na iwasilishwe bungeni na Naibu Spika na siyo Ofisi ya
Waziri Mkuu," iliongeza taarifa hiyo.
Kamati hizo pia zimeitaka Serikali
iandae mjadala wa kitaifa wa kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana na vitendo vya
rushwa na mmomonyoko wa maadili na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma iweke
uwazi wa kutangaza umiliki wa mali za viongozi.
Pia kamati hizo zimetaka Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha
askari wa usalama barabarani wanatumia utaratibu wa kisasa wa kutoa risiti za
malipo za elektroniki. Ofisi za Serikali zifanye ununuzi wake kwa
wafanyabiashara wanaotumia mashine za kielektroniki pekee.
TRA pia imetakiwa kuhamasisha
wananchi na wafanyabiashara umuhimu wa matumizi ya risiti za elektroniki na
Serikali idhibiti kampuni za uwakala wa kupakia na kupakua mizigo.
Kamati hizo pia zimeshauri Sheria ya
Kupambana na Utakatishaji wa Fedha ya 2006 irekebishwe ili iweke viwango vya
fedha ambazo mtu anaweza kuingia au kutoka nazo nchini bila kuzitaja.
Source: www.mjengwablog.co.tz
No comments:
Post a Comment