Dar es Salaam. Wajumbe wa Baraza la Katiba la
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, wametaka kipengele cha Mahakama ya
Kadhi kiwekwe kwenye Katiba Mpya.
Amiri Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya
na Taasisi za Kiislam, Sheikh Mussa Kundecha, alisema jana kuwa ingawa rasimu
ya Katiba haina kupengele hicho, lakini wao wanaona hiyo ni haki yao.
“Tunataka kipengele cha Mahakama ya
Kadhi kiwekwe Katiba Mpya na iendeshwe na kugharamiwa na Serikali,”
alisema Sheikh Kundecha wakati wajumbe hao walipokuwa wakijadili rasimu ya
Katiba.
Alisema Waislamu wengi waliotoa maoni
yao kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walitaka kuwapo kwa mahakama hiyo
lakini cha kushangaza tume hiyo iliyatupa.
“Sasa licha ya kwamba kipengele hicho
hakipo kwenye rasimu, bado tunaendelea na kilio chetu cha kutaka kiwekwe,”
alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, wiki iliyopita alisema kipengele
ambacho hakipo kwenye rasimu hakitawekwa kwenye Katiba Mpya.
Sheikh Kundecha alihoji iweje kuwe na
Mahakama za Biashara inazoendeshwa na Serikali, wakati kuna Watanzania wachache
ambao ni wafanyabiashara.
“Kuna wafanyabiashara wachache lakini
wana mahakama yao, kunakuwa na ugumu gani kuweka Mahakama ya Kadhi kwa
ajili ya Waislamu?” alihoji Kundecha. Mwaka jana, Serikali iliruhusu kuanzishwa
kwa Mahakama ya Kadhi ambayo iko nje ya mfumo wa Serikali.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment