Kiingilio cha chini kwenye mechi ya
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Simba na Yanga itakayochezwa Jumamosi (Oktoba
20 mwaka huu) kitakuwa sh. 5,000. Kiingilio hicho ni kwa viti vya rangi ya
kijani ambavyo ni 19,648.
Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu
kiingilio ni sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000, VIP C
kiingilio ni sh. 15,000, VIP B itakuwa sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748
tu tiketi moja itapatikana kwa sh. 30,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja
kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni katika vituo mbalimbali.
Vituo hivyo ni Shule ya Sekondari
Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora,
Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, na
BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.
Mechi hiyo namba 63 itachezeshwa na
Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam, ambapo atasaidiwa na Hamis Changwalu wa Dar
es Salaam pia, na Ferdinand Chacha wa Bukoba. Mwamuzi wa akiba ni Oden Mbaga wa
Dar es Salaam.
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa John
Kiteve kutoka Iringa wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Stanley
Lugenge wa Njombe.
MECHI TATU FDL ZASOGEZWA MBELE
Mechi tatu za Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) katika kundi A na C zimesogezwa mbele kutokana na viwanja vya Kambarage,
Shinyanga na Nangwanda Sijaona, Mtwara kuwa na shughuli nyingine za kijamii.
Katika kundi A, mechi kati ya Ndanda
na Transit Camp iliyokuwa ichezwe Oktoba 19 mwaka huu sasa itafanyika Oktoba 21
mwaka huu kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Stand United na JKT Kanembwa
zilizokuwa zicheze Oktoba 19 mwaka huu, sasa mechi hiyo ya kundi C itafanyika
Novemba 2 mwaka huu Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Nayo mechi ya Mwadui
na Polisi Dodoma iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo Oktoba 26 mwaka huu
imesogezwa hadi Novemba 3 mwaka huu.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)
No comments:
Post a Comment