Viongozi katika mkutano wa kilele wa
Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa,
Ethiopia,
wametaka kesi inayoendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu - ICC dhidi
ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta icheleweshwe
Haya yanajiri baada ya viongozi hao
wa Afrika kulalamika kuwa mahakama ya ICC inalilenga tu bara la Afrika katika
kesi zake. Rais Kenyatta pamoja na naibu wake William Ruto, wanakabiliwa na
mashitaka ya uhalifu wa kivita kuhusiana na machafuko yaliyofuatia uchaguzi
mkuu uliokuwa wa utata wa mwaka wa 2007, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na
wengine wengi kuwachwa bila makao. Kesi ya Kenyatta inatarajiwa kuanza mwezi
ujao wa Novemba.
Umoja wa Afrika pia umeunga mkono
azimio linalosema kuwa hakuna kiongozi yeyote wa nchi barani Afrika atakayefika
katika mahakama ya kimataifa. Suala la kujiondoa kutoka ICC pia lilijadiliwa
katika mkutano huo wa kilele mjini Addis
Ababa, lakini halikuungwa mkono kwa kutosha.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia
ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza kuu la AU, Tedros Adhamom Ghebreyesus,
amesema AU haina mamlaka ya kumzuia kiongozi wa taifa kushitakiwa mjini The
Hague, ikiwa ni pamoja na Kenyatta, lakini nchi za Afrika zinapanga kuwasiliana
na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka kesi ya Kenyatta icheleweshwe
kabla ya mashitaka yake kuanza rasmi mnamo Novemba 12.
Baraza la Usalama lina mamlaka ya
kuamuru kesi hiyo kucheleweshwa kwa mwaka mmoja, lakini kama hilo litafanyika au la, ndio suali kuu. Kesi
haijawahi kucheleweshwa hapo kabla. Ghebreyesus amesema kama uamuzi huo
hautachukuliwa, basi AU itaomba kesi dhidi ya Kenyatta iahirishwe, na kama hilo halitafanyika, basi
viongozi wa Afrika wataamua kuwa Kenyatta hastahili kufikishwa katika mahakama
hiyo mjini The Hague.
Uamuzi huo uliofanywa katika siku ya
mwisho ya mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi wa Umoja wa Afrika ulikuwa wa
kauli moja, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn. Kenyatta
na Rais wa Sudan Omar al-Bashir ambaye pia anatakiwa kwa uhalifu wa kivita,
walihudhuria kikao hicho.
Kilio kutoka makundi ya haki za
binaadamu
Hatua hiyo ya AU maramoja
ilishutumiwa na makundi ya kutetea haki za binaadamu, kutoka Kenya na pia ya
kimataifa. Naibu mkurugenzi mkuu wa Tume ya Kutetea Haki za Binaadamu nchini Kenya – KHRC Davis Malombe anasema wito wa
kutaka kesi hiyo icheleweshwe “ni jaribio jengine la kuvuruga na kuchelewesha
haki kwa waathiriwa wa Kenya
na unasaliti madai ya ahadi ya AU ya kupambana na ukwepaji sheria“.
Baada ya kuwasili mjini Addis Ababa, Ethiopia kabla ya kikao, Kenyatta
alitoa hotuba iliyokuwa na maneno makali, akiishutumu ICC kuwa wakala wa himaya
ya kibeberu inayosambaratika. Alisema “Hata ingawa tuliongozwa na kudhibitiwa
na mabeberu na maslahi ya kikoloni katika miaka iliyopita,sasa sisi ni mataifa
yenye fahari, na yaliyo na uhuru . Zaidi ya yote, hatima yetu iko mikononi
mwetu. Na wakati huo huo, zaidi kuliko yote, ni muhimu kwetu kuwa macho dhidi
ya mifumo inayoendelea kuwekwa na watu wa nje, wenye nia ya kuidhibiti hatima
hiyo”.
Rais huyo wa Kenya aliupongeza Umoja wa Afrika kwa kumuunga
mkono akisema “kama Rais wa Kenya,
inanipa hisia za kina za majivuno ya kudumu kujua kuwa ninaweza kuutegemea
Umoja wa Afrika, kunisikiliza na kunisaidia wakati wa matatizo. Afrika daima
imesimama na mimi”. Bunge la Kenya
tayari limepitisha mswada unaoitaka nchi hiyo ijiondoe kutoka ICC.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Abdu Mtullya
No comments:
Post a Comment