Monday, October 14, 2013

SIMULIZI YA HAYATI BABA WA TAIFA MWALIMU NYERERE



WAKATI taifa likiadhimisha miaka 14 baada ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, mmoja wa wateule wake amefichua siri kwamba kabla ya uhuru, Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta alilala baharini kumwombea aitawale Tanganyika.
Akizungumza na Tanzania Daima nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mzee Iddi Nhende alitoboa siri hiyo akisema kuwa ndiyo maana utawala wa Nyerere uliogopwa na watu wengi duniani.

Kwa mujibu wa mzee huyo wa miaka 81, siku tatu kabla ya kupandishwa kwa bendera ya uhuru wa Tanganyika, Kenyatta ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha African National Union (KANU), alikuwa akilala baharini mbele ya jengo la Ikulu.

“Ilikuwa ikifika saa mbili usiku watu wote tuliokuwa naye tunabeba mikeka na soda tunakwenda kulala ufukweni mbele ya jengo la Ikulu. Tulikuwa tunatandika mikeka yetu, anayetaka anakunywa soda na Kenyatta analala katikati… kushoto na kulia wanalala wale wajukuu zake wa kike.

“Hapo anauchapa usingizi hadi saa sita usiku, akawa ananiambia muda huo ukifika nimpige mateke kwenye unyayo ili kumuamsha… sio jambo rahisi kwa mlinzi kumpiga teke bosi wake, lakini Kenyatta alikuwa jeuri bwana (anasema kwa msisitizo na mshangao).

“Basi nikawa nafanya hivyo, akiamka tu anatuambia tukunje suruali zetu tuingie baharini kumwombea Nyerere ili atawale vizuri Tanganyika, tukawa tunaingia kwenye maji hadi usawa wa magoti, anachukua usinga wake na kuanza kutumwagia maji vichwani,” alisema mzee Nhende.

Kuhusu utawala wa Nyerere, alisema watumishi wa serikali walifunzwa ujamaa, kupendana kwa dhati na kuheshimiana huku akisisitiza kwamba haikuwa rahisi kufanya hujuma kama ilivyo sasa.

Alisema hivi sasa wananchi wamechoshwa na rushwa iliyomea mizizi kwenye wizara, idara, taasisi na mashirika ya umma, na kubainisha kwamba wachache wanaopata nafasi wanazitumia vibaya bila kujali maslahi ya Watanzania wengine.

Mzee huyo anaiomba serikali kuwarejeshea heshima ya taifa watu wake na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kupunguza pengo kati ya masikini na tajiri alilodai ndiyo chanzo cha maovu yanayoendelea sasa. (Kwa maelezo zaidi soma makala ya mzee huyo ukurasa wa 14)

Lembeli alipuka
Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), amesema kuwa Watanzania wanavuna walichopanda baada ya kumdhalilisha na hatimaye kuzika mema yote aliyowaachia Nyerere.

Lembeli alitoa kauli hiyo wakati akitoa maoni yake juu ya kumbukumbu ya miaka 14 baada ya kifo cha muasisi huyo, akisema kuwa Azimio la Arusha, miiko ya uongozi, misingi ya umoja vimezikwa na kuruhusu rushwa kutamalaki, ikiwa ni pamoja na kuifanya fedha kuwa kigezo katika kusaka uongozi.

“Nchi yetu sasa inakabiliwa na fujo, wizi, ujangili, Watanzania kubaguana kwa misingi ya dini, kabila na hata rangi, rasilimali za taifa kutoroshwa na kukithiri kwa ufukara. Tumeruhusu makundi yasiyo halali ya kibepari kujipenyeza ndani ya jamii, hivyo kuvuruga kabisa ustaarabu aliotuachia Nyerere,” alisema.

Kwa mujibu wa Lembeli, wananchi wote pamoja na viongozi wanatakiwa kutubu mbele za Mungu kutokana na kuyazika mema aliyowaachia Nyerere.

No comments: