Wednesday, October 16, 2013

Anas al-Liby akanusha mashitaka US



Anas Al-Liby aliyekamatwa na wanajeshi wa Marekani mjini Tripoli kwa kuhusika na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya balozi za Marekani mwaka 1998 amekausha madai ya ugaidi dhidi yake.

Abu Anas al-Liby, ambaye jina lake halisi ni Nazih Abdul-Hamed al-Ruqai, alikanusha madai dhidi yake kupitia kwa wakili wake.
Anatuhumiwa kwa kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la al-Qaeda na kupanga mashambulizi ya kigaidi dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998.

Watu zaidi ya 220 walipoteza maisha yao.
Bwana Liby, mwenye umri wa miaka 49, alisemekana kuwa na kesi ya kujibu mwaka 2000.
Siku ya Jumanne Liby alionekana akiwa amefungwa pingu mkononi katika mahakama moja mjini New York.

Liby, alisikiza kwa maakini jaji akimusomea mashitaka dhidi yake .
Baadaye alikanusha madai hayo dhidi yake na jaji akaakhirisha kesi hiyo hadi Oktoba 22.
Mshukiwa aliondoshwa mahakamani baada ya jaji kusema muwa lazima aendelee kuzuiliwa kwani kuna tisho la yeye kutoroka.

Kumekuwa na ghadhabu nchini Libya tangu makomando wa Marekani kumkamata al Liby anayedaiwa kuwa mmoja wa viongozi wa kundi la Al Qaeda mjini Tripoli mapema mwezi Oktoba.

Wengi walikiona kitendo hicho kama cha kutoheshimu uhuru wa Libya.
Hata hivyo Marekani kupitia kwa waziri wake wa mambo ya nje John Kerry imesema kuwa Liby alikuwa mshukiwa halali aliyepaswa kukamatwa.
Hata hivyo serikali ya Libya baada ya kukamatwa kwa Liby ilimtaka balozi wa Marekani nchini humo kueleza kwa nini ilifanya hivyo

Waziri mkuu wa Libya Al Zeydan ambaye alitekwa nyara kwa masaa kadhaa siku chache baada ya Al Libya kukamatwa, alisema kuwa wahalifu wenye uraia wa Libya wanapaswa tu kushitakiwa na kuhukumiwa ndani ya nchi hiyo
Majasusi walimuhoji Libya kwenye mali ya kijeshi kwa wiki moja kabla ya kumpeleka mahakamani huku wanawe wakisema kuwa serikali ilihusika katika kukamatwa kwake, madai ambayo serikali imekanusha.
Chanzo: BBC

No comments: