Sunday, April 6, 2014

UKAWA kuvunja Bunge

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) umetishia kuvunja Bunge Maalumu la Katiba iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaendelea kutumia rasimu yake badala ya kutumia rasimu ya pili iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Msimamo huo ulitolewa jana katika kongamano la wananchi wa Dar es Salaam ambalo lilihutubiwa na makatibu wakuu wa vyama vya siasa vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF, ambavyo vinaunda UKAWA katika ukumbi wa Land Mark jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika ukumbi huo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema UKAWA wapo tayari kususia au kuvunjika kwa Bunge la Katiba endapo CCM wataendelea kutumia rasimu yao.

Alisema hivi sasa CCM wanafanya hila za kuhujumu rasimu iliyotolewa na Warioba kwa kutoa rushwa kwa baadhi ya wajumbe wasikubaliane na mambo mengi yaliyopo kwenye rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Dk. Slaa alisema UKAWA watafikia hatua ya kuvunja au kususia vikao vya Bunge endapo CCM itakataa kurejesha dokezo la rasimu halisi ya pili ya Jaji Warioba lenye kifungu 1 hadi 6 kinachojadili masuala ya utawala na muundo wa Muungano.

Alisema UKAWA haitakiwi kuzembea katika hatua hiyo ya awali, kwa kuwa kifungu 1 hadi 6 ndio msingi mzima wa Katiba mpya inayotakiwa kupatikana, bila hivyo hakuna katiba.

Dk. Slaa alisema wajumbe hao wanatumia fursa ya kuingia na rasimu ya CCM ili kuendeleza  upotoshaji huo baada ya kufundishwa na Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge ambapo aliitumia fursa hiyo kuwapa semina ya kutumia rasimu yao ya CCM.

“Upotoshaji uliofanywa na Rais Kikwete wakati analihutubia bunge na baadaye kukutana nao ndio unaoendelea mpaka sasa … UKAWA hawawezi kuvumilia hilo kwa sababu wapo kwa ajili ya wananchi na si CCM,” alisema Dk. Slaa.

Alisema Rais Kikwete aliitumia nafasi hiyo vibaya kama Amiri Jeshi Mkuu kwa kulichochea Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi kwamba serikali tatu zinaweza kufanya nchi isitawalike, unaweza kutumia gharama kubwa na hata kama nchi itakopa kwa ajili ya kuziendesha, itashindwa kulipa.

“Ndugu zangu hizo ni hoja dhaifu sana, alipaswa azifafanue ni namna gani nchi itashindwa kutawalika wakati wananchi wenyewe waliyatoa maoni hayo ambayo sasa yanafanyiwa kazi … nia yake ilikuwa ni kulichochea jeshi na wananchi wayachukue maoni yao,” alisema Dk. Slaa.

Dk. Slaa alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 ulikuwa wa hiari na si huu wa sasa wa katiba mpya unaolazimishwa na CCM kwa nguvu na njama nyingu ambazo zote zimegunduliwa.

“Hakuna mwenye nia ya kuvunja Muungano wetu … hapa kinachotafutwa ni namna gani maridhiano yatafikiwa baina ya pande mbili kulingana na maoni ya wananchi wenyewe waliyoyatoa katika mchakato wa awali, ili katiba mpya ya kuongoza vizazi na vizazi ipatikane,” alisema.

Alitoa mfano wa nchi ya Uingereza ambayo iliungana kwa hiari na nchi nyingine nyingi za bara hilo kwa zaidi ya miaka 500, lakini hivi sasa nchi ya Scotland inafanya mchakato wa kujiondoa katika muungano huo, alidai hivyo ndivyo makubaliano katika suala la Muungano wa Tanzania unapaswa kuwa.

Dk. Slaa alimtaka Rais Kikwete kutoa majibu kwa wananchi kuhusu muungano tuliokuwa nao sasa kama ni wa nchi moja yenye serikali mbili au nchi mbili zenye serikali mbili, ndipo aendelee kuwachochea watu wake kuhusu serikali mbili anazozitaka.

“Kama mwaka 2010 CCM ilifanya marekebisho namba 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa kuifanya Zanzibar iwe nchi kamili, hivyo kuwa nchi mbili zenye serikali mbili … Katiba ya Muungano ya 1977 pamoja na marekebisho haiyatambui,” alisema.

Alisema kama anataka hivyo, ni vema akaitisha maoni ya wananchi wa Zanzibar kukubali au kukataa  serikali mbili na nchi mbili pamoja na masharti yatakayowekwa kwa maandishi na sivyo ilivyo sasa.

Alisisitiza kwamba kinachofanywa sasa na UKAWA ni wananchi na nchi kupata Katiba yao na si ya matakwa ya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na vyama vingine vya siasa.

Naye Katibu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, alimtaka Rais Kikwete kurekebisha hadharani maneno aliyoyatoa katika hotuba yake ili kuondoa hofu na mkanganyiko kwa wananchii na vikosi vya ulinzi na usalama kuhusu mchakato wa katiba mpya.

“Hofu na mkanganyiko iliyojengeka ni lazima ibadilishwe na viongozi wa CCM, hasa Rais Kikwete …ili wananchi tusiamini kuwa matokeo yoyote ya katiba mpya yana madhara,” alisema Nyambabe.

Nyambabe alisema ili kuziba ombwe la uongozi wa CCM na serikali, UKAWA ndani na nje ya bunge inatakiwa kuonyesha dira/njia bora ya kupata katiba mpya kwa amani na utulivu.

“UKAWA nje ya Bunge tunasisitiza kwamba maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya katiba mpya yaheshimiwe …tunasisitiza kwamba katiba bora itapatikana kwa maridhiano na si mivutano na kutunishiana misuli,” alisema.

Naye Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa CUF,  Julius Mtatiro, aliwataka wananchi wawaamini wajumbe wa UKAWA waliopo katika Bunge Maalumu kuwa wanafanya kazi kwa masilahi ya nchi.

Mtatiro alisema wajumbe wa CCM watatumia mbinu na hila kuingiza mambo yao, lakini mwisho wa hayo ni wiki ijayo, ambapo watafanya uamuzi wa kutoka bungeni.

“Tunawaomba wananchi mfuatilie bunge wiki ijayo … tusipotimiziwa yale ambayo wananchi wanayataka katika katiba yao inayozungumzia serikali tatu, jiandaeni kutupokea,” alisema Mtatiro huku akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo.

Chanzo: Tanzania Daima

No comments: