Tuesday, April 1, 2014

MICHEZONI: Kipigo cha Yanga: Ni mkono wa Mtu

Michael Balou (kulia) akijiandaa kuwatoka viungo wa Simba, Jonas Mkude (namba20) na Henry Joseph katika mechi ya Ligi Kuu Bara, jana Jumapili. Simba ilifungwa mabao 2-1 na kusalia kwenye nafasi yake ya nne katika msimamo wa Bara. 


KIPIGO cha mabao 2-1 ilichokipata Yanga jana Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga mbele ya Mgambo JKT, kimewashitua mashabiki wa timu hiyo ambao walikuwa wakidai kwamba kuna mkono wa mtu.

Mashabiki hao ambao wengi wao walitoka Dar es Salaam,  walichanganyikiwa zaidi baada kusikia Azam FC imeipiga Simba mabao 2-1 jijini Dar es Salaam na kuwaacha kwa pengo la pointi saba kileleni katika mbio za kuelekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Azam imetimiza pointi pointi 53 ambazo zimewaweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya kwanza tangu iasisiwe Juni 24, 2007.

Yanga imebaki kwenye nafasi ya pili na pointi 46 huku Mbeya City ikifikisha pointi 45 na kuzidi kujikita nafasi ya tatu baada ya kuilaza Prisons bao 1-0 pia jana Jumapili na kufufua matumaini ya kuwania nafasi ya pili.

Pointi 53 zinaweza kufikiwa na Yanga au Mbeya City pekee. Matokeo ya Azam na Simba, yanawafanya Wekundu wa Msimbazi kubaki nafasi ya nne na pointi zao 36 baada ya mechi 23.

Katika mchezo huo wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, hali ya hewa ya mawingu na mvua nyepesi iliwazuia mashabiki wengi kufika uwanjani kwa hofu ya mvua.

Mashabiki wengi wa Yanga walionekana kuiunga mkono Simba ili iweze kushinda na kuiwekea kiwingu Azam isiweze kuendelea kujikita kileleni, lakini mambo yalienda kinyume.

Lakini cha kushangaza mashabiki wa Simba walikuwa hawashangilii timu yao inaposhambulia au hata ilipopiga bao la kusawazisha kwa madai kwamba walikuwa hawataki kuinyooshea njia Yanga.

Iliwachukua Azam dakika 16 kupata bao la kwanza lililofungwa na Khamis Mcha baada ya mpira uliopigwa na Kipre Tchetche kuelekea langoni mwa Simba kurudi uwanjani na wachezaji wa Simba beki Joseph Owino na Amissi Tambwe walijichanganya katika kuokoa,   ndipo Mcha alipofunga.

Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha Simba ambao walilishambulia lango la Azam mara kwa mara huku wakimtumia zaidi winga, Uhuru Selemani ambaye alikuwa akionyeshana kazi na beki, Gadiel Michael.

Inawezekana haikuwa bahati ya Simba, kwani dakika ya 26 Uhuru alikosa bao la wazi akishindwa kumalizia pasi safi ya Ramadhan Singano ‘Messi’. Kipa wa Azam, Aishi Manula, aliuwahi mpira na kuokoa.

Messi alipiga mpira kwa juu dakika ya 31 akiwa ndani ya eneo la hatari la Azam, lakini Tambwe alipiga kichwa kilichotoka nje ya lango. Hata hivyo, Azam waliamka na kufanya shambulizi kali dakika ya 33 baada ya Tchetche kupiga kupiga krosi safi iliyomkuta Mcha ambaye alipiga nje.

Simba ilipata bao la kusawazisha dakika ya 45 lililofungwa kwa kichwa na Owino akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na William Gallas kutoka nje eneo la hatari la Azam. Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko.

Azam walikianza kipindi cha pili kwa kasi na kufika langoni mwa Simba mara kadhaa na dakika ya 56 ikafunga bao la pili kupitia John Bocco. Bocco alifunga akimalizia mpira uliogonga mwamba na kurudi uwanjani ambao ulipigwa na Gadiel.

Simba ilicharuka baada ya Azam kupata bao hilo huku ikimtumia zaidi Uhuru kuanzisha mashambulizi, lakini harakati zake ziliishia kupiga krosi ambazo zilikosa waunganishaji.

Azam ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Mcha na kuingia Kelvin Friday wakati Simba iliwatoa Messi, Henry Joseph na Harun Chanongo na nafasi zao zilichukuliwa na Ibrahim Twaha, Abdulhalim Humud na Awadh Juma.

Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo hayo na kumfanya Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic, kutoamini macho yake kwa kipigo hicho huku timu yake ikionekana kuimarika.

“Tumecheza vizuri lakini hatukutumia vyema nafasi sita za mabao ya wazi, naamini tumecheza vizuri kwa asilimia zaidi ya 60, makosa ya mabeki ndiyo yaliyotugharimu,” alisema Logarusic.

Kocha wa Azam, James Omog alisema: “Nimefurahi kuwa ushindi huu, ni kama nilivyosema awali kuwa lengo letu ni kushinda kila mechi iliyo mbele yangu.”

Mgambo yaisimamisha Yanga

Yanga imejiweka katika nafasi ngumu ya kutetea ubingwa wake kwa kipigo cha jana Jumapili mjini Tanga. Yanga imecheza mechi 22. Mgambo yenyewe imejiimarisha katika kuhakikisha haishuki daraja kwa kufikisha pointi 22, ijapokuwa imeng’ang’ania nafasi yao ya 11.

Bao la kwanza la Mgambo lilifungwa dakika ya kwanza na Fully Maganga ambaye alitumia vyema makosa ya kipa wa Yanga, Juma Kaseja na beki Kelvin Yondani waliojichanganya wakati wakirudishiana mpira. Mfungaji aliugonga na kufunga kirahisi.

Yanga ilijitahidi kutafuta bao la kusawazisha, lakini kila mbinu yake haikufanya kazi ipasavyo na Mgambo kwenda mapumziko ikiwa mbele.

Yanga ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 53 kwa njia ya penalti baada ya beki wa Mgambo, Novart Lufungu, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari. Penalti hiyo ilifungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Mgambo ikafunga la pili dakika ya 65 kwa penalti iliyopigwa na Malimi Busungu. Penalti hiyo ilisababishwa na beki Kelvin Yondani kumvuta jezi mchezaji mmoja wa Mgambo. Katika mchezo huo, mchezaji wa Mgambo Mohamed Neto alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 30 baada ya mwamuzi Alex Mahaji kumhisi amevaa nguo zaidi ya moja wakati wa mchezo.

Awali Neto alikuwa na kadi ya njano baada ya kumchezea faulo mchezaji wa Yanga. Baadhi ya mashabiki walihusisha uvaaji wa mchezaji huyo na imani za kishirikina wakiamini kuna kitu.

Mbeya City mwendo mdundo

Kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mbeya City ilitumia dakika mbili tu kuinyoosha Prisons kwa kuilaza bao 1-0. Bao pekee la Mbeya City lilifungwa na Paul Nonga dakika ya pili baada ya Mbeya City kufanya shambulizi la kushitukiza langoni mwa Prisons.

Mabeki wa Prisons na viungo wake walikuwa wamepanda kushambulia, lakini walijisahau kurudi haraka kuzuia ndipo Nonga alipofunga.

Kwa kipigo hicho, Prisons imebaki nafasi ya 10 ikiwa na pointi 22.

JKT Ruvu yaizima Rhino

Rhino Rangers ya Tabora imezidi kujiweka katika mazingira ya hatari ya kushuka daraja baada ya kufungwa mabao 3-1 na JKT Ruvu katika mechi iliyopigwa  Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Mbagala, Dar es Salaam.

Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) bado ipo mkiani mwa ligi hiyo ikiwa na pointi 13 katika mechi 23 ilizocheza.

JKT Ruvu ipo nafasi ya tisa ikifikisha pointi 28 katika mechi 23 ilizocheza.

Mabao ya JKT yalifungwa na Idd Mbaga dakika 24, Emmanuel Swita dakika 34 kwa njia ya penalti baada ya Sosthenes Manyasi kuangushwa eneo la hatari. Bao la tatu la JKT lilifungwa na Samwel Kanute dakika ya 82.

Bao pekee la Rhino lilifungwa dakika ya 48 kwa njia ya penalti na Jerome Gervais baada ya Omary Mtaki wa JKT kumchezea rafu Rajab Twaha.  

Mtibwa yaimaliza Coastal Union

Mtibwa Sugar iliutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani wa Manungu uliopo Turiani, Morogoro baada ya kuifunga Coastal Union mabao 3-1. Mabao ya Mtibwa yalifungwa na Mussa Mgosi, Mohammed Mkopi na Jamal Mnyate. Bao pekee la Coastal lilifungwa na Behewa Sembwana.

Katika mchezo mwingine uliochezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar ilitoka suluhu na Ruvu Shooting.

Chanzo: Mwanaspoti

No comments: